Ya pili: Kigawanyo cha pili katika shirki ndogo ni shirki iliyojificha. Ni shirki katika matakwa na makusudio. Ni kujionyesha na kutaka kusikika. Ni kama mfano mtu afanye kitendo miongoni mwa yale anayojikurubisha kwayo mtu kwa Allaah na huku anataka watu wamsifu. Kama mtu kuipamba swalah yake au akatoa swadaqah ili watu wamsifie. Au akatamka matamshi na akasoma kwa sauti nzuri ili watu wamsikie na baadaye wamsifu na kumtapa. Kujionyesha kukichanganyikana na kitendo kunakiharibu. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo basi yule anayetaraji kukutana na Mola wake, basi na atende matendo mema na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kikubwa ninachokikhofia juu yenu ni shirki ndogo.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni ipi shirki ndogo? Akasema: “Ni kujionyesha.”[2]

Miongoni mwazo kunaingia vilevile kufanya kitendo kwa ajili ya tamaa ya kidunia. Kama mfano wa anayehiji, akaadhini, akawaswalisha watu kwa ajili ya mali, akajifunza elimu ya dini au akapambana kwa jili ya mali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ameangamia mja wa dinari! Ameangamia mja wa dirhamu! Ameangamia mja wa Khamiyswah! Ameangamia mja wa Khamiylah! Akipewa huridhia na kama hakupewa hukasirika.”[3]

Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusu shirki katika matakwa na nia ni bahari isiyokuwa na ufuo. Ni wachache mno wanaosalimika. Mwenye kutaka kwa kitendo chake usiokuwa uso wa Allaah na akanuia kitu mbali na kujikurubisha Kwake na akataka malipo kwacho, basi ameshirikisha katika nia na utashi wake. Kumtakasia nia Allaah ni yeye amtakasie Allaah katika matendo yake, maneno yake, matakwa yake na nia yake. Hii ndio Haniyfiyyah mila ya Ibraahiym ambayo Allaah amewaamrisha waja Wake wote na hakubali kutoka kwa yeyote isiyokuwa hiyo. Kwani ndio uhakika wa Uislamu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitokubaliwa kutoka kwake naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[4]

Hiyo ndio mila ya Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo yule mwenye kuipa mgongo, basi ni mpumbavu mkubwa miongoni mwa wapumbavu.”[5]

Kutokana na yaliyotangulia tunafupisha kwa kusema kwamba kuna tofauti kati ya shirki kubwa na shirki ndogo, nazo ni zifuatazo:

1- Shirki kubwa inamtoa mtu nje ya Uislamu na shirki ndogo haimtoi mtu nje ya Uislamu. Lakini hata hivyo inaipunguza Tawhiyd.

2- Shirki kubwa inamdumisha mwenye nayo Motoni na shirki ndogo haidumishi mwenye nayo ndani yake ikiwa ataingia.

3- Shirki kubwa inaharibu matendo yote na shirki ndogo haiharibu matendo yote. Kinachoharibu ni kujionyesha na kitendo kwa ajili ya dunia kitendo kilichochanganyikana nacho peke yake.

4- Shirki kubwa inahalalisha damu na mali na shirki ndogo haihalalishi viwili hivyo.

[1] 18:110

[2] Ahmad (23686).

[3] al-Bukhaariy (2887).

[4] 03:85

[5] al-Jawaab al-Kaafiy, uk. 115.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 11/03/2020