Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtapata viongozi ambapo kuna vitu mtavitambua na vyengine hamtovitambua. Yule atakayekemea basi amesalimika na yule mwenye kuchukia ametakasika. Tatizo liko kwa yule atakayeridhia na kufuata.” Wakasema: “Ee  Mtume wa Allaah! Tusiwapige vita?” Akasema: “Hapana, maadamu wanaswali.”[1]

Maadamu wanaswali basi haijuzu kuwafanyia mapinduzi. Mtu asemeje ikiwa wanaswali, wanafunga, wanatoa zakaah, wanahiji na wanawaacha waislamu wafanye yote haya na mengi zaidi? Ni upi msimamo wa wafanya mapinduzi wa leo juu ya haya? Wameshikamana na msimamo upi juu ya Hadiyth:

“Hapana, maadamu wanaswali.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewakataza na kusema:

“Hapana, maadamu wanaswali.”

Pamoja na kuwa wamezembea mambo mengi ya Uislamu amesema:

“Hapana, maadamu wanaswali.”

Hakusema:

“Hapana, maadamu wanaswali, wanatoa zakaah, wanahiji… “

Alichosema tu ni:

“Hapana, maadamu wanaswali.”

Kwa nini? Kwa sababu uasi unapelekea katika madhara makubwa. Unauangamiza Uislamu. Waislamu wanaagamia. Ummah unaangamia. Ufisadi unaenezwa na matunda ya bidii zinaharibiwa. Heshima inavunjwa. Waislamu wanadhalilishwa na kudhoofishwa mpaka wanakuwa tonge lepesi kwa maadui. Inakuwa ni uasi baada ya uasi.

Hii leo wafanya mapinduzi wamezipata nchi zao kupitia njia ya mapinduzi, uchaguzi na mengineyo. Wamefanya nini? Wamehakikisha nini? Ni watu wako mbali kabisa na kuutendea kazi Uislamu. Bali wamewapiku wale viongozi waliopinda kwa kuandaa mikutano ya umoja wa dini, kujenga makanisa, kuwajengea njia manaswara na kuwatweza waislamu na kuwatumia na kuwaangamiza katika dini na dunia yao. Wamefika kupitia uchaguzi, mapinduzi na mengineyo na wako katika wizara. Ni maneno tu matupu. Hakuna tofauti kati yao na wengineo. Hatuwaamini watu hawa. Watu hawa hamu yao kubwa ni kufikia uongozi kwa kutumia njia yoyote ile. Baada ya hapo wanaupa Uislamu mgongo. Ni jambo ambalo mna uzoefu nalo na mmeliona katika miji mingi. Kwanza wanafanya mapinduzi kwa kutumia jina la Uislamu. Halafu wanapelekwa na ukomunisti au mfumo potofu mwingine wowote. Hekima zote zinapatikana katika miongozo inayotolewa na mwekaji Shari´ah huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliye na hekima, mwenye huruma, mpole, shujaa na jasiri. Yeye ndiye ambaye kaufunza Ummah ushujaa, lakini katika jambo hili ameamrisha kusubiri mpaka pale kutapoonekana kufuru ya wazi.

[1] Muslim (1854).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 416-417
  • Imechapishwa: 18/10/2017