43. Fadhila za Maswahabah na Radd kwa wale wenye kuwaponda


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

15- Sema “Watu bora baada ya Muhammad

    ni mawaziri wake, kisha ´Uthmaan [ndio maoni] yenye nguvu

16- Wanne wao ni kiumbe bora anayekuja baada yao

     ´Aliy kiongozi mwema kwa kheri”

MAELEZO

Huu ni utafiti juu ya haki ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Nao si wengine ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ndio karne bora. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wenu ni karne yangu, kisha wataofuatia, kisha wataofuatia.”[1]

Mpokezi anasema:

“Sikumbuki baada ya karne yangu alitaja karne mbili au tatu.”

Bi maana inakuwa karne nne. Zinaitwa kuwa ni karne bora kutokana na Hadiyth hii.

Bora katika karne hizi ni ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Allaah amewasifu katika Kitabu Chake (Radhiya Allaahu ´anhum). Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Na wale waliotangulia awali katika Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani ipitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” (09:100)

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na  [zikataifishwa] mali zao wanatafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli.” (59:08)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amewasifu na kuwatapa ya kwamba:

أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Hao ndio wakweli.”

Amefungamanisha ukweli kwao kwa vile waliuhakikisha. Hii ni dalili yenye kuonesha fadhila na nafasi walizo nazo kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Halafu anakuja zandiki na mkanamungu mmoja ambaye anadai Uislamu na kuwahujumu Maswahabah na kuwasema vibaya. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Hao ndio wakweli.”

Jitu hili linamkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall).

Amesema (Jalla wa ´Alaa) kuhusu Answaar:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ

“Na wale waliokuwa na makazi na wakawa na imani kabla yao… “

Bi maana mji wa kuhajiri. Nao ni Answaar al-Madiynah.

يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“… wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawapati kuhisi uzito wowote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wako na njaa. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.” (59:09)

Haya ni matapo na sifa kwa Answaar na kutajwa sifa zao nzuri. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amethibitisha juu yao kufaulu. Amesema:

وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.”

Ni dalili kwamba Allaah amewaepusha na ubakhili na tamaa ya uchu wa na nafsi zao mpaka wakawa:

وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ

“… na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wako na njaa.”

Wanazitanguliza haja za ndugu zao japokuwa wao wenyewe wako na njaa. Pindi ndugu zao walihama kwenda kwao basi wakawafungulia vifua na nyoyo zao. Sivyo tu bali wakawashirikisha katika mali zao na majumba yao – Allaah awawie radhi wote. Halafu akasema kuhusu wale waliokuja baada yao:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ

“Na wale waliokuja baada yao… “

Baada ya Maswahabah mpaka siku ya Qiyaamah:

يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“… wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.” (59:10)

Hapa kumebainisha kwamba lililo la wajibu kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni kuwaombea du´aa, kuwaombea msamaha, kutambua kutangulia kwao katika imani na kumuomba Allaah azitakase nyoyo zetu kutokamana na kuwa na chuki, vifundo na kuwachukia. Hapa kuna dalili ya kusifiwa kwa Maswahabah na kubainisha yaliyo ya wajibu kwa wale waliokuja baada yao mpaka siku ya Qiyaamah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Msiwatukane Maswahabah zangu. Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu mfano wa mlima wa Uhud hatofikia robo ya mmoja wao wala nusu yake.”[2]

Iwapo mmoja wenu atatoa swadaqah ya dhahabu mfano wa mlima wa Uhud kwa nia safi kabisa, akatoa yote, hatofikia mfano wa ujira na thawabu za Swahabah mmoja kwa kutoa robo au nusu ya chakula. Mlima wa dhahabu wa ambaye si Swahabah haufikii robo ya chakula cha mmoja wao. Hilo ni kutokana na fadhila na nafasi yao. Kwa sababu miongoni mwa sababu za ujira kuzidishwa ni ule utukufu ambao mtendaji yuko nao mbele ya Allaah.

[1] al-Bukhaariy (6690), (6428), (365) na (2651) na Muslim (2525) na (214)

[2] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (222) na (2541)