45. Haya ndio malengo ya wenye kuwatukana Maswahabah


Dini na Sunnah hii imetufikia kutoka wapi? Sio kupitia kwa Maswahabah? Wao ndio wakati na kati baina yetu sisi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio walitufikishia dini kwa amana walipoipokea kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila Hadiyth utakuta “kutoka kwa fulani, kutoka kwa fulani kutoka kwa Swahabah”. Wao ndio wakati na kati baina yetu sisi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kufikisha dini. Wametuhifadhia Sunnah na Qur-aan na wakavifikisha kwetu.

Jengine ni wepi walioeneza Uislamu kwa kupigana kwao Jihaad na kulingania katika Uislamu mashariki na magharibi? Je, sio Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Ni wepi waliopambana na walioritadi baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Je, si wao ndio ambao Allaah aliwafanya kuwa imara juu ya dini hii pindi watu wa shari walipotaka kutumia fursa ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakataka kuitikisa dini, kuwaritadisha watu na kuwaondosha kwayo? Allaah akaifanya dini hii kuwa imara kupitia Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumwongoza mbora wao ambaye ni Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh).

Hizi ni baadhi ya fadhila na sifa zao tukufu (Radhiya Allaahu ´anhum).

Sababu zilizowafanya waandishi kuyataja masuala haya katika vitabu vya ´Aqiydah ni ili kuyaraddi mapote potevu yenye kufanya uadui juu ya Uislamu. Malengo yao ni kuutukana Uislamu. Hawakuona njia ilio karibu zaidi isipokuwa hii ya kuwatukana Maswahabah. Kwa kuwa wao ndio waliobeba dini hii na wakaifikisha kwa Ummah. Hivyo wakaona wakiwatukana Maswahabah – ambao ndio wakati na kati baina yetu sisi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kufikisha dini – basi watakuwa wameutukana Uislamu. Kwa sababu Uislamu utakuwa haukuthibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa wale walioinukuu hawatumiwi kama hoja. Haya ndio malengo yao.