45. Mwenye busara na kuwasamehe kwake watu

1 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alikuja bwana mmoja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi ninao ndugu ambao ninawaunga ilihali wao wananikata, wananifanyia mabaya ilihali mimi nawafanyia mazuri na wananifanyia ujinga na mimi nawafanyia upole. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mambo yakiwa hivo ulivosema basi ni kama vile unawanyunyizia majivu yenye kuweka. Utaendelea kuwa na msaidizi kutoka kwa Allaah muda wa kuwa uko hivyo.

2 – Ni lazima kwa mwenye busara kuizoweza nafsi yake kuwasamehe watu wote na kuacha kulipiza mabaya. Hakuna kitu kinachotuliza mkabala mbaya kama mkabala mwema. Hakuna kitu kinachofanya mkabala mbaya kukua na kuwaka moto kama kisasi.

3 – Ayyuub amesema:

“Mwanamme hatokuwa mtukufu mpaka awe na sifa mbili; kuvipa kisogo vile vilivyoko mikononi mwa watu na kuwasamehe.”

4 – ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz amesema:

“Vitu anavopend zaidi Allaah ni vitatu; kusamehe licha ya kuwa na nguvu, ukatikati wakati wa uwezo na upole wakati wa ´ibaadah. Hakuna yeyote ambaye atakuwa mpole kwa mwengine duniani isipokuwa Allaah atamfanyia upole siku ya Qiyaamah.”

5 – Ni wajibu kwa aliye na busara kupuuzilia mbali kila aliyemfanyia mabaya kwa kutaraji Allaah amsamehe kwa uhalifu wake aliofanya katika masiku yake ya nyuma. Yule mwenye kupuuzia mbali anafanya hivo kwa sababu anapendelea malipo. Anayeadhibu kuna khatari kubwa kwa yeye kujutia adhabu yake ingawa itakuwa ni kulipiza kisasi peke yake. Kuhusu yule ambaye anaye ndugu anayempenda, basi amsemehe maisha mazima.

6 – al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Mvumilie ndugu yako mpaka pale anapofanya makosa 70.” Kukasemwa: “Ee Abu ´Aliy! Inakuweje?” Akasema: “Kwa sababu ndugu yako ambaye umejenga naye udugu kwa ajili ya hafanyi makosa 70.”

7 – al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Yule mwenye kumtafuta ndugu asiyekuwa na mapungufu basi atabaki pasi na ndugu.”

8 – Watu wasiohitajia hata kidogo chuki ni wale wenye kuacha kulipiza. Watu walio watukufu zaidi ni wale wenye kurudisha mkabala mbaya kwa mkabala wa upole. Hakuna fadhilah isipokuwa tu kwa yule mwenye kumfanyia uzuri yula aliyemfanyia ubaya. Kumtendea wema yule aliyekufanyia wema si vengine isipokuwa ni kulingana kwa tabia. Wakati mwingine hata wanyama wanakuwa namna hiyo. Endapo kupuuzilia mbali kusingekuwa na sifa nzuri nyingine zaidi ya kuipumzisha nafsi na kuifariji moyo basi ingelikuwa inatosha kwa aliye na busara kutochafua wakati wake kwa kuwa na tabia za wanyama na kulipiza ubaya mabaya. Yule mwenye kulipiza ubaya mabaya basi mwenye kufanya vibaya ijapo si yeye aliyeanza.

9 – Luqmaan alisema kumwambia mwanae:

“Amesema uongo mwenye kusema kuwa shari inazima shari. Akiwa ni mwenye kusema kweli basi hebu awashe moto pambizoni na moto mwingine na aone kama mmoja utazima mwingine. Kheri ndio yenye kuzima shari kama ambavyo maji yanauzima moto.

10 – Mwenye busara hufanya vizuri wakati anapokabiliwa kwa utovu wa adabu na halipizi ubaya mfano wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 166-170
  • Imechapishwa: 13/08/2021