45. Baadhi ya sifa tukufu za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Pamoja na misingi hii wanaamrisha mema na wanakataza maovu kwa yale ambayo Shari´ah imeyawajibisha. Wanaonelea kufanya Hajj, kupigana Jihaad, Swalah ya Ijumaa na sikukuu pamoja na viongozi [watawala], ni mamoja wakiwa wema au waovu. Wanahifadhi Swalah ya Jamaa´ah na wanaona kuwapa naswaha Ummah ni katika sehemu ya Dini. Na wanaamini maana ya kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini kwa muumini mwenzake ni kama jengo; upande mmoja unaupa nguvu upande mwingine.”

Halafu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakutanisha baina ya vidole vyake viwili.[1]

Na kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mfano wa waumini, katika kupendana kwao, na kuhurumiana kwao na kuhisiana kwao, ni kama mfano wa mwili mmoja. Wakati kiungo cha mwili kinapatwa na maumivu, mwili mzima unapatwa na homa.”[2]

Na wanaamrisha kuwa na subira wakati wa mitihani, kuwa na shukurani wakati wa raha na kuridhia kwa shida iliyokadiriwa. Wanalingania katika tabia nzuri na matendo mema. Na wanaamini maana ya kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini mwenye imani kamilifu ni yule mwenye tabia nzuri zaidi.”[3]

Na wanahimiza uunge uhusiano na yule uliyekatana naye, na ummpe yule uliyemnyima, umsamehe yule aliyekudhulumu na kukufanyia ubaya.

Na wanaamrisha kuwatendea wema wazazi wawili na kuwaunga ndugu, kuwatendea wema majirani, kuwafanyia wema mayatima na masikini, na wasafiri na watumwa.

Na wanakataza majivuno na kiburi, ukandamizaji na unyanyasaji kwa viumbe, sawa iwe kwa haki au pasi na haki.

Na wanaamrisha kuwa na maadili mema na wanakataza mabaya.

Na katika kila wanayoyasema na kuyafanya – katika haya na mengineyo – wanafuata Kitabu na Sunnah. Njia yao ni Dini ya Uislamu ambayo Allaah Amemtuma kwayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini alipoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Ummah wake utagawanyika mapote sabini na tatu na yote yataingia Motoni isipokuwa moja, nayo ni al-Jamaa´ah.”[4]

Na katika Hadiyth nyingine kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni wale ambao watakuwemo kwa mfano wa yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[5]

wamekuwa wale wenye kushikamana bara bara na Uislamu wa wazi na msafi kabisa, ni “Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah”. Na miongoni mwao kuna wakweli, mashahidi na watu wema na vilevile kuna maimamu wa uongofu na wenye kuzuia giza la kwenye mwangaza. Wana nafasi kuu na fadhila zingine tulizozitaja. Miongoni mwao kuna ´Abdaal na maimamu wa Dini ambao wamekusanyika Waislamu kwa uongofu wao.

Nao ni at-Twaaifah al-Mansuurah, ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu wao:

“Na hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa ni chenye kunusuriwa juu ya haki. Hatowadhuru wale wenye kwenda kinyume nao na kuwapinga mpaka itapofika Qiyaamah.”[6]

Hitimisho

Tunamuomba Allaah Atujaalie katika wao, na wala Asizipotoe nyoyo zetu baada ya Kutuongoza na Aturehemu. Hakika Yeye Ndiye Al-Wahhaab. Na Allaah Anajua zaidi. Swalah na salaam zimwendee Muhammad, ahli zake na Maswahabah wake wote.

MAELEZO

Maneno haya ambayo ameyataja mwandishi kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni maneno mazito. Ni maneno ambayo yanapaswa kuandikwa kwa maji ya dhahabu. Inampasa kila muumini ayaamini, ayatendee kazi na ayafuate. Haya ndio maneno ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Qur-aan Tukufu na Sunnah Twaharifu imefahamisha hayo. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kusifika na kheri zote.

Pamoja na misingi hii wanaamrisha mema… – Wanaamrisha mema na kukataza maovu kwa mujibu wa Shari´ah. Wamefungamana na Shari´ah. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki walinzi wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza maovu.” (09:71)

Wanaonelea kufanya Hajj… – Wanaonelea kusimamisha swalah pamoja na Ijumaa kwa Jamaa´ah, kupigana Jihaad pamoja na viongozi, ni mamoja wawe wema au waovu. Hili ni kutokana na hekima inayopatikana katika kufanya hivi. Mzigo wa madhambi yake yako juu yake. Wanaswali pamoja naye Ijumaa na swalah za Jamaa´ah na kupigana Jihaad pamoja naye hata kama atakuwa ni mwenye kufanya baadhi ya maasi. Hivi ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa Banuu Umayyah, Abul-´Abbaas na wengineo.

Wanaamrisha kuwatendea wema wazazi wawili, kuunga kizazi, kufanya ujirani mwema, walingania katika kuwa na tabia njema, kufanya matendo mazuri, wanahimiza kumuunga yule uliyemkata, umsamehe yule aliyekudhulumu na ummpe aliyekunyima. Wanaamini yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mfano wa waumini, katika kupendana kwao, na kuhurumiana kwao na kuhisiana kwao, ni kama mfano wa mwili mmoja. Wakati kiungo cha mwili kinapatwa na maumivu, mwili mzima unapatwa na homa.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini kwa muumini mwenzake ni kama jengo; upande mmoja unaupa nguvu upande mwingine.”

“Muumini mwenye imani kamilifu ni yule mwenye tabia nzuri zaidi.”

Yote haya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kuyaamini. Katika yote wanayoyasema na kuyafanya ni wenye kufungamana na Qur-aan na Sunnah. Wao hawana malengo mengine. Bali maneno yao na matendo yao ni wenye kufungamana na Qur-aan na Sunnah. Kwa ajili hii ndio maana wakaitwa “Ahl-us-Sunnah”, “Ahl-ul-Jamaa´ah na “Ahl-ul-Kitaab was-Sunnah”. Si kwa jengine bali ni kwa sababu wamekusanyika, kufungamana na kushirikiana katika hayo. Wao ndio Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Ahl-ul-Kitaab was-Sunnah. Hivi ndivyo walivyobainisha wanachuoni.

Na miongoni mwao kuna wakweli, mashahidi… – Katika wao kuna maimamu wa uongofu na elimu. Hawa ni wale waliosimama bara bara katika dini na wakajifungamanisha na Shari´ah. Wote hao wanaingia katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Miongoni mwao kuna ´Abdaal… – Katika wao kuna ´Abdaal. Hawa ni wale wenye kubadilishana baadhi kwa wengine. ´Abdaal ni wanachuoni ambao hawa wanawarithi wengine. Kwa maana ya kwamba anapokufa mwanachuoni huyu anakuja baada yake mwengine mpaka kifike Qiyaamah. Hii ndio hali ya Ummah huu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Na hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa ni chenye kunusuriwa juu ya haki. Hatowadhuru wale wenye kwenda kinyume nao na kuwapinga mpaka itapofika Qiyaamah.”

Katika kipindi hicho waumini wanaume na wanawake wote watakuwa wameshafariki. Kutakuwa hakukubaki isipokuwa viumbe waovu tu ndio wataosimamiwa na Qiyaamah.

Tunamuomba Allaah atujaalie sisi na nyinyi kuwa katika wao, atukinge sisi na nyinyi kutokana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu na ainusuru dini Yake na alinyanyue Neno Lake.

Hakuna nguvu za kufanya utiifu na kuacha maasi isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake na Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (6026) na Muslim (2585)

[2] al-Bukhaariy (6011) na Muslim (2586)

[3] Ahmad (2/472), Abuu Daawuud (4682) na at-Tirmidhiy (1162). Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) kasema kuwa ni Swahiyh katika “Swahiyh at-Tirmidhiy” (3/886)

[4] Abuu Daawuud (4596), Ahmad (2/333), at-Tirmidhiy (2778). Ibn Maajah (3991) na wengine. Tazama “as-Silsilah as-Swahiyhah” (204) ya Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah).

[5] at-Tirmidhiy (2779) na al-Haakim (1/129).

[6] al-Bukhaariy (3641) na Muslim (1037).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com