42. Maovu ya pili: Kufunika kuta kwa zulia

2- Kufunika kuta kwa zulia

Jambo la pili: Jambo la pili ambalo mtu anatakiwa kujiepusha nalo ni kufunika kuta kwa pazia na vitu mfano wake – hata kama itakuwa kwa kitu kingine kisichokuwa hariri – kwa sababu ni israfu na mapambo ambayo hayakuwekwa katika Shari´ah kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishiriki katika vita moja wapo. Wakati nikimtarajia kurudi nilichukua zulia langu ambalo lilikuwa na picha ambapo nikafunika upande mmoja wa ukuta. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoingia nilikutana naye katika chumba ambapo nikamwambia: “as-Salaam ´alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh, ee Mtume. Shukurani zote njema anastahiki Allaah ambaye ametukuza, akakunusuru dhidi ya maadui wako, akakutuliza macho yako na akakukirimu” lakini hata hivo hakunizungumzisha. Nikatambua usoni mwake kukasirika. Akaingia nyumbani kwa haraka na akalivuta pazia kwa nguvu mpaka likaanguka chini halafu akasema: “Unafunika kuta kwa pazia lililo na picha? Allaah hakutuamrisha kwa vile tulivyoruzukiwa tuvivishe mawe na saruji.” ´Aaishah anaendelea kusimulia: “Hivyo basi tukalikata pazia hilo[1] na kufanya mito miwili na tukalijaza na usumba. Mtume (Swallla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulitia hilo kasoro na alikuwa akiiegemea.”

Kwa ajili hii baadhi ya Salaf walikuwa wakikataa kuingia nyumba ambazo kuta zake zimefunikwa. Saalim bin ´Abdillaah:

“Nilifanya harusi wakati wa baba yangu na Abu Ayyuub alikuwa miongoni mwa waalikwa. Walifunika kuta za nyumba yangu kwa kitambaa cha kijani. Abu Ayyuub akakaribia na kuingia ndani ambapo akaniona nimesimama. Halafu akatazama na kuona nyumba imefunikwa na mazulia ya kijani ambapo akasema: “Ee ´Abdullaah! Mbona umefunika kuta?” Baba yangu akaona haya na akasema: “Ee Abu Ayyuub! Wanawake wametushinda.” Akasema: “Kuna ambao nilikuwa nachelea juu yao kushindwa na wanawake lakini sikuwa nikichelea juu yako kama wanawake watakushinda.” Kisha akasema: “Sintokula chakula  chenu na wala sintoingia nyumba yenu” halafu akatoka (Allaah amrehemu).”

[1] al-Bayhaqiy amesema:

“Tamko hili linafahamisha juu ya machukizo ya kufunika ukuta ijapokuwa sababu ya tamko kwa yale tuliyopokea kupitia njia za Hadiyth linafahamisha juu ya kwamba machukizo yalikuwa kutokana na ile picha iliyomo ndani yake.”

Machukizo yalikuwa katika mambo yote mawili kukiwemo hili alilotaja al-Bayhaqiy na kufunika uso kama ilivyo wazi katika zile ziada mbili ambazo tumezipokea katika baadhi ya njia za Hadiyth ya kwanza “… lililo na picha… “ na nyingine “Unafunika kuta… “ Mapokezi haya mawili yamekuanya sababu zote mbili. Lakini al-Bayhaqiy anapewa udhuru pengine hakuliona hilo. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Shaafi´iyyah akiwemo al-Baghawiy katika “Sharh-us-Sunnah” (02/218/03) pia wameonelea kuwa Hadiyth inafidisha juu ya machukizo ya kufunika ukuta kwa pazia. Shaykh Abu Naswr al-Maqdisiy ameweka wazi ya kwamba ni haramu kwa kutumia dalili Hadiyth hii kama ilivyo katika “al-Fath” (25/09). Tofauti hii inahusiana na pale pazia hilo litakuwa sio hariri wala dhahabu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Imechukizwa kutundika pazia juu ya milango pasi na haja kwa sababu ya kuwepo kufuli na vitu mfano wake. Vivyo hivyo kufunika pazia chumbani pasi na haja. Jambo likizidi juu ya haja inakuwa israfu. Je, inafikia katika uharamu? Ni jambo linahitajia kuangaliwa vizuri.” al-Ikhtiyaaraat (144)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 198-201
  • Imechapishwa: 19/04/2018