Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kumpiga mawe mzinifu aliyeoa/kuolewa au aliwahi kuoa/kuolewa ni haki endapo atakiri mwenyewe au kukawepo ushahidi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe na wale viongozi waongofu pia walipiga mawe.”

MAELEZO

Kuliteremshwa Aayah kuhusu kupiga mawe. Baadaye kikafutwa kisomo chake na kukabaki hukumu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake baada yake walipiga mawe. Kwa hivyo ni lazima kwetu kuifanyia kazi hukumu hii na kutotumbukia katika yale aliyochelea kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) juu yetu[1]. Imaam Ahmad amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe… “

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpiga mawe Maa´iz, mwanamke kutoka katika kabila la Ghaamidiy[2], mwanamke kutoka katika kabila la Juhaaniy[3] na wanawake wawili wa kiyahudi[4]. Imaam Ahamd amesema:

“… na wale viongozi waongofu pia walipiga mawe.”

Bi maana Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy bin Abiy Twaalib – Allaah awe radhi nao wote. Walipiga mawe kwa sababu walitambua kuwa hukumu bado ni yenye kubaki na kwamba imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kupiga mawe hakukufutwa wala hakukubadilishwa. Ni jambo litaendelea kufanya kazi mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Allaah alimtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa haki na akamteremshia Kitabu ambapo ndani yake kulikuwemo Aayah ya kupiga mawe. Tuliisoma, tukaihifadhi na kuifahamu. Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga mawe na sisi tukapiga mawe baada yake. Nakhofia kutakuja siku aseme mwenye kusema: ”Naapa kwa Allaah! Hatupati Aayah kuhusu kupiga mawe ndani ya Qur-aan” na wakapotea kwa sababu ya kuacha jambo la wajibu lililoteremshwa na Allaah. Kupiga mawe ndani ya Qur-aan ni haki na ni kitu kilitumika kwa wanaume na wanawake ambao wako au waliwahi kuingia ndani ya ndoa na wakazini baada ya hilo kuthibiti kwa dalili, ujauzito au kukubali kwa mtu mwenyewe.” (al-Bukhaariy (6830) na Muslim (1691))

[2] Muslim (1695).

[3] Muslim (1696).

[4] al-Bukhaariy (6841) na Muslim (1699).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 157-158
  • Imechapishwa: 05/06/2019