44. Mtenda dhambi huko Aakhirah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule mwenye kukutana na Allaah baada ya kufanya dhambi inayopelekea kuadhibiwa Motoni ilihali ametubia na sio mwenye kuendelea juu yake, Allaah anamsamehe. Anakubali tawbah kutoka kwa waja Wake na anayasamehe madhambi. Yule mwenye kukutana Naye baada ya kutekelezewa adhabu ya dhambi yake hapa duniani, basi hiyo ndio kafara yake. Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atakayekutana Naye hali ya kuwa ni mwenye kuendelea juu ya madhambi yake pasi na kutubia madhambi yanayopelekea kuadhibiwa, jambo lake liko kwa Allaah; akitaka kumuadhibu Atamuadhibu na akitaka kumsamehe Atamsamehe[1]. Hata hivyo yule atakayekutana Naye akiwa ni kafiri atamuadhibu na wala hatomsamehe.”

MAELEZO

Mwenye kukutana na Allaah akiwa na dhambi kubwa ambayo tayari amekwishatubia kwayo, basi tunatarajia kwamba Allaah atamsamehe. Akikutana Naye kabla ya kutubia, basi jambo lake liko kwa Allaah; akitaka atamsamehe na akitaka atamuadhibu. Hata hivyo tunaamini kuwa mwisho wa kila mpwekeshaji ni Peponi mwanzoni au mwishoni ijapokuwa ataadhibiwa Motoni – na Allaah (Ta´ala) ndiye anajua zaidi.

Muumbaji ndiye atakayeamua ni kipi atachowafanya wale watenda madhambi makubwa; akitaka kuwasamehe na kuwaingiza Peponi bila ya hesabu, atafanya hivo, na akitaka kumuadhibu mtu kwa sababu ya dhambi yake kubwa, atafanya hivo kwani hakuna yeyote awezaye kuzuia hukumu Yake. Hakuna yeyote awezaye kurudisha alichoamua na anafanya akitakacho. Imaam Ahmad amesema:

“Hata hivyo yule atakayekutana Naye akiwa ni kafiri atamuadhibu na wala hatomsamehe.”

Dalili zimefahamisha kuwa kila kafiri aliyekufa hali ya kuwa ni kafiri basi atadumishwa Motoni milele; kamwe hatotoka ndani yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ يَصْلَوْنَهَا يَوْمَ الدِّينِ وَمَا هُمْ عَنْهَا بِغَائِبِينَ

“Hakika waumini watendao mema kwa wingi bila shaka watakuwa katika neema na hakika watendao dhambi bila shaka watakuwa katika Moto uwakao vikali mno; watauingia waungue siku ya malipo – nao hawatokosa kuweko humo.”[2]

[1] al-Bukhaariy (3892) na Muslim (1709).

[2] 82:13-16

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 153-154
  • Imechapishwa: 02/05/2019