38- Haijuzu kumvua shahidi nguo aliyouliwa akiwa ameivaa. Bali azikwe akiwa ameivaa. Hayo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu wauliwaji wa Uhud:

“Wagubikeni katika nguo zao.”

Ameipokea Ahmad (05/431) kwa tamko hili. Katika upokezi wake mwingine imekuja:

“Wagubikeni kwa damu zao.”

Vilevile ameipokea an-Nasaa´iy (01/282) na ash-Shawkaaniy (04/34) ameiegemeza kwa Abu Daawuud ambapo akakosea katika hilo.

Kuhusiana na maudhui haya ipo Hadiyth kutoka kwa Jaabir, Abu Barzah na Anas. Tazama masuala ya 32 Hadiyth ya kwanza, ya pili na ya tatu ukurasa wa 52-53.

39- Imependekezwa kumvika sanda kwa nguo moja au nyingi juu ya nguo zake. Hivo ndivo alivofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Musw´ab bin ´Umayr na Hamzah bin ´Abdil-Muttwalib. Visa vyao vimekwishatangulia katika masuala ya 34, 36 na 37. Kuhusu maudhui haya kuna visa viwili vyengine:

Cha kwanza: Shaddaad bin al-Haad ameeleza:

“Kuna bwana mmoja katika mabedui alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamwamini na akamfuata. Kisha akasema: “Nahajiri pamoja nawe.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawausia baadhi ya Maswahabah zake juu yake. Wakati ilipokuwa vita vya [Khaybar] Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipata ngawira [ndani yake kulikuwa kuna] kitu. Akagawa na akamgawia na bwana yule ambapo akawapa Maswahabah zake kile alichomgawia. Alikuwa akichunga wanyama wao. Alipowajia wakampa kile walichopewa. Akasema: “Ni kipi hichi?” Wakasema: “Ni fungu lako amekugawia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akalichukua na akaenda nalo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasem: “Ni kipi hichi?” Akamjibu: “Nimekugawia.” Akasema: “Mimi sikukufuata kwa sababu ya haya. Lakini mimi nimekufuata ili nipigwe mshale hapa – akaashiria kooni mwake – na nife ambapo niingie Peponi.” Akasema: “Ukiwa mkweli kwa Allaah basi Allaah atakufanya uwe mkweli.” Wakakaa kitambo kidogo. Kisha wakaandoka kumpiga vita adui. Baadaye wakamleta kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiwa wamembeba na mshale umempiga pale alipoashiria. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndiye yule?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Amekuwa mkweli kwa Allaah na Allaah akamfanya kuwa mkweli.” Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamvika sanda ndani ya joho la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamtanguliza mbele na kumswalia. Ikawa miongoni mwa yaliyodhihiri kutoka katika swalah yake:

اللهم هذا عبدك، خرج مهارجرا في سبيلك، فقتل شهيدا، أنا شهيد على ذلك

“Ee Allaah! Hakika huyu ni mja Wako ambaye ametoka hali ya kuwa ni mwenye kuhajiri katika njia Yako na akauliwa shahidi na mimi ni shahidi juu ya hayo.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (01/277) na at-Twahaawiy katika “Sharh-ul-Ma´aaniy” (01/291), al-Haakim (03/595-596) na al-Bayhaqiy katika “as-Sunan” (04/15-16) na “ad-Dalaa-il” (04/22).

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Wapokezi wote wako juu ya sharti za Muslim isipokuwa tu Shaddaad bin al-Haad hakumpokelea chochote, jambo ambalo halidhuru. Ni Swahabah anayetambulika. Kuhusu maneno ya ash-Shawkaaniy katika “an-Nayl al-Awtwaar” (03/37) akimuiga an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/565) kwamba ni Taabiy´ hilo ni kosa la wazi na wala watu wasighurike nalo.

Cha pili:  az-Zubayr bin al-´Awwaam (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Ilipokuwa siku ya Uhud alikuja mwanamke mmoja akiwa ni mwenye kufanya haraka mpaka alipokaribia kufika pale pahali palipowekwa wafu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yule mama asije kuwaona ambapo akasema: “Mwanamke huyo! Mwanamke huyo!” Nikahisi kuwa ni mama yake na Swafiyyah ambapo nikatoka kumwelekea na nikamuwahi kabla ya kufika kwa wale wafu. Akanipiga kwa mikono yake kifuani mwake. Alikuwa ni mwanamke mwenye nguvu. Akasema: “Niondokee hapa, huna ardhi wewe!” Nikasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekulenga wewe. Basi ndipo akasimama na akatoa nje mashuka mawili aliokuwa nayo na kusema: “Mashuka mawili haya niliyokuja nayo ni kwa ajili ya ndugu yangu Hamzah. Nimefikiwa na khabari juu ya kuuawa kwake. Kwa hivyo mvikeni sanda kwa mashuka mawili haya.” Tukaja na mashuka mawili yale ili tumkafini kwayo Hamzah. Tahamaki pambizoni mwake alikuwa bwana mmoja kutoka katika Answaar ambaye ameuawa na amefanyiwa yale aliyofanyiwa Hamzah ambapo tukahisi vibaya na aibu kumvika sanda Hamzah kwenye mashuka mawili ilihali bwana huyu wa Answaar hana sanda yoyote. Tukasema: “Hamzah apate shuka moja na bwana huyu wa Answaar apate shuka moja. Tukazipima ambapo moja ikawa ni kubwa zaidi kuliko nyingine. Tukawapigia kura ambapo kila moja katika mashuka yale mawili likamwangukia lile shuka linalomstahikia.”

Ameipokea Ahmad (1418) na mtiririko ni wake kwa cheni ya wapokezi nzuri, al-Bayhaqiy (03/401) na cheni ya wapokezi ni Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 80-82
  • Imechapishwa: 24/02/2020