1- Kufuru kilugha maana yake ni kufunika na kusitiri. Maana ya kufuru Kishari´ah ni kinyume cha imani. Kufuru ni kutomwamini Allaah na Mtume Wake. Ni mamoja kuambatane na kukadhibisha au kusiambatane na kitendo hicho. Bali kule kuwa na mashaka peke yake, kupuuza, hasadi, kiburi au kufuata baadhi ya matamanio yanayomzuia mtu kutofuata ujumbe. Ingawa mkadhibishaji ana ukafiri mkubwa zaidi. Vivyo hivyo mkanushaji na mkadhibishaji kwa ajili ya hasadi pamoja na kuyakinisha ukweli wa Mitume[1].

Aina za kufuru

2- Kuna aina mbili za kufuru

Kufuru kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu. Imegawanyika mafungu matano:

Fungu la kwanza: Kufuru ya kukadhibisha. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ

“Nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Allaah uongo au aliyekadhibisha haki ilipomjia? Je, si katika Jahannam ndio yatakuwa makazi ya makafiri?”[2]

Fungu la pili: Kufuru ya kukataa na kufanya kiburi pamoja na kusadikisha. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

”Pindi Tulipowaambia Malaika: ”Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri.”[3]

Fungu la tatu: Kufuru na mashaka. Hiyo ni kufuru ya dhana. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِ أَبَدًا وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا  لَّـٰكِنَّا هُوَ اللَّـهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا

“Akaingia bustanini mwake hali naye amejidhulumu nafsi yake akasema: “Sidhani kama haya yatatoweka kamwe na wala sidhani kama Qiyaamah kitasimama na hata kama nitarudishwa kwa Mola wangu, bila shaka nitakuta marejeo bora kuliko haya. Rafiki yake akamwambia na huku anajadiliana naye: “Je, umemkufuru Yule aliyekuumba kutokana na mchanga, kisha kutokana na manii, kisha akakusawazisha kuwa mtu? Lakini Yeye Allaah ndiye Mola wangu na wala sitomshirikisha Mola wangu na yeyote.”[4]

Fungu la nne: Kufuru ya kupuuza. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

“Na wale waliokufuru kwa yale wanayoonywa kwayo ni wenye kukengeuka.”[5]

Fungu la tano: Kufuru ya unafiki. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ

“Hayo ni kwa kuwa wao waliamini, kisha wakakufuru, basi ikapigwa chapa juu ya nyoyo zao kwa hiyo hawafahamu.”[6]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/335).

[2] 29:68

[3] 02:34

[4] 18:35-38

[5] 46:03

[6] 63:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 16/03/2020