45. Anayotakiwa kufanya mwenye hedhi na asiyotakiwa wakati wa kuhiji

11 – Anayotakiwa kufanya mwanamke mwenye hedhi katika ´ibaadah za hajj na asiyotakiwa kufanya mpaka kwanza atwahirike.

a) Mwanamke mwenye hedhi atafanya ´ibaadah zote za hajj katika Ihraam, kusimama zile sehemu za ´ibaadah, kusimama ´Arafah, kulala Muzdalifah na kurusha vijiwe. Asitufu Ka´bah mpaka kwanza atwahirike. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Fanya yale anayofanya mwenye kuhiji isipokuwa tu usifanye Twawaaf kwenye Nyumba mpaka utwahirike.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Fanya anayofanya mwenye kuhiji isipokuwa usitufu kwenye Ka´bah mpaka kwanza uoge.”

ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Hadiyth iko wazi juu ya makatazo kwa mwenye hedhi kutufu mpaka ikatike kwanza damu yake na aoge. Makatazo yanapelekea katika kuharibika. Kwa hiyo Twawaaf ya mwenye kuhiji itakuwa ni batili. Hayo ndio maoni ya wanachuoni wengi.”[1]

Asifanye Sa´y kati ya Swafaa na Marwah. Kwa sababu Sa´y haisihi isipokuwa baada ya Twawaaf ya ´ibaadah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) hakufanya Sa´y isipokuwa baada ya Twawaaf. Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´”

“Lau mtu alifanya Sa´y kabla ya Twawaaf tunaona kuwa haisihi. Hayo pia ndio maoni ya wanachuoni wengi. Tumeshatangulia kutoka kwa al-Mawaardiy kwamba amenakili maafikiano juu ya hilo. Pia ndio madhehebu ya Maalik, Abu Haniyfah na Ahmad. Ibn-ul-Mundhir ameeleza kutoka kwa ´Atwaa´ na baadhi ya Ahl-ul-Hadiyth ya kwamba inasihi. Wenzetu pia wamesimulia kutoka kwa ´Atwaa´ na Daawuud. Dalili yetu ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) alifanya Sa´y baada ya Twawaaf na akasema (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam): “Chukueni kutoka kwangu ´ibaadah zenu za hajj.” Ama kuhusu Hadiyth ya Swahabah Ibn Shurayk (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema: “Alitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) kwenda kuhiji na akawa anajiwa na watu; kuna mmoja akamuuliza: “Ee Mtume wa Allaah! Nilifanya Sa´y kabla ya Twawaaf, nilichelewesha kitu au nilitanguliza kitu. Akasema: “Hakuna neno isipokuwa kwa mtu ambaye amekopesha kwa heshima ya mtu muislamu ilihali amemdhulumu; huyo ndiye ameangamia na akapata dhambi.” Hadiyth hii inafasiriwa kama alivyoifasiri al-Khattwaabiy na wengineo ya kwamba maneno yake: “Nilifanya Sa´y kabla ya Twawaaf” kwamba alifanya Sa´y baada ya Twawaaf-ul-Quduum na kabla ya Twawaaf-ul-Ifaadhwah.”[2]

Shaykh wetu Muhammad al-Aamiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika tafsiri yake ya Qur-aan “Adhwaa´-ul-Bayaan”:

“Tambua kwamba wanachuoni wengi wanaona kuwa kufanya Sa´y hakusihi isipokuwa baada ya Twawaaf. Hivyo wanachuoni wengi hao wanaona kuwa iwapo mtu atafanya Sa´y kabla ya Twawaaf basi Sa´y yake haitosihi. Miongoni mwao ni wale maimamu wane na al-Mawaardiy na wengineo wamenukuu maafikiano juu ya hilo. Kisha akamnukuu an-Nawawiy, ambaye tumekwishampitia punde tu, na akajibu Hadiyth ya Ibn Shurayk kisha akasema: “Maneno yake “Nilifanya Sa´y kabla ya Twawaaf” ya kwamba ni Twawaaf-ul-Ifaadhwah ambayo ndio nguzo. Hayo hayapingani kwamba alifanya Sa´y baada ya Twawaaf-ul-Quduum ambayo sio nguzo.”[3]

Mtunzi wa al-Mughniy amesema:

“Sa´y ni yenye kufuatia Twawaaf; haisihi isipokuwa aitangulizie Twawaaf. Akifanya Sa´y kabla yake haitosihi. Hayo ndio maoni ya Maalik, ash-Shaafi´iy na watu wa rai. ´Atwaa´ amesema: “Inasihi.” Ahmad pia anaona kuwa inasihi akiwa ni mwenye kusahau na akiwa ni mwenye kukusudia haisihi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) alipoulizwa juu ya kutanguliza na kuchelewesha katika hali ya ujinga na kusahau akajibu: “Hakuna neno.” Wajihi wa kwanza ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) alifanya Sa´y baada ya Twawaaf na yeye ndiye amesema: “Chukueni kutoka kwangu ´ibaadah zenu za hajj.”[4]

Imetambulika kutokana na yaliyotangulia kwamba Hadiyth ambayo inatumiwa na wale wenye kusema kwamba Twawaaf kabla ya Sa´y inasihi hakuna mategemeo yoyote. Kwa sababu inafasiriwa kwa moja katika ya mambo mawili:

1 – Inamuhusu yule ambaye alifanya Sa´y kabla ya Twawaaf-ul-Ifaadhwah na alikuwa tayari amekwishafanya Twawaaf-ul-Quduum. Kwa hiyo Sa´y yake inakuwa imetokea baada ya Twawaaf.

2 – Ni kwa yule ambaye ni mjinga na mwenye kusahau na si ambaye amefanya kwa makusudi.

Nimerefusha mambo haya kwa sababu hii leo wamejitokeza watu ambao wanatoa fatwa juu ya kufaa kufanya Sa´y kabisa kabla ya Twawaaf.

[1] (05/49).

[2] (08/82).

[3] (05/252).

[4] (05/240) chapa ya Hajar.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 90-93
  • Imechapishwa: 13/11/2019