44. Mwenye busara na subira juu ya matatizo


1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Kisha akaiamrisha iandike yatayokuweko mpaka siku ya Qiyaamah.”

2 – Ni wajibu kwa aliye na busara kuyakinisha kwamba kila kitu kimekwishapangwa. Yapo ambayo yatayokea na hakuna njia ya kuyakwepa. Ambayo hayatokuwepo basi hakuna namna kwa viumbe kuyafanya yawepo.

3 – Mtu akisibiwa na hali ya shida basi ni lazima ajivike shuka mbili; subira na kuridhia. Katika hali hii anakuwa na ujira kamilifu. Ni majanga mangapi yalikuwa mazito kabisa kujinasua nayo kisha yakawa mepesi kwa muda wa kupepesa kwa macho?

4 – Abul-Hajjaaj al-Azdiy amesema:

“Tulimuuliza Salmaan nini maana ya kuamini Qadar. Akasema: “Ni pale ambapo mja atajua kuwa yale yaliyompata hayakuwa ya kumkosa na yale yaliyomkosa hayakuwa ya kumpata.”

5 – ´Abdul-Waahid bin Zayd amesema:

“Nilisema kumwambia al-Hasan al-Baswriy: “Ni wapi unatoa tabia hii?” Akasema: “Kutokana na uchache wa kumridhia Allaah.” Nikasema: “Ni wapi umetoa uchache wa kumridhia Allaah?” Akasema: “Kutokana na uchache wa kumtambua Allaah.”

6 – Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

“Nilimsikia bwana mmoja aliyesilimu akisema: “Allaah alimteremshia Wahy Daawuud: “Ee Daawuud! Subiria matatizo hivyo utapata msaada kutoka Kwangu.”

7 – ´Abdul-Waahid bin Zayd amesema:

“Sipendi kuwepo kitendo chochote kitachoitangulia subira isipokuwa kuridhia. Sitambui kama kuna kitu ambacho ni kitukufu na kilicho juu zaidi kama kuridhia. Kuridhia ndio kichwa cha mapenzi kumpenda Allaah.”

8 – Subira imekusanya kila kitu. Subira ndio nguzo ya maamuzi na msaada wa akili. Subira ndio jereha la kheri na ufumbuzi kwa yule asiyekuwa na ufumbuzi.”

9 – Maymuum bin Mahraan amesema:

“Hakuna mja yeyote, si Nabii wala mwengine, aliyefikia kheri bila kuwa na subira.”

 10 – Subira inaweza kugawanywa mafungu matatu; kusubiri juu ya maasi, kusubiri juu ya matendo mema na kusubiri wakati wa matatizo. Bora ni ile subira juu ya maasi. Mwenye busara anatakiwa kuzipangilia hali zake tatu kwa kuwa na subira ili awe radhi na Allaah (Jalla wa ´Alaa) wakati wa hali nzito na nyepesi. Namuomba Allaah kuweza kufikia ngazi hiyo.

11 – Thaabit al-Bunaaniy amesema:

“Silah bin Ushaym alikuwa vitani pamoja na mtoto wake. Akamwambia: “Mwanangu kipenzi! Sogea mbele upigane mpaka uuawe ili niweze kutarajia malipo kutoka kwa Allaah kwa sababu ya subira nitayofanya. Akasogea mbele akapigana mpaka akauawa. Baada ya hapo baba yake na yeye akasogea mbele akapigana mpaka akauawa. Wanawake walipokusanyika mke wake Mu´aadhah al-´Adhriyyah akawaambia: “Ikiwa mmekuja kwa ajili ya kunipa hongera karibuni. Ikiwa mmekuja kwa sababu nyingine rejeeni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 155-163
  • Imechapishwa: 12/08/2021