42. Baadhi ya hukumu zinazomuhumu mwanamke katika Hajj na ´Umrah III

5 – Anayofanya mwanamke kabla ya Ihraam. Anatakiwa kufanya kama anavofanya mwanaume kwa njia ya kuoga, kujisafisha, kukata yale anayohitajia kukata kama vile nywele, kucha, kuondosha harufu mbaya asije kuhitajia mambo hayo katika hali ya Ihraam ilihali amekatazwa nayo. Asipohitajia kitu katika hayo basi sio lazima na sio katika hukumu maalum za Ihraam. Hakuna neno akajitia manukato mwilini mwake kwa vitu visvyokuwa na harufu nzuri katika manukato. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah:

“Tulikuwa tukitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tunafunga paji zetu za uso kwa miski wakati wa Ihraam. Mmoja wetu anapotokwa na jasho basi hutirika juu ya uso wake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anayaona na wala hatukatazi.”

Ameipokea Abu Daawuud.

ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Kunyamza kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunafahamisha juu ya kujuzu. Kwa sababu hanyamazii batili.”

6- Wakati mwanamke anahirimia atavua Burqu´ na Niqaab – ikiwa amevaa viwili hivyo – kabla ya kuhirimia. Viwili hivyo ni vifuniko vya uso na vina tundu mbili kwa ajili ya macho ambapo mwanamke huangalia kwenye tundu hizo mbili. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwanamke mwenye kuhirimia asivae Niqaab.”

Ameipkea al-Bukhaariy.

Burqu´ ni nzito zaidi kuliko Niqaab. Mwanamke pia atavua vilivyo katika viganja vyake viwili katika soksi za mikono ikiwa amezivaa kabla ya Ihraam. Soksi hizo ni kitu kinachowekwa katika mikono huingizwa kwenye mikono na kuisitiri. Kisha atafunika uso wake kwa isiyokuwa Niqaab wala Burqu´ kwa kuweka Khimaar au nguo wakati atapoona wanaume ambao sio Mahram zake. Vivyo hivyo atafunika mikono yake wasimuone kwa zisizokuwa soki za mikono kwa mfano kwa kuifunika na nguo. Kwa sababu uso na mikono ni uchi ambao ni lazima kuvifunika mbele ya wanaume katika hali ya Ihraam na kwenginepo. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusu mwanamke yeye wote ni uchi. Kwa ajili hii ndio maana imefaa kuvaa nguo zenye kumsitiri na ajifunike kwa Mahmal. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemkataza kuvaa Niqaab na kuvaa vifuniko vya mikono. Vifuniko vya mikono ni kama soksi zinazowekwa kwenye mikono. Lau mwanamke atafunika uso wake kwa kitu kisichogusa uso ni jambo linalofaa kwa maafikiano. Na ikiwa kinamgusa maoni yenye nguvu ni kwamba inafaa. Mwanamke hakalifishwi kuweka mbali sitara yake na uso; si kwa mti wala mkono. Kwani hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya sawa kati ya uso wake na mkono wake na viwili hivyo ni kama mwili wa mwanaume na si kama kichwa chake. Wake zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakiteremsha nguo juu ya nyuso zao bila kuzingatia kuweka mbali nguo zao na hizo nyuso. Hakuna mwanachuoni yeyote aliyenukuu kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Ihraam ya mwanamke katika uso wake. Hayakuwa hayo isipokuwa ni maoni ya baadhi ya Salaf.”

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema “Tahdhiyb-us-Sunan”[1]:

“Haikutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) herufi hata moja inayosema kwamba ni lazima kwa mwanamke kuacha wazi uso wake wakati wa Ihraam; isipokuwa tu makatazo ya Niqaab.” Mpaka aliposema: “Imethibiti kutoka kwa Asmaa´ kwamba alikuwa akifunika uso wake ilihali ni mwenye kuhirimia. ´Aaishah amesema: “Wapanda farasi wanaume walikuwa wakitupitia na sisi tuko kwenye Ihraam pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanapotujongelea, kila mmoja wetu anateremsha mavazi yake ya juu, Jilbaab, usoni mwake. Wanapokuwa wameshapita, tunajifunua tena.”

Ameipokea Abu Daawuud.

Hivyo basi, ee dada wa Kiislamu, tambua kwamba umekatazwa kufunika uso na mikono kwa kitu cha kufunika na khaswakhaswa Niqaab na Burqu´. Ni wajibu kufunika uso na mikono yako mbele ya wanaume wasiokuwa Mahram zako kwa Khimaar, nguo na wavyo na kwamba hakuna msingi wa kuweka kitu kitakachozuia kile kifuniko na kugusa uso; si kwa kuweka mti, kilemba wala vyenginevyo.

[1] (02/350).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 86-88
  • Imechapishwa: 12/11/2019