43. Hakuna awezae kufikia ngazi ya Maswahabah


Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wale waliotangamana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakamuona kwa macho (hata kama ni kwa muda mchache), wakamsikia na wakamuamini ni wabora kuliko wale waliokuja baadaye ambao hawakumuona hata kama watatenda matendo mazuri yote.”

Yule mkubwa kabisa ambaye amekuja baadaye hamfikii yule swahabah aliye chini kabisa hata kama huyo mkubwa kabisa atafanya matendo mazuri yote. Ikiwa dhahabu zetu zilizo sawa na mlima wa Uhud hazifikii hata vitanga viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake, ina maana ya kwamba hatuwezi kufikia ngazi yao hata kama watatoa kitanga kimoja cha mkono. Mtu asemeje ikiwa watatoa yote waliokuwa wakimiliki? Kuna Maswahabah waliotoa yote waliokuwa wakimiliki. Kuna wengine waliojitolea nusu ya mali yao yote. Kuna wengine walioandaa jeshi, kama alivyofanya ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Walijitolea mali zao kwa ajili ya Allaah. Lau mmoja wao atajitolea tende, kitanga kimoja cha mkono au kitu kingine basi yule aliyekuja baadaye hawezi kufikia ngazi hii.

Imamu huyu alitambua nafasi walionayo Maswahabah. Ni wajibu kwetu vilevile kutambua nafasi na ngazi yao na tutambue kuwa wao ndio watu bora kabisa baada ya Mitume. Utu haukuwahi kamwe kuwa na watu mfano wao mbali na Mitume. Kamwe hakukuwahi kuwa watu wenye imani, yakini, Ikhlaasw  na mapambano kama wao. Kupitia wao Allaah ameifungua mioyo na miji. Ummah unanawiri kwa ujumbe walioufikisha kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mapambano yao kwa ajili ya dini hii. Kwa ajili hiyo wana kila haki ya maadhimisho na heshima kutoka kwetu. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba tunapenda na kuchukia kwa ajili yao.

Kuanzia hapa Ahl-us-Sunnah wanasema yule mwenye kumponda swahabah mmoja tu ni zandiki. Mtu asemeje kwa yule anayewatukana, anawaponda na kuwakufurisha Maswahabah? Yule mwenye kumponda swahabah mmoja tu ni Raafidhwiy khabithi.  Heshima ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inatakiwa kulindwa. Hivyo pasi na shaka ndivyo mambo yalivyo kwa kuzingatia ya kwamba Allaah amewaridhia, amewaahidi Pepo na kuwapa ngazi hii kubwa. Maswahabah walikuwa wakizinduana wao kwa wao juu ya hili. Waliokuja baadaye walilitambua hili. Wanachuoni wa ummah wa kale walilitambua hili. Takataka tu, wajinga, wapotevu na mazanadiki ndio wenye chuki dhidi ya watu hawa. Ndio maana kuwachukia Answaar ni alama ya unafiki na kuwapenda Answaar ni alama ya imani. Kusemwe nini inapokuja katika msimamo kwa Muhaajiruun? Kuwapenda kuna haki zaidi kuwa ni imani na kuwachukia kuna haki zaidi kuwa ni unafiki. Mtu asemeje chuki na uadui huu ukianzia kwa Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy na ndugu zao katika wale Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakubwa? Watu hawa wanaona kuwa mayahudi wafuasi wa Ibn Sabaa´ ni bora kuliko Abu Bakr na ´Umar. Kwa mujibu wao masomo ya Ibn Sabaa´ myahudi ni bora kuliko masomo ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Masomo ya Raafidhwah na masomo ya Khawaarij yanatoka katika masomo ya Ibn Sabaa´. Raafidhwah na Khawaarij walifanya uasi kwa ´Uthmaan. Wote ni wanafunzi wa Ibn Sabaa´. Kwa mujibu wao Ibn Sabaa´ alitoa watu wengi ambao ni waumini na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa waumini watatu, wane au kumi tu. Hivyo ndivyo wanavyosema Raafidhwah.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 413-414
  • Imechapishwa: 11/10/2017