45. Mji mzima wanaswali Dhuhr baada ya kumaliza kuswali ijumaa

Swali 45: Kuna mji ambao ndani yake kuna takriban misikiti thelathini na tano na yote inaswali swalah ya ijumaa. Waswaliji wanapomaliza kuswali swalah ya ijumaa basi wanaswali baada yake Dhuhr. Je, kitendo hichi kinafaa[1]?

Jibu: Ni jambo limetambulika kilazima katika dini na kupitia dalili za Shari´ah ya kwamba Allaah (Subhaanah) hakuweka Shari´ah siku ya ijumaa katika wakati wa adhuhuri isipokuwa faradhi moja peke yake juu ya wanamme, wakazi na waungwana ambao ´ibaadah ni yenye kuwawajibikia. Nayo si nyingine ni swalah ya ijumaa. Waislamu wakifanya hivo basi hawana faradhi nyingine; si Dhuhr wala nyengine. Bali swalah ya ijumaa ndio faradhi ya wakati huo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) na Salaf hawakuwa wakiswali faradhi nyingine baada ya swalah ya ijumaa. Kitendo hichi kilizuliwa baada yao baada ya kupita vizazi vingi. Hapana shaka kwamba ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Tahadharini na mambo yaliyozuliwa, kwani kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila ni upotevu”[2]

Amesema pia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hapana shaka kwamba kuswali Dhuhr baada ya kumaliza kuswali swalah ya ijumaa ni kitu kilichozuliwa na hakiko katika dini yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo kinakuwa ni chenye kurudishwa nyuma. Isitoshe ni kitu kinachoingia katika Bid´ah na upotofu ambao umetahadharishwa na mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanazuoni wamezindua juu ya jambo hilo. Miongoni mwa ambao wamezindua jambo hilo ni Shaykh Jamaad-ud-Diyn al-Qaasimiy katika kitabu chake kwa jina “Iswlaa-ul-Masaajid minal-Bid´ah wal-´Awaaid”, Shaykh na ´Allaamah Muhammad Ahmad ´Abdis-Salaam katika kitabu chake kwa jina “as-Sunan wal-Mubtada´aat”.

Akisema mwenye kusema kwamba wanafanya hivo kwa sababu ya kuchukua tahadhari (الاحتياط) na kukhofia pengine swalah ya ijumaa haikusihi, basi atajibiwa msemaji huyu kwamba msingi ni kusihi kwa swalah ya ijumaa, kusalimika kwake na kutolazimika Dhuhr bali kutokufaa kwake katika wakati wa Dhuhr kwa ambaye inamlazimu faradhi ya ijumaa. Kuchukua tahadhari kumewekwa katika Shari´ah pale ambapo Sunnah haiko wazi na kukawepo na mashaka. Ama katika mfano wa hali hii si pahala pa kutilia mashaka. Bali tunatambua kupitia dalili kwamba kilicho cha lazima ni kuswali swalah ya ijumaa pekee. Kwa hivyo haifai nyengine badala yake wala kuongezea juu yake eti kwa lengo la kuchukua tahadhari kutokana na kusihi kwake na kuunda Shari´ah mpya ambayo haikuidhinishwa na Allaah. Swalah ya Dhuhr ndani ya wakati huu inakwenda kinyume na dalili za ki-Shari´ah zinazotambulika vyema katika dini. Kwa hivyo ikalazimika kuachwa na kutahadhari. Kuifanya hakuna mashiko yoyote yanayotegemewa. Bali hayo yanatokana na wasiwasi wa shaytwaan ambaye anawapa watu muda mpaka afikie kuwazuia kutokamana na uongofu na awawekee mfumo wa dini ambao Allaah hakuuidhinisha. Ni kama ambavo amewapambia baadhi yao kuchukua tahadhari katika jambo la wudhuu´ mpaka akawaadhibu katika twahara na akawafanya wasiweze kumaliza kila wanapokaribia kumaliza ambapo akawatia wasiwasi kwamba haukusihi na kwamba kuna kiungo ambacho hawakukiosha vizuri. Vivyo hivyo ndivo alivowafanya baadhi yao katika swalah wanapopiga Takbiyr kwa ajili ya swalah basi anawatia wasiwasi kwamba hawakuleta Takbiyr ipasavyo. Basi anaendelea kuwatia wasiwasi kwamba hawakuleta Takbiyr ipasavyo. Matokeo yake basi mtu huyu utamuona anapiga Takbiyr hii baada ya nyingine mpaka anakosa Rak´ah ya kwanza, kusoma ndani yake au sehemu yake kubwa. Hivi ni vitimbi na njama za shaytwaan na kupupia kwake kuyabatilisha matendo ya muislamu na kumbabaishia dini yake. Tunamwomba Allaah usalama juu yetu na kwa waislamu wengine na kusalimika kutokamana na vitimbi na wasiwasi wake. Kwani hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.

Kwa kumalizia ni kwamba kuswali swalah ya Dhuhr baada ya swalah ya ijumaa ni Bid´ah na upotofu na kuzua Shari´ah ambayo haikuidhinishwa na Allaah. Kwa hiyo ni lazima kuiacha, kutahadhari nayo, kuwatahadharisha watu nayo na kutosheka na swalah ya ijumaa. Hivo ndivo alivopita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah baada yake na wale waliowafuata kwa wema mpaka hii leo. Nayo ndio haki ambayo haina mashaka yoyote. Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyowafanya kufaulu wa mwanzo wao.”

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/363-365).

[2] Abu Daawuud (3991).

[3] al-Bukhaariy (2499) na Muslim (3242).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 94-97
  • Imechapishwa: 07/12/2021