42. Maana ya swahabah


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Watu bora baada ya watu hawa ni Maswahabah wengine wote wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); karne ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwao.”

Bi maana baada ya wale kumi na wale walioshiriki katika Badr, Hudaybiyah na wengineo.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kila ambaye alisuhubiana naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwaka, mwezi, siku moja, saa au akapata kumuona tu ni swahabah wake.”

Watu hawa wana matangamano mafupi kuliko wale waliotangulia. Kushiriki kwao katika jihaad na vitani ni kuchache. Ngazi zao ni za chini. Lakini kwa sababu tu ya matangamano haya wanafikia ngazi ambayo ni kubwa kiasi cha kwamba hakuna yeyote awezaye kuifikia katika wale waliokuja baada yao pasi na kujali ni matendo gani atayoyafanya.

Hapa anaelezea maana ya swahabah na ni vipi anafikia ngazi hii kuu. Endapo atamuona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa muda mchache tu, sembuse iwapo atasuhubiana nae mwaka mmoja, mwezi mmoja, siku moja au saa. Maana sahihi ya swahabah ni yule aliyemuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamuamini na akafa hali ya kuwa ni muislamu. Iwapo atamuona tu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kupokea kutoka kwake basi huyo ni swahabah ambaye anafikia ngazi hii kuu na anaingia ndani ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia vitanga viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[1]

Wote  – Allaah akitaka – wana ngazi hii kuu. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… ni swahabah wake.”

Hata kama alimuona tu na akamuamini basi ni swahabah. Mtu kama huyo hakuna budi ni swahabah na usuhuba wake ni kwa mujibu wa kiasi alivyotangamana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy walikuwa ni Muhaajiruun walioshi naye Makkah na al-Madiynah. Walipambana, wakajitolea na mengineyo. Wao ni bora kuliko wengine. Hivyo ndivyo hali ilivyoendelea mpaka yule  wa mwisho wao aliyeingia katika Uislamu baada ya kufunguliwa mji wa Makkah. Hata kama mtu alimuona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) saa au muda mchache anaingia katika Maswahabah na anapata utukufu wa matangamano haya.

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 412-413
  • Imechapishwa: 11/10/2017