10- Mwenye kuhitajia kutofunga kwa sababu ya kuzuia dharurah kama mfano wa kumwokoa mtu ambaye amelindwa kuuliwa kwa mujibu wa Shari´ah kwa sababu ya kuzama, kuchomeka moto, kujigonga na mfano wa hayo. Akiwa hawezi kumwokoa isipokuwa mpaka ajitie nguvu kwa sababu yake kwa yeye kula na kunywa basi inafaa kwake kufanya hivo. Bali katika hali hiyo italazimika kwake kula. Kwa sababu ni lazima kumwokoa na kifo ambaye amelindwa kuuliwa. Jambo ambalo lililo la wajibu halitimii isipokuwa mpaka mtu alifanye basi nalo litakuwa ni wajibu kufanywa. Baadaye atalazimika kulipa siku aliyokula.

Mfano wa hilo ni yule mwenye kuhitajia kula kwa sababu ya kujitia nguvu kwa ajili ya kupambana katika njia ya Allaah ili kuwapiga vita maadui. Katika hali hiyo atakula na atalipa zile siku alizokula. Ni mamoja hayo yametokea safarini au katika mji wake akiingiliwa na adui. Kwa sababu kufanya hivo kuna kuwatetea waislamu na kuliweka juu ya neno la Allaah (´Azza wa Jall). Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kueleka Makkah na sisi tumefunga. Tukatua kwenye kituo kimoja ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika nyinyi mmemkaribia adui wenu na kufungua kunawatia nguvu zaidi.”

Ikawa ni ruhusa; miongoni mwetu wako waliofunga na wengine wakafungua. Kisha tukatua kwenye kituo kingine ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nyinyi kesho mtakutana na adui. Kula ndio kunakutieni nguvu zaidi; hivyo basi kuleni.”

Hayo yakawa ni maazimio na hivyo tukafungua.”

Katika Hadiyth hii kuna ishara inayoashiria kwamba nguvu juu ya kupambana ni sababu yenye kujitegemea pasi na safari. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya sababu ya jambo la kufungua ni nguvu juu ya kupambana na adui pasi na safari. Kwa ajili hiyo hakuwaamrisha kufungua katika kile kituo cha mara ya kwanza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 09/05/2020