Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya nadhiri ni maneno Yake (Ta´ala):

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا

“Ambao wanatimiza nadhiri zao na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea.” (al-Insaan 76 : 07)

MAELEZO

Dalili inayofahamisha kuwa nadhiri ni katika ´ibaadah ni maneno Yake (Ta´ala):

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا

“Ambao wanatimiza nadhiri zao na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea.”

Dalili katika Aayah hapa ni kwamba Allaah amewasifu kwa kutekeleza kwao nadhiri, jambo ambalo ni dalili inayoonyesha kwamba Allaah anapenda kitendo hicho. Kila kitendo ambacho kinapendwa na Allaah huzingatiwa kuwa ni ´ibaadah. Hilo linatiliwa nguvu zaidi na maneno Yake (Ta´ala):

وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا

“… na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea.”

Tambua kuwa aina mbalimbali za nadhiri ambazo Allaah (Ta´ala) amewasifu kwazo watu hawa wenye kuzitekeleza ni zile aina za ´ibaadah ambazo Allaah (´Azza wa Jall) amezifaradhisha. Mtu akianza kufanya ´ibaadah ambayo ni ya lazima, basi anatakiwa kuitimiza. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ

“Kisha waondoshe takataka zao na watimize nadhiri zao na watufu katika Nyumba ya kale.” (al-Hajj 22 : 29)

Nadhiri inayohusiana na mtu kujilazimisha jambo fulani au kumtii Allaah, lisilokuwa la wajibu, imechukizwa. Baadhi ya wanachuoni wamesema pia ya kwamba ni haramu kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu kuweka nadhiri na akasema:

“Hakika haileti kheri, isipokuwa tu inatoka kwa mtu ambaye ni bakhili.”[1]

Pamoja na hivyo mtu akiweka nadhiri ya kumtii Allaah, basi italazimika kuitekeleza. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuweka nadhiri ya kumtii Allaah, basi amtii.”[2]

Kwa kufupiza ni kwamba ´ibaadah zote ambazo ni faradhi huitwa “nadhiri”. Ama kuhusu nadhiri ambazo ni maalum ni ile ambayo mtu anailazimisha nafsi yake jambo kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Wanachuoni wameigawanya nadhiri maalum katika vipengele vingi na imetajwa kwa undani zaidi katika vitabu vya Fiqh.

[1]  al-Bukhaari (6608), Muslim (1639), Ahmad (2/61), Abu Daawuud (3277), at-Tirmidhiy (1578), an-Nasaa´iy (3810), Ibn Maajah (2122) na ad-Daarimiy (2340).

[2] al-Bukhaariy (6696) na (6670), Ahmad (6/36), Abu Daawuud (3279), at-Tirmidhiy (1564), an-Nasaa´iy (3816) na (3817), Ibn Maajah  (2126) na Maalik (983).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 67
  • Imechapishwa: 28/05/2020