44. Mlango kuhusu kusema “Akitaka Allaah na wewe”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Qutaylah amesema:

“Kuna myahudi alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema: “Hakika nyinyi mnafanya shirki. Mnasema: “Akitaka Allaah na ukataka wewe” na mnasema: “Naapa kwa Ka´bah.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amewaamrisha wanapotaka kuapa basi waseme: “Naapa kwa Mola wa Ka´bah” na waseme: “Akitaka Allaah kisha wewe”.”[1]

Ameipokea an-Nasaa´iy na ameisahihisha.

2- an-Nasaa´iy amepokea vilevile Hadiyth kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Kuna mtu alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Akitaka Allaah na ukataka wewe”. Ndipo akasema: “Je, umenifanya mimi kuwa mshirika wa Allaah?” Watakiwa kusema: “Akitaka Allaah pekee.”[2]

3- Ibn Maajah amepokea kutoka kwa at-Twufayl ambaye ni kaka wa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa upande wa mama yake, amesema:

“Nimeona ndotoni ambapo niliwapitia kundi la mayahudi na kuwaambia: “Nyinyi ni watu wazuri lau msingelisema kwamba ´Uzayr ni mwana wa Allaah.” Wakasema: “Nanyi ni watu wazuri pia lau msingelisema: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Baada ya hapo nikawapitia kundi katika manaswara na nikawaambia: “Nyinyi ni watu wazuri lau msingelisema kwamba al-Masiyh ni mwana wa Allaah”. Nao wakasema: “Nanyi ni watu wazuri pia  lau msingelisema: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Kulipopambazuka nikamweleza niliyemweleza kisha nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikamweleza. Akasema: “Je, umemweleza haya yeyote?” Nikasema: “Ndio.” Akamhimidi Allaah na kumsifu kisha akasema “Ama baada ya hayo; hakika Twufayl ameona ndoto na kishamweleza aliyemweleza katika nyinyi. Hakika nyinyi mlikuwa mkisema maneno kadhaa na kadhaa ambayo yalikuwa yakinitatiza nikawa nashindwa kuwakataza nayo. Hivyo msisemi: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Lakini semeni: “Akitaka Allaah pekee”.”[3]

MAELEZO

Anachotaka mwandishi ni kubainisha hukumu ya kusema “Akitaka Allaah na akataka fulani” na mfano wa maneno kama hayo na kwamba kilicho cha wajibu ni kusema “Akitaka Allaah kisha fulani”. Haya ndio yanayopelekewa na Tawhiyd na Ikhlaasw. Ndani yake kuna ukamilifu wa Tawhiyd na kujitenga mbali na aina zote za shirki. Hukumu ya kusema namna hiyo ni kwamba haifai. Makusudio ya mlango huu kwa msemo mwingine ni kwamba hukumu ya kutamka namna hiyo.

Kamilifu zaidi ni kusema “Akitaka Allaah pekee”. Hata hivyo inafaa kusema “Akitaka Allaah kisha akataka fulani”. Ama kusema “Akitaka Allaah na akataka fulani” haijuzu. Ni aina ya shirki ndogo na linaipunguza Tawhiyd. Vilevile inahusiana na matamshi mfano wa hayo.

1- Qutaylah amesema:

“Kuna myahudi alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema: “Hakika nyinyi mnafanya shirki. Mnasema: “Akitaka Allaah na ukataka wewe” na mnasema: “Naapa kwa Ka´bah.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amewaamrisha wanapotaka kuapa basi waseme: “Naapa kwa Mola wa Ka´bah” na waseme: “Akitaka Allaah kisha wewe”.”

Ameipokea an-Nasaa´iy na ameisahihisha.

Hapa kuna dalili inayoonyesha kwamba watu wapotevu wanaweza kuyafahamu baadhi ya mambo japokuwa wao wenyewe ni wenye kutumbukia katika dhambi na kufuru mbaya zaidi. Kwa ajili hiyo mayahudi waliwakaripia waislamu kwa sababu ya matamshi hayo yote haya kwa sababu tu ya chuki na vifundo walivyo navyo dhidi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo walipatia katika haya. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha waseme “Akitaka Allaah kisha akataka fulani” na waape kwa Mola wa Ka´bah.

2- an-Nasaa´iy amepokea vilevile Hadiyth kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Kuna mtu alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Akitaka Allaah na ukataka wewe”. Ndipo akasema: “Je, umenifanya mimi kuwa mshirika wa Allaah?” Watakiwa kusema: “Akitaka Allaah pekee.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Je, umenifanya kuwa ni mwenye kulingana na Allaah?”

 3- Ibn Maajah amepokea kutoka kwa at-Twufayl ambaye ni kaka wa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa upande wa mama yake, amesema:

“Nimeona ndotoni ambapo niliwapitia kundi la mayahudi na kuwaambia: “Nyinyi ni watu wazuri lau msingelisema kwamba ´Uzayr ni mwana wa Allaah.” Wakasema: “Nanyi ni watu wazuri pia lau msingelisema: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Baada ya hapo nikawapitia kundi katika manaswara na nikawaambia: “Nyinyi ni watu wazuri lau msingelisema kwamba al-Masiyh ni mwana wa Allaah”. Nao wakasema: “Nanyi ni watu wazuri pia  lau msingelisema: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Kulipopambazuka nikamweleza niliyemweleza kisha nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikamweleza. Akasema: “Je, umemweleza haya yeyote?” Nikasema: “Ndio.” Akamhimidi Allaah na kumsifu kisha akasema “Ama baada ya hayo; hakika Twufayl ameona ndoto na kishamweleza aliyemweleza katika nyinyi. Hakika nyinyi mlikuwa mkisema maneno kadhaa na kadhaa ambayo yalikuwa yakinitatiza nikawa nashindwa kuwakataza nayo. Hivyo msisemi: “Akitaka Allaah na akataka Muhammad”. Lakini semeni: “Akitaka Allaah pekee”.”

Bi maana mlikuwa ni wenye kustahiki kusifiwa msingelisema hivo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika nyinyi mlikuwa mkisema maneno kadhaa na kadhaa ambayo yalikuwa yakinitatiza nikawa nashindwa kuwakataza nayo.”

Kwa sababu kulikuwa hakujakuja kitu kutoka kwa Allaah. Wakati ndoto ilipokuja ndipo kukaja sababu ya kuwakataza. Vivyo hivyo kumekuja Wahy wa makatazo juu ya kusema hivo na badala yake maamrisho ya kusema:

“Akitaka Allaah pekee.”

Katika Hadiyth iliopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kuhusu kipofu, mwenye ukoma na mwenye upara imekuja:

“Hakuna yeyote awezaye kunifikisha hii leo isipokuwa Allaah kisha wewe.”[4]

Hili ndilo la wajibu.

Ni kama tulivosema kwamba kusema “Akitaka Allaah na wewe” ni shirki ndogo. Inaweza vilevile kuwa shirki kubwa ikiwa anamaanisha kwamba mtu huyo yeye ndiye anayeyaendesha mambo kwa kutaka kwake mwenyewe.

[1] an-Nasaa’iy (3773) na at-Twabaraaniy (7). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (136).

[2] al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (783) na at-Twabaraaniy (13005).

[3] Ibn Maajah (2118), Ahmad (20713), Ibn Hibbaan (5725), al-Haakim (5945) na at-Twabaraaniy (8214). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (1721).

[4] al-Bukhaariy (3464) na Muslim (2964).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 138-139
  • Imechapishwa: 02/11/2018