43. Mwenye busara na kumtegemea kwake Allaah

1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah amekadiria makadirio miaka 50.000 kabla ya kuumba mbingu na ardhi.”

2 – Ni wajibu kwa yule mwenye busara daima amtegemee Yule Aliyejibebesha jukumu la ruzuku. Kwani utegemezi ndio mpangilio wa imani na ni jambo linalokwenda sambamba na Tawhiyd. Utegemezi ndio sababu inayotokomeza umasikini na kuleta utulivu.

3 – Hakuna yeyote atakayemtegemea Allaah (Jalla wa ´Alaa) kutokana na moyo salama kiasi cha kwamba akaamini yale ambayo Allaah amedhamini zaidi kuliko vile anavyoamini yaliyomo mkononi mwake, isipokuwa Allaah hamwachi kwa viumbe wake na badala akamruzuku kwa njia asiyoitarajia.

4 – Abuud-Dardaa´ amesema:

”Riziki humtafuta mwenye nayo kama ambavo kifo kinavomtafuta.”

5 – Mwenye busara anatambua kwamba riziki imekwishapangwa na Allaah akadhamini kuwahifadhia nayo waja Wake katika ule muda ambao wanaihitajia.

6 – al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Kufikiria juu ya riziki yangu kamwe hakukuwahi kunitikisa.”

7 – Ni wajibu kwa mwenye busara kutambua kwamba sababu inayomfanya yule mwenye kushindwa kufikia haja yake ndio inayomzuia yule mwenye maamuzi kutokamana na kufanya hivo. Kwa hivyo mwenye busara hatakiwi kuhuzunika juu ya kitu anachokitamani lakini akakikosa au kile anachokitaka lakini kikampata. Kitu cha kidunia kitamjia mtu pasi na kukichokea.

8 – Yamaan an-Najraaniy amesema:

“Nilimpitia mtawa katika jangwa na mimi nikiwa na njaa. Nikasema: “Ee mtawa! Je, una kilichobaki?” Akanipa kikapu kilichokuw na mkate nusu. Nikala kutoka humo na nikampa kilichobaki. Akasema: “Chukua akiba iliyobaki njiani.” Nikasema: “Ambaye amenipa chakula mahali hapa kusipokuwa na mtu atanipa chakula ninaposhikwa na njaa ilihali sina kitu.”

9 –  Utegemezi ni kule kukata mafungamano kwa kuwatupilia mbali viumbe na kuonyesha haja yako kwa Allaah peke yake. Pengine mtu akawa ni tajiri na anamtegemea kikweli Allaah wakati anaona kulingana sawa utajiri na umasikini vyote viwili; anashukuru wakati wa kupata na anaridhika wakati wa kukosa. Anaweza kuwa mtu mwengine ambaye hamiliki chochote katika vitu vya dunia. Hamtegemei Allaah ikiwa anapendelea utajiri zaidi kuliko umasikini. Haridhiki wakati anapokuwa katika hali ya umasikini na wala hashukuru wakati anapokuwa tajiri.

10 – Nafiy´ bin Khaalid amesema:

“Tulikuwa tumeenda kutembea kwa Rabiy´ah al-´Adawiyyah na tukaongelea sababu za kupata riziki. Tukawa tunazungumza na yeye amenyamaza. Tulipomaliza akasema: “Khasara kwa yule anayedai kumpenda kisha akamfikiria vibaya juu ya riziki Yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 153-155
  • Imechapishwa: 11/08/2021