9 – Ni wajibu wake katika Twawaaf kujisiri kikamilifu, kuteremsha sauti, kuteremsha macho na asisongamane na wanaume na khaswakhaswa pale mbele ya jiwe au kona ya upande wa yemeni. Kutufu sehemu za mwisho za kutufu pasi na kusongamana na watu ndio bora kwake kuliko kutufu karibu na Ka´bah na huku anasongamana na watu. Kwa sababu kusongamana na watu ni haramu kutokana na ile fitina inayopatikana ndani yake.

Ama kuisogelea Ka´bah na kubusu jiwe ni mambo mawili yaliyosuniwa ikiwepesika kufanya hivo. Asifanye jambo la haramu kwa ajili ya kutaka kufanya Sunnah. Bali katika hali kama hii sio Sunnah juu yake. Katika hali kama hii Sunnah juu yake ni yeye kuliashiria kwa mkono wake akilikabili.

“Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´”:

“Wenzetu wamesema kwamba si Sunnah kwa mwanamke kulibusu jiwe wala kulishika isipokuwa tu pakiwa patupu pale pahali pa kutufu usiku au wakati mwingine kutokana na yale madhara yanayopatikana juu yake na kwa wengine.”[1]

Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Imependekezwa kwa mwanamke kutufu usiku. Kwa sababu ni sitara zaidi kwake na msongamano mchache na hivyo anaweza kuisogelea Ka´bah na kuligusa jiwe.”[2]

10 – Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Kutufu kwa mwanamke na kufanya kwake Sa´y ni kutembea kote. Ibn-un-Mundhir amesema: “Wanachuoni wameafikiana juu ya kwamba hakuna wale wenye kukimbiakimbia kwa wanawake si karibu na Ka´bah wala baina ya Swafaa na Marwah wala hakuna jambo la kuacha bega la kulia wazi. Kwa sababu msingi wa mambo hayo ni kudhihirisha ushujaa na hayo hayakusudiwi juu ya mwanamke. Jengine ni kwa sababu kunakusudiwa juu ya wanawake kujisitiri na katika kukimbiakimbia na kuacha bega moja wazi kunapelekea kubaki wazi.”[3]

[1] (08/37).

[2] (03/331).

[3] (03/394).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 13/11/2019