43. Sifa kamilifu za Allaah


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Naye yujuu kabisa, Aliyetukuka, Mjuzi wa yote, Mwenye khabari ya kila kitu ambaye anakiendesha kila kitu, Muweza, Mwenye kusikia, Mwenye kuona, Aliye juu, Aliye mkubwa.

MAELEZO

Yeye yuko juu ya viumbe Wake kwa dhati Yake, uwezo na utawala.

Yeye ni Mtukufu; hakuna kikubwa kumshinda (Subhaanahu wa Ta´ala).

Yeye ni Mjuzi wa kila kitu na Mwenye khabari ya hali zote za viumbe Wake.

Anawaendesha viumbe Wake. Hakuna kinachotikisika wala kutulizana, kudondoka wala kupanda isipokuwa kwa idhini Yake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hakuna mwanamke yeyote anayebeba mimba na wala hazai isipokuwa kwa ujuzi Wake na hapewi umri mrefu yeyote yule mwenye umri mrefu na wala hapunguziwi katika umri wake isipokuwa yamo katika Kitabu – hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[1]

Kitabu kusudiwa hapa ni Ubao uliohifadhiwa. Alianza kwanza kukijua kila kitu baadaye ndio akayaandika katika Ubao uliohifadhiwa. Kwa hivyo ni Mwenye kukiendesha kila kitu.

Uwezo wa Allaah ni mkubwa. Hakuna chochote kinachomshinda ardhini wala mbinguni. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake ardhini wala mbinguni. Yale anayoyataka, huwa, na yale asiyoyataka, hayawi. Kuhusu viumbe, wanaweza kuyataka mambo lakini wasiyaweze. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika si venginevyo amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.”[2]

Kwa hivyo Yeye ni muweza (Subhaanahu wa Ta´ala). Pale anapolitaka jambo basi husema tu: “Kuwa!” – na kikawa.

Allaah ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Haya ni majina mawili yaliyobeba sifa mbili; ya kusikia na ya kuona. Kiumbe pia ni mwenye kusikia na ni mwenye kuona. Lakini kusikia na kuona kwa Allaah sio kama kusikia na kuona kwa kiumbe. Sifa za kiumbe ni zenye kuendana na yeye na sifa za Allaah ni zenye kuendana na Yeye. Majina pekee ndio yenye kushirikiana lakini hata hivyo uhakika na namna ni vyenye kutofautiana. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا

“Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu, hivyo tukamjaalia mwenye kusikia na kuona.”[3]

Allaah pia ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Hata hivyo majina na sifa za Allaah si zenye kufanana na majina na sifa za viumbe. Ijapo majina ni yenye kushirikiana lakini uhakika na namna ni vyenye kutofautiana.

Allaah yujuu. Yuko juu ya viumbe Wake. Yeye anao ujuu wa moja kwa moja; ujuu wa dhati, wa hadhi na wa utawala. Aina zote hizi tatu za ujuu zimethibiti kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Allaah ni Mkubwa. Hakuna kikubwa zaidi kumshinda Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Ndio maana unasema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Bi maana ni mkubwa kuliko kila kitu. Hakuna yeyote ambaye ni mkubwa kuliko Allaah.

[1] 35:11

[2] 36:82

[3] 76:2

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 36
  • Imechapishwa: 28/07/2021