45. Yuko karibu na mtu kuliko mshipa wa shingoni mwake

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Amemuumba mtu na anajua kile nafsi yake inamnong´oneza; na Yeye yuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake. Hakuna jani linalodondoka chini isipokuwa analijua wala punje katika giza la ardhi wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika kitabu kinachobainisha.

MAELEZO

Anajua yale mtu anayofikiria kabla hajayazungumza. Allaah yuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni. Ukaribu huu hauna maana ya mchanganyiko. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko karibu kwa ujuzi Wake. Ukaribu Wake kwa waja ni kwa njia ya kuwazunguka na utambuzi, na si kwa njia ya kuchanganyikana nao.

Kitabu kinachobainisha ni Ubao uliohifadhiwa. Kila kitu kimeandikwa katika Ubao uliohifadhiwa. Allaah alianza kukijua kila kitu, kisha baadaye akakiandika. Kuamini Qadar kuna nguzo nne:

1 – Allaah alikijua kila kitu kwa elimu Yake ya milele na isyokuwa na kikomo.

2 – Kisha Allaah akakiandika kila kitu katika Ubao uliohifadhiwa.

3 – Pale anapotaka kitu kiwe basi kinakuwa:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika si venginevyo amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.”[1]

4 – Baada ya kukitaka kitu basi hukiumba.

[1] 36:82

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 38
  • Imechapishwa: 28/07/2021