Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Viongozi na kiongozi wa waumini wanatakiwa kusikilizwa na kutiiwa sawa wawe wema au waovu. Yule mwenye kuchukua ukhaliyfah, watu wakakusanyika juu yake na wakaridhika nao na yule mwenye kuchukua uongozi kwa mabavu mpaka akawa khaliyfah anaitwa kiongozi wa waumini.”

MAELEZO

Kiongozi wa waumini anatakiwa kusikilizwa na kutiiwa. Ni mamoja ni mwema au muovu. Inahusiana na mtu ambaye Ummah umekusanyika juu yake mpaka akawa khaliyfah na mtu anayechukua uongozi kwa mabavu, akamfanyia uasi yule kiongozi aliyetangulia, akakabiliana naye mpaka nchi ikasimama. Haijuzu kuwafanyia uasi. Ukimfanyia mapinduzi kwa mara nyingine basi Ummah utatumbukia katika vita vya kuendelea. Kimsingi ni kwamba haifai kufanya uasi. Allaah akimsalitishia mtu kumfanyia mapinduzi kiongozi na akakabiliana naye na akasimamisha nchi mpya, waislamu wanawajibika kusimama katika mpaka huu na wajisalimishe na kiongozi huyu mpya ambaye amechukua uongozi kimabavu. Haijalishi kitu kiongozi huyu mpya ameipata nafasi yake kupitia uchaguzi, mashauriano au kupitia njia ya mabavu na nguvu mpaka akashika uongozi, basi itakuwa ni wajibu kujisalimisha chini yake na kuisalimisha damu ya waislamu. Ni mamoja awe mwema au muovu ni wajibu kutiiwa.

Tazama Imaam Ahmad, al-Bukhaariy na maimamu wa Uislamu wote namna ambavyo wanafanya kumtii mtawala ni msingi miongoni mwa misingi ya Uislamu pasi na kujali akiwa ni mwema au muovu.

Khawaarij, Raafidhwah na wengine wanaweza kukubali pale ambapo akiwa ni mwema na huenda wasikubali. Kwa mujibu wa Raafidhwah si Abu Bakr wala ´Umar hawakuwa wema. Kwa mujibu wa Khawaarij ´Aliy hakuwa mwema. Kwa ujumla ni wenye kukubaliana kwamba ni mwema. Hata hivyo wanatofautiana kama alikuwa mtenda dhambi. Kwa hali yoyote haijuzu kumfanyia uasi khaliyfah muislamu ambaye ni mtenda dhambi, mkandamizaji, mwenye kudhulumu na mtenda maasi maadamu bado ni muislamu. Kumethibiti juu ya hilo Hadiyth nyingi ikiwa ni pamoja vilevile na zifuatazo:

“Tulikula kiapo cha usikivu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kusikia na kutii katika mepesi na mazito, tuyapendayo na tuyachukiayo, tutapoona wengine wanapendelewa juu yetu na kutogombana na mwenye jambo lake mpaka pale tutapoona kufuru ya wazi.”[1]

[1] Muslim (1709).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 416-417
  • Imechapishwa: 11/10/2017