Swali 44: Nimepokea barua zako mbili na nimetafakari yale uliyoyataja ndani yake ambapo mmetofautiana juu ya hukumu ya kutekeleza swalah ya ijumaa katika vijiji na mnataka hukumu yangu katika jambo hilo[1].

Jibu: Namwomba Allaah atujaalie sisi na nyinyi kuwa miongoni mwa walinganizi wa uongofu na wanusuraji wa haki, atutunuku sote uelewa katika dini Yake na uimara juu yake. Kwani Yeye ndiye mbora Awezaye kusimamia jambo hilo. Haifichikani kwamba haki ni kitu kilichompotea muumini na pale anapokipata hukichukua. Haifichikani pia kwamba marejeo katika mambo yaliyo na tofauti ni Qur-aan na Sunnah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[3]

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: ”Mtiini Allaah na mtiini Mtume, mkigeukilia basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa; na mkimtii mtaongoka na hapana juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi.”[4]

Nimezingatia dalili za pande mbili zinazosema kuwa ni lazima kuswali swalah ya ijumaa katika vijiji na wanaosema kuwa sio lazima na si sahihi. Nimeona dalili na wale wenye maoni ya kwanza – nao ndio wengi zaidi – ndio ziko wazi, nyingi na sahihi zaidi. Miongoni mwa mamb yanayoweka wazi jambo hilo ni kwamba Allaah (Subhaanah) amefaradhisha juu ya waja Wake kutekeleza swalah ya ijumaa pale aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ

“Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya swalah siku ya ijumaa, basi kimbilieni kumtaja Allaah na acheni biashara.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakome watu kuacha [swalah za] ijumaa au Allaah atazipiga muhuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa waghafilikaji.”[6]

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali swalah ya ijumaa Madiynah ambapo hapo mwanzoni baada ya Hijrah ilikuwa na hukumu kama ya kijiji. Alimkubalia As´ad bin Zaraarah kuswali swalah ya ijumaa Naqiy´ al-Khadhwamaat ambayo ilikuwa na hukumu kama ya kijiji. Haikuthibiti kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza jambo hilo. Hadiyth juu ya hilo cheni ya wapokezi wake ni nzuri[7]. Amekosea ambaye ameitia kasoro kwa Ibn Ishaaq. Kwa sababu imethibiti kuweka wazi kusikia. Hivyo ile shubuha ya ubabaishaji inakuwa yenye kuondoka.

Isitoshe yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalani kama mlivyoniona nikiswali.”[8]

Tulimuona akiswali swalah ya ijumaa Madiynah wakati alipohamiaeko.

Jengine yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakubalia watu wa Jawaathaa ambacho ilikuwa ni kijiji moja wapo cha Bahrayn kuswali swalah ya ijumaa. Hadiyth juu ya hilo imepokelewa katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy.

Aidha ni moja kati ya zile swalah tano katika siku ya ijumaa. Kwa hiyo inawalazimu watu wa kijijini kama ilivyo kwa watu wa mjini. Ni kama swalah ya Dhuhr juu ya kila mmoja katika siku isiyokuwa ya ijumaa. Aliacha kuitekeleza mashambani na safarini kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaamrisha watu wa mashambani na wasafiri kuiswali. Aidha hakuitekeleza alipokuwa safarini. Hivyo ndivo ikawajibika kuitekeleza mbali na hali hizo. Kama inavotambulika mbali na hali hizo ni vijiji na miji. Jengine ni kwamba kuiswali kuna manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuwakusanya watu wa kijiji katika msikiti mmoja, kuwapa mawaidha na kuwakumbusha kila wiki kwa yale Allaah aliyowawekea katika Shari´ah katika Khutbah ya ijumaa.

Kutokana na zile dalili tulizozitaja itamkuia wazi usahihi wa maoni ya wanazuoni wengi kila ambaye ana inswafu na kwamba ndio iko karibu zaidi na haki kuliko maoni ya wale waliokwenda kinyume nao, kwamba ndio yenye manufaa zaidi kwa waislamu katika jambo la dini na dunia yao na kwamba ndio ilio karibu zaidi na kuitakasa dhimma na kutengemaa kwa Ummah.

Kuhusu Athar ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ni yenye kutoka kwake. Haikusihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama walivobainisha wengi akiwemo an-Nawawiy (Rahimahu Allaah). Ingawa kuhusu kusihi kutoka kwake ni jambo lenye walakini pia. Kwa sababu katika cheni ya wapokezi wake kwa ´Abdur-Razzaaq ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) hajasema wazi kwamba alisikia. Isitoshe ni mwenye kusifika jambo la Tadliys. Jaabir al-Ja´fiy na Haarith al-A´uur wote ni wanyonge. Katika cheni ya wapokezi wake kwa Ibn Abiy Shaybah al-A´mash ambapo hajasema wazi kwamba alisikia. Naye ni Mudallis anayejulikana. Lakini kule kusimulia kwake kwa kutotaja majina na ath-Thawriy kutotaja majina kunafasiriwa kusikia kwa yale ambayo al-Bukhaariy na Muslim (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wamepokea kutoka kwake katika “as-Swahiyh” zao. Katika vitabu vyengine hakuna kikwazo cha kuyaweka walakini mapokezi yao ikiwa hawakuweka wazi jambo la kusikia. Haya ndio yaliyonidhihirikia.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/359-362).

[2] 04:59

[3] 42:10

[4] 24:54

[5] 62:09

[6] Muslim (1432), an-Nasaa´iy (1353) na Ibn Maajah (786).

[7] Abu Daawuud (1069), Ibn Maajah (1082), Ibn Khuzaymah (1724) na al-Haakim (1039).

[8] al-Bukhaariy (696) na ad-Daarimiy (1225).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 90-94
  • Imechapishwa: 06/12/2021