43. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya wakeze Mtume, Ahl-ul-Bayt na Maswahabah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni:

Wenye nyoyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama Alivyowasifia Allaah katika Kauli Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

”Na wale waliokuja baada yao ni wenye kusema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (59:10)

Na kumtii vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kauli yake:

“Msiwatukane Maswahabah zangu! Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu sawa na [mlima wa] Uhud, haitofikia Mudd[1] iliotolewa nao wala nusu yake.”[2]

Wanayakubali yaliyokuja katika Kitabu, Sunnah na Ijmaa´ kutokana na fadhila na nafasi zao. Wanawafadhilisha waliojitolea na kupigana vita kabla ya ushindi – nayo ni suluhu ya Hudaybiyah – wao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao waliojitolea baadae na wakapigana. Na wanawatanguliza Muhaajiruun juu ya Answaar. Wanaamini ya kwamba Allaah Kawaambia wale waliopigana vita vya Badr – na walikuwa miatatu na kumi na kitu:

“Fanyeni mtakacho. Nimeshawasamehe.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema kuwa:

“Hakuna yeyote kati yenu atoae bay´ah [kiapo cha usikivu na utiifu] chini ya mti atakayeingia Motoni.”[4]

Bali Yuko radhi nao, nao wako radhi Naye na walikuwa zaidi ya elfu moja na mianne.

Na wanamshahidilia Pepo yule ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kamshahidilia, kama wale (Maswahabah) kumi, na Thaabit bin Qays bin Shimmaas na Maswahabah wengineo.

Na wanayathibitisha yale yaliyopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhu) na wengine, ya kwamba mbora wa Ummah huu baada ya Mtume wake ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan na halafu ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum), kama zilivyotolea dalili hivyo Aathaar. Hali kadhalika kama walivyokubaliana Maswahabah kumtanguliza ´Uthmaan kwa kumpa bay´ah, pamoja na kuwa baadhi ya Ahl-us-Sunnah wametofautiana kwa ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) – baada ya kukubaliana kwao kumtanguliza Abu Bakr na ´Umar – ni nani aliyebora. Kuna baadhi ambao wamemtanguliza ´Uthmaan kisha baada ya hapo wakanyamaza au wakasema kuwa wanne ni ´Aliy. Na baadhi ya wengine wakamtanguliza ´Aliy na wengine wakasimama.

Lakini, mwishoni walikubaliana Ahl-us-Sunnah kumtanguliza ´Uthmaan kisha ´Aliy, hata kama masuala haya – kuhusu ´Uthmaan na ´Aliy – wengi katika Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa sio ya msingi ambayo atahukumiwa upotevu yule atakayeyakhalifu, lakini masuala ambayo mtu atahukumiwa upotevu ni masuala ya Uongozi. Hili ni kwa sababu wanaamini ya kwamba Khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan na kisha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Atayakekashifu uongozi wa mmoja katika maimamu hawa, basi ni mpotevu kuliko punda wa kufugwa.

Wanawapenda na kufanya urafiki na watu wa familia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanafuata wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema siku ya Ghadiyr Khumm:

“Ninawakumbusha kwa Allaah kuhusiana na watu wa familia yangu! Ninawakumbusha kwa Allaah kuhusiana na watu wa familia yangu!”[5]

Kamwambia hali kadhalika mtoto wa ami yake Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye alikuwa amekuja kushtaki ya kwamba baadhi ya Quraysh wanawachukia Banuu Haashim. Akasema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye Nafsi yangu iko Mkononi Mwake. Hawatoamini mpaka wawapende kwa ajili ya Allaah na kwa ukaribu wenu kwangu.”[6]

Na amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah Kawachagua Banuu Ismaa´iyl. Na kutoka Banuu Ismaa´iyl Amechagua Kanaanah. Na kutoka Kanaanah Amechagua Quraysh. Na kutoka Quraysh Amechagua Banuu Haashim na Amenichagua mimi kutoka Banuu Haashim.”[7]

Hali kadhalika wanawapenda na kufanya urafiki na wake za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wao ni wamama wa waumini. Na wanaamini ya kwamba wao ndio wakeze Aakhirah, na khususan Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ni mama wa watoto wake wengi. Na yeye ndiye alikuwa wa kwanza kumuamini na kumsaidia kwa kazi yake na alikuwa ni mwenye manzilah ya juu kwake.

Na asw-Swiddiyqah bint asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhumaa), ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Ubora wa ´Aaishah kwa kulinganisha na wanawake wengine ni kama ubora wa Thariyd kulinganisha na chakula chengeni.”[8]

Na wanajitenga mbali na njia ya Raafidhwah, ambao wanawachukia na kuwatukana Maswahabah, hali kadhalika Nawaaswib, ambao wanawaudhi watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ima kwa kauli au matendo.

Na wanayanyamazia yaliyopitika baina ya Maswahabah na wanasema:

“Kati ya mapokezi haya yaliyopokelewa kuna ambayo ni ya uongo, na kuna ambayo yamezidishwa juu yake na kupunguzwa, na kuna ambayo yamebadilishwa kwa sura yake ya kihakika na ndani yake kuna ya sahihi ambayo wamepewa udhuru kwayo. Ima walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakapatia, au walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakakosea.”

Wao pamoja na hivyo hawaitakidi ya kwamba kila mmoja katika Maswahabah kakingwa na dhambi kubwa au ndogo. Bali kinyume chake kuna uwezekano wakafanya dhambi kwa ujumla. Wana haki ya kutangulizwa na fadhila ambazo zinafanya wanasamehewa kwa lile wangelolifanya – ikiwa wamefanya kitu. Wanasamehewa hata madhambi ambayo yasingelisamehewa kwa mwengine yeyote baada yao, kwa kuwa wana mema mengi ambayo hana yeyote wa baada yao, na ambayo vilevile yanafuta makosa yao.

Kumethibiti kwa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba wao ndio karne bora na kwamba akitoa Swadaqah mmoja wao kiasi cha Mudd ina uzito zaidi kuliko inayotolewa na aliye baada yao, hata kama huyu atatoa dhahabu sawa na kiasi cha mlima wa Uhud.

Ikiwa mmoja wao atapitikiwa na dhambi, atakuwa ima katubia kwa dhambi hiyo, au kaleta mema ambayo yameifuta au amesamehewa kwa fadhila za kutangulia kwake, au [kasamehewa] kwa uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na hakuna ambaye ana haki zaidi ya uombezi wake isipokuwa wao – au kapewa mtihani kwa majaribio ya duniani ambayo yamefuta dhambi yake.

Ikiwa madhambi haya yaliyofanywa yanafanywa namna hii, vipi kwa mambo ambayo walikuwa ni wenye kujitahidi kuifikia haki? Ikiwa wamepatia wana ujira mara mbili na wakikosea wana ujira mara moja na kosa lao limesamehewa. Isitoshe, matendo mabaya yaliyofanywa na baadhi yao ni machache mno na yasiyokuwa na maana ukilinganisha na fadhila za nafasi yao na mema yao, kama kwa mfano kumuamini Allaah na Mtume Wake, na kupigana Jihaad katika njia ya Allaah, Hijrah, nusra, elimu yenye manufaa na matendo mema n.k. Yule atakayetazana historia ya Maswahabah kwa elimu na umaizi na fadhila Alizowaneemesha Allaah kwazo, basi atajua kwa yakini ya kwamba wao ndio viumbe bora baada ya Mitume. Kamwe hakupatapo kuwepo na hakutokuwepo mtu mfano wao. Wao ndio wasomi wa wasomi katika Ummah huu – ambao ndio watu bora na wa karimu kwa Allaah (Ta´ala).

MAELEZO

Mlango huu ni miongoni mwa milango bora na muhimu kabisa ya kitabu hiki ambacho ni “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” kuhusiana na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ndani yake mna Radd kwa Raafidhwah na Nawaaswib. Vilevile ndani yake mna ubainifu wa fadhila na manzilah zao (Radhiya Allaahu ´anhum). Ni mlango mkubwa. Mwandishi amefanya vizuri kabisa kwa kuleta ibara ambazo ziko wazi na bainifu zaidi.

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah… – Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni wenye mioyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mioyo yao iko salama. Wanawapenda na kuwatakia radhi. Kwa sababu kuwapenda ni sehemu katika dini (Radhiya Allaahu ´anhum). Wao ndio wabebaji wa Shari´ah na karne bora. Kwa ajili hiyo ndio maana kuwapenda ikawa ni dini. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawapenda kwa ajili ya Allaah na mioyo yao iko salama juu yao. Ni wenye mapenzi tele juu yao. Ndimi zao ziko salama kwa njia ya kwamba hawawatukani na wala hawawatii kasoro. Badala yake wanawatakia radhi na kuwaombea du´aa. Kwa sababu kufanya hivyo ni kumtii Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na Mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.” (49:10)

Isitoshe wanatekeleza wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Msiwatukane Maswahabah zangu! Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu sawa na (mlima wa) Uhud, haitofikia Mudd iliotolewa nao wala nusu yake.”

Hii ni moja katika sifa ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni wenye ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio viumbe bora baada ya Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Hakupatapo kuwepo na wala hakutokuwepo mfano wao (Radhiya Allaahu ´anhum).

Lililo la wajibu ni kuwapenda kwa ajili ya Allaah, kuwaombea radhi, kunyamazia mizozo iliyopitika kati yao na kuamini kuwa wao ndio karne bora.

Na wanayathibitisha yale yaliyopokelewa kwa njia nyingi… – Kadhalika inatakiwa kuamini ya kwamba mbora katika makhaliyfah waongofu ni asw-Swiddiyq, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan halafu ´Aliy. Licha ya kwamba kuna baadhi ya watu waliovutana kidogo kama inatakiwa kumtanguliza ´Uthmaan juu ya ´Aliy au kinyume chake. Lakini hatimaye Ahl-us-Sunnah walifikia kuona kuwa kuwa ´Uthmaan ndiye watatu na kwamba ´Aliy ndiye wanne. Hili linahusiana na uongozi na ubora.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanatakiwa kuamini hivi na wajitenge mbali na mwenendo wa Raafidhwah ambao kazi yao wao ni kuwatukana Maswahabah na kuwafanyia maudhi. Vilevile wanatakiwa kujitenga mbali na mwenendo wa Nawaaswib ambao wanawaudhi watu wa nyumba ya kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno na vitendo. Ahl-us-Sunnah wanatakiwa kujiepusha na tabia hii chafu.

Na wanamshahidilia Pepo… – Kadhalika wanamshuhudilia yule ambaye ameshahidiliwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Pepo ikiwa ni pamoja na wale Maswahabah kumi, Thaabit bin Qays bin Shammaas, ´Abdullaah bin Salaam, ´Ukkaashah bin Muhswan na wengineo ambao wameshahidiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanatakiwa kushahidiliwa. Ambaye kumethibiti kushahidiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anashahidiliwa.

Wanayakubali yaliyokuja katika Kitabu, Sunnah na Ijmaa´… – Kadhalika wanaamini yaliyothibiti kuhusu watu wa vita vya Badr ambapo waliambiwa:

“Fanyeni mtakacho. Nimeshawasamehe.”

Vilevile wanaamini kuwa hatoingia Motoni yeyote ambaye alitoa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti. Hii ni ile bay´ah ya Ridhwaan. Kwa sababu imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Hakuna yeyote kati yenu atoae bay´ah chini ya mti atakayeingia Motoni.”

Sivyo tu, bali Allaah akateremsha kuhusu wao:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا

“Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe chini ya mti, [Allaah] Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao, basi Akawateremshia utulivu na Akawapa ushindi wa karibu.” (48:18)

Yote haya ni katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Ni wajibu kwa watu wa imani baada yao kufuata mfumo wao na waamini kuwa Maswahabah wote ndio wabora wa Ummah na wenye fadhila zaidi.

Na wanayanyamazia yaliyopitika baina ya Maswahabah… – Kuhusiana na kasoro zenye kusimuliwa kutoka kwa baadhi ya Maswahabah ni chache sana ukilinganisha na kheri nyingi alizowapa Allaah, fadhila zao na matendo yao makubwa. Aliyofanya mmoja wao ima atakuwa alitubia kwayo, alifanya jema lililofuta ovu hilo, alisamehewa na fadhila za kutangulia kwake, atapata uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kwani wao ni wenye haki zaidi ya kupata uombezi wake – au kwa sababu ya mitihani ya maradhi na mengineyo ambayo yalifanya akasamehewa. Hivi ndivyo wanavyoonelea Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika masuala haya yaliyotajwa na mwandishi (Rahimahu Allaah).

Muumini anatakiwa kuuhifadhi mlango huu vizuri na atendee kazi maana yake. Vilevile ´Aqiydah yake inatakiwa iwe imebobea ili aweze kutofautiana na Ahl-ul-Bid´ah wote ikiwa ni pamoja na Raafidhwah, Nawaaswib na wazushi wengine ambao dhana zao zimefeli au wamevuka mipaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama wanavyofanya Raafidhwah. Wengine dhana zao zikafeli, wakazembea kunako haki zao, kama wanavyofanya Khawaarij, Mu´tazilah na mfano wao miongoni mwa wale ambao wana maneno na matendo machafu juu ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kizazi chake (Radhiya Allaahu ´anhum). Tunamuomba Allaah awawie radhi na atujaalie kuwa ni miongoni mwa wenye kuwafuata kwa wema.

[1] Imaam ´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema: ”Mudd ni sawa na kama robo hivo.” (Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah (02/252) iliyochapishwa na Daar Ibn-ul-Jawziy).

[2] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

[3] al-Bukhaariy (3007) Muslim (2494).

[4] Abuu Daawuud (4649) na (4650), at-Tirmidhiy (3748) na (3757), Ibn Maajah (134) na wengine. Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika “Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (4010).

[5] Muslim (2408).

[6] Ahmad katika ”Fadhwaail-us-Swahaabah” (1756).

[7] Muslim (2276).

[8] al-Bukhaariy (3770) na Muslim (2446).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com