Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah Ameutumia kila Ummah Mtume, kuanzia kwa Nuuh mpaka kwa Muhammad, ili kuwaamrisha kumuabudu Allaah Peke Yake na akiwakataza shirki. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.”” (Ibraahiym 16:36)

Allaah amewafaradhishia viumbe vyote kukanusha Twaaghuut na badala yake kumuamini Allaah. Ibn Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.”

Twawaaghiyt ni wengi. Wakubwa wao ni watano:

  1. Ibliys, Allaah amlaani.
  2. Yule mwenye kuabudiwa hali ya kuwa yuko radhi kwa hilo.
  3. Yule mwenye kuwaita watu katika kumuabudu.
  4. Yule mwenye kudai kujua kitu katika elimu ya ghaibu.
  5. Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah.

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Hapana kulazimisha katika Dini, kwani imekwishabainika kati ya Uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.” (al-Baqarah 02:256)

MAELEZO

Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa badala ya Allaah na kikaridhika na hilo. Kadhalika kila yule mwenye kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah au akalingania katika hilo. Twaaghuut imetokamana na neno الطغيان na ni kule kuvuka mpaka.

Twaaghuut ni yule anayevuka mpaka ima kwa shirki yake na kufuru yake au akalingania katika hayo yaliyotajwa. Mbaya wao kabisa ni Ibliys, Allaah amlaani. Vilevile inahusiana na kila yule mwenye kuwaita wengine wamuabudu yeye au akaridhia wengine wamuabudu yeye badala ya Allaah, kama alivyofanya Fir´awn na Namruud. Pia anaingia humo kila yule mwenye kudai kujua mambo yaliyofichikana. Mfano wa hao ni makuhani, wapiga ramli na wachawi, katika kipindi cha kishirikiana na baada ya kuja Uislamu. Kadhalika anaingia humo yule mwenye kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kwa kukusudia. Hawa ndio wakubwa wa Twawaaghiyt. Kila yule ambaye atavuka mpaka na akaacha kumtii Allaah ni Twaaghuut.

Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ

“Hapana kulazimisha katika Dini, kwani imekwishabainika kati ya Uongofu na upotofu.”

Uongofu ni Uislamu na yale yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Upotofu ni kufuru na upotevu. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ

“Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah.”

Kukufuru Twaaghuut ina maana ajitenge nayo mbali na aitakidi kuwa ni batili. Anatakiwia kujiweka mbali na shirki. Kumuamini Allaah ina maana asadikishe kuwa Allaah ndiye muabudiwa Wake na kwamba ndiye mungu wa haki, aamini Shari´ah na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ajisalimishe na hayo. Mwenye kufanya hayo ndiye muumini. Halafu (Ta´ala) akasema:

فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“… atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.” (02:256)

Bi maana ameshikilia kishikilio madhubuti, nayo ni hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Anayefanya hivo ameshikilia kishikilio madhubuti kisichovunjika. Mwenye kushikamana kikweli na shahaadah na akawa na msimamo juu yake atafikia Pepo na furaha. Shahaadah ina masharti yake; Allaah peke yake ndiye anatakiwa kuabudiwa, ndiye anatakiwa kutiiwa na Shari´ah Yake inatakiwa kufuatwa.

Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume na Nabii wa mwisho. Yeye ndiye Mtume wa Allaah kwa walimwengu wote; majini na watu wote. Ni wajibu kwa kila yule ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kumtii yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kufuata Shari´ah yake. Hairuhusiwi kwa yeyote kuacha kumfuata. Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imefuta Shari´ah zote zilizotangulia hapo awali. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”” (07:158)

Kabla yake amesema (Subhaanah):

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Basi wale waliomwamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafuata Nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.” (07:157)

وَمَن يَكْفُرْ بِهِ مِنَ الْأَحْزَابِ فَالنَّارُ مَوْعِدُهُ

”Atakayeikanusha kati ya makundi, basi Moto ndio mahali pa miadi yake.” (11:17)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

”Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake hakuna myahudi wala mnaswara yeyote katika Ummah huu atayesikia kuhusu ujio wangu kisha asiamini yale niliyotumwa nayo, isipokuwa atakuwa katika watu wa Motoni.”[1]

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi kama hizo juu ya hilo. Wanachuoni wote wamekubaliana juu ya kwamba haifai kwa yeyote katika Ummah huu kuacha Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba yule mwenye kuonelea hivo ni kafiri.

[1] Muslim (153).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 15/02/2017