44. Mpangilio wa fadhila za Maswahabah


Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba Muhaajiruun ni bora kuliko Answaar kwa kuwa Allaah ametangulia kuwataja wao. Jengine ni kwa sababu wameziacha mali zao, watoto wao na miji yao na wakahajiri katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ

“Wanatafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli.” (59:08)

Kisha wabora katika Muhaajiruun ni wale makhaliyfah wanne; Abu Bakr asw-Swiddiyq, kisha ´Umar al-Faaruuq, halafu ´Uthmaan Dhun-Nurayn, kisha ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhum).

Halafu wanafuata wale kumi waliobashiriwa Pepo.

Kisha wanafuata walioshuhudia vita vya Badr.

Kisha wanafuata waliompa kiapo cha usikivu na utiifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chini ya mti:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini walipokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti.” (48:19)

Allaah (´Azza wa Jall) ameeleza kuwa amewaridhia. Halafu anajitokeza mtenda dhambi mkubwa mmoja kisha anawasema vibaya Maswahabah. Allaah awakebehi waovu na wapotevu.

Halafu wale waliosilimu kabla ya Ushindi wa Makkah ni bora kuliko wale waliosilimu baada ya Ushindi. Amesema (Ta´ala):

لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚأُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ

“Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi [wa Makkah] na akapigana. Hao watapata daraja kuu kabisa kuliko wale waliotoa baada [ya ushindi] na wakapigana – na wote Allaah amewaahidi Pepo.” (59:10)

Wote wawili, waliosilimu kabla ya Ushindi na waliosilimu baada ya Ushindi:

وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ

“Wote Allaah amewaahidi Pepo.”

Hakuna yeyote anayewafikia Maswahabah katika fadhila vovyote atavyotenda. Inatosheleza kwao kuwapenda, kufuata mwongozo wao, kuwasifu, asimtukane yeyote katika wao, asipekue kasoro zao na asiingilie yaliyopitika kati yao kwa sababu ya fitina iliyowaingilia. Waliingiliwa na janga pasi na wao kupenda. Asiwepo yeyote atayeingilia suala la Maswahabah isipokuwa kwa kuwasifu, kuwaombea msamaha na huruma, kuiga mwongozo wao na kuwapenda kwa kuwa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanawapenda. Sisi tunampenda yule anayependwa na Allaah na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).