Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ عَلِمُواْ لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الآخِرَةِ مِنْ خَلاَقٍ

 “Kwa hakika wamekwishaelewa kwamba atakayenunua [kwa kujipatia elimu ya uchawi huo] hatopata katika Aakhirah fungu lolote.” (al-Baqarah 02:102)

2-

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ

”Je, huzingatii wale ambao wamepewa sehemu ya Kitabu [hapo kale] wanaamini mazimwi na Twaaghuut?” (an-Nisaa´ 04:51)

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Jibt ni uchawi na Twaaghuut ni shaytwaan.”[1]

2- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Twaaghuut ni makuhani walikuwa wakiteremkiwa na mashaytwaan. Katika kila kabila kuna mmoja.”

3- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na dhambi saba zenye kuangamiza.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni yepi hayo?” Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, uchawi, kuiua nafsi ambayo Allaah kaiharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya mayatima, kukimbia siku ya vita na kuwazulia uongo wa kuzini wanawake waumini waliohifadhika.”[2]

4- Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Adhabu ya mchawi ni kuuawa kwa upanga.”[3]

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Sahihi ni kwamba ni maneno ya Swahabah.”

5- al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Bajaalah bin ´Abadah aliyesimulia:

“´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliandika barua ambapo ndani yake kulikuwemo:

“Muueni kila mchawi mwanaume na mchawi mwanamke.”

Tukawaua wachawi watatu.”

6- Imesihi kutoka kwa Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba yeye aliamrisha auawe kijakazi wake ambaye alikuwa kamfanyia uchawi ambapo akauawa[4]. Vivyo hivyo kitendo hicho kimesihi kutoka kwa Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) pia[5].

Ahmad amesema:

“Imesihi kupokelewa kutoka kwa Maswahabah watatu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Uchawi ni mambo yanayofanywa na mchawi ambapo anafunga vifundo, madawa na kupulizia katika vifundo hivyo na mambo mengine ambayo wanayapokea kutoka kwa majini na mashaytwaan. Uchawi ni yale yanayowaroga watu. Uchawi umeitwa kuwa ni uchawi kwa sababu unafanywa kwa njia ya kujificha.

Uchawi ni uovu na shirki. Kwa sababu mtu hawezi kufikia uchawi isipokuwa kwa kupata msaada kutoka kwa mashaytwaan na mtu huyo akajikurubisha kwao na akawaabudu badala ya Allaah:

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme [kumwambia mtu huyo]: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.” (al-Baqarah 02:102)

Ni dalili inayothibitisha kwamba kujifunza uchawi ni kufuru. Kisha akasema (Ta´ala):

1-

وَلَقَدْ عَلِمُواْ لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الآخِرَةِ مِنْ خَلاَقٍ

 “Kwa hakika wamekwishaelewa kwamba atakayenunua [kwa kujipatia elimu ya uchawi huo] hatopata katika Aakhirah fungu lolote.”

Kuununua maana yake kuufanya. Mtu kama huyo hana fungu lolote mbele ya Allaah. Hii ni dalili inayoonyesha kwamba uchawi ni uovu na ni haramu:

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme [kumwambia mtu huyo]: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.” (al-Baqarah 02:102)

 Ni dalili inayofahamisha kwamba uchawi ni kinyume na imani na kumcha Allaah. Kwa ajili hiyo wamesema wanachuoni kwamba uchawi ni kufuru na upotevu kwa sababu hakuna njia ya mtu kufikia uchawi isipokuwa mpaka awaabudu majini na mashaytwaan. Imesemekana vilevile kwamba inatakiwa kupambanua; uchawi wenye maana ya kuwaabudu majini na mashaytwaan ni kumkufuru na kumshirikisha Allaah, na uchawi wenye maana ya madawa ambayo hayana mahusiano yoyote na mashaytwaan na kuwaabudu – basi ni haramu, dhambi na uovu mkubwa na vilevile ni kuwadhulumu na kuwashambulia viumbe. Kwa sababu watu wenye kufanya mambo hayo wanaharibu  na kuzibadilisha akili za watu.

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ

”Je, huzingatii wale ambao wamepewa sehemu ya Kitabu [hapo kale] wanaamini mazimwi na Twaaghuut?”

Aayah hii imeteremka kuhusu mayahudi. Allaah amekhabarisha kwamba wanaamini mazimwi na shaytwaan. Wajuzi wa lugha wamesema kuwa Jibt ni kitu kisichokuwa na kheri ndani yake kama mfano wa uchawi, sanamu na mfano wake. Twaaghuut ni kila chenye kuvukiwa mipaka. Msemo huo unatumiwa kwa mashaytwaan katika majini na watu kwa sababu wamevuka mipaka kwa kufuru na upotevu wao.

2- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Twaaghuut ni makuhani walikuwa wakiteremkiwa na mashaytwaan. Katika kila kabila kuna mmoja.”

Hii ina maana kwamba kuhani ni katika Twaaghuut. Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kufuatwa na kutiiwa ambacho mja anachupa kwacho mipaka.”

Bi maana anayefuatwa katika batili na kutiiwa katika isiyokuwa Shari´ah ya Allaah. Viongozi wake ni watano:

1- Ibliys.

2- Mtu anayewaita wengine wamwabudu, kama vile Fir´wan.

3- Anayeabudiwa na wakati huohuo akaridhia hilo.

4- Anayedai kujua mambo yaliyofichikana.

5- Anayehukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kwa kukusudia.

Wachawi na makuhani wanaingia katika sampuli hizo kwa sababu wameiacha njia iliyonyooka na kuwakera watu kwa matendo yao.

3- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na dhambi saba zenye kuangamiza.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni yepi hayo?” Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, uchawi, kuiua nafsi ambayo Allaah kaiharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya mayatima, kukimbia siku ya vita na kuwazulia uongo wa kuzini wanawake waumini waghafilikaji na waliohifadhika.”

Kubwa katika hayo ni shirki. Kisha kunafuata uchawi kwa sababu mara nyingi unatokamana na shirki. Kwani uchawi una maana ya kuwaabudu majini na kuwaomba msaada na kujikurubisha kwao. Baada ya hapo kunafuatia kuiua nafsi ambayo imeharamishwa na Allaah isipokuwa kwa haki, riba, kukimbia siku ya vita ambapo yamekutana makundi mawili katika safu ana kwa ana ambapo mtu akalikimbia kundi lake na kuwatuhumu machafu wanawake waumini wenye kujihifadhi. Tuhuma hapa inahusiana na uchafu wa uzinzi.

Wameitwa waghafilikaji kwa sababu mara nyingi huwa hawatambui waliowatuhumu. Hukumu hiyohiyo inahusiana na wanaume wenye kujihifadhi. Hii ni dhambi kubwa. Mtuhumu anastahiki kusimamishiwa adhabu. Lakini hili mara nyingi linakuwa kwa wanawake. Ndio maana yule mwenye kuwatuhumu anatakiwa kuadhibiwa.

Haijuzu kwenda kwa wachawi kwa ajili ya matibabu hata kama itahusiana na kujitibu. Haijalishi kitu hata kama mtu hayuko radhi na uchawi. Kwa sababu mtu akienda kwa wachawi anaita na kushaji´isha katika shirki na katika yale aliyoharamisha Allaah. Yule mwenye kufanyiwa uchawi ajitibu kwa madawa yenye kuafikiana na Shari´ah. Haya ndio maoni  sahihi ya wanachuoni.

4- Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Adhabu ya mchawi ni kuuawa kwa upanga.”

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Sahihi ni kwamba ni maneno ya Swahabah.”

Alisema hivo wakati kulikuwepo mchawi katika kikao cha al-Waliyd bin Yaziyd. Mchawi huyu alikuwa eti anakikata kichwa chake kisha anakirudisha. al-Waliyd akamwendea pasi na yule mchawi kujua kitu na akampiga upanga. Halafu akasema: “Kama ni mkweli basi akirudishe kichwa chake hivi sasa.” Hapo ndipo Jundub akasema hivo. Ni maneno yake aliyoyafikia kutoka katika dalili za Shari´ah. Malengo yake ni kwamba mchawi anatakiwa kuuawa pasi na kumtaka atubie. Kutubia kwake hakuzuii kuuawa. Huenda akawa ni mwenye kudanganya na akadhihirisha kuwa ametubia na madhara yake yakabaki kwa watu. Yule ambaye itathibiti kama kweli ni mchawi basi ni wajibu kumuua ili asije kuwadhuru watu.

5- al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Bajaalah bin ´Abadah aliyesimulia:

“´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliandika barua ambapo ndani yake kulikuwemo:

“Muueni kila mchawi mwanaume na mchawi mwanamke.”

Tukawaua wachawi watatu.”

Aliwaandikia wakubwa wa majeshi Shaam. Wanatakiwa kuuawa kutokana na yale madhara ambayo hayawezi kutokomea isipokuwa kwa kuuawa. Wao ni waongo, kama wanafiki, wanaweza kujionyesha kwa uinje tu kuwa wametubia. Mchawi anauawa kwa ukafiri na tawbah yake haikubaliwi. Haya ndio maoni sahihi.

6- Imesihi kutoka kwa Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba yeye aliamrisha auawe kijakazi wake ambaye alikuwa kamfanyia uchawi ambapo akauawa.” Vivyo hivyo kitendo hicho kimesihi kutoka kwa Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) pia.

Ahmad amesema:

“Imesihi kupokelewa kutoka kwa Maswahabah watatu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Bi maana imesihi kupokelewa kutoka kwa Maswahabah watatu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nao ni ´Umar, Jundub na Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhum). Haya ndio maoni ya sawa.

Faida

Baadhi ya wanachuoni akiwemo ash-Shaafi´iy wamesema ikiwa uchawi wa mchawi unatokamana na mambo yanayotambulika yanayoudhi/yanayokera na yanasababisha maradhi pasi na kuzigeuza akili na pasi na ndani yake kuna kudai kujua mambo yaliyofichikana na pasi na kuwatumia na kuwataka msaada mashaytwaan na kutumia vyengine alivyoharamisha Allaah, basi asiuawe. Hoja yao ni kwamba haya sio uchawi, bali ni maudhi tu na dhuluma. Mtu huyu anatakiwa kupigwa na kutiwa adabu. Maswahabah walichokuwa wanalenga kuhusu kuuawa kwa wachawi ni wale wanaowatumia majini na kuwaabudu na kudai kwamba wanajua mambo yaliyofichikana. Hali kama hii ndio hutokea mara nyingi kwa wachawi. Hawa wanatakiwa kuuawa. Haya ndio maoni ya sawa.

Imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanyiwa uchawi. Lakini hata hivyo ni jambo halikuathiri kitu katika mambo ya ujumbe. Yaligusa tu katika mambo yanayohusiana kati yake yeye na familia yake, kama alivyopokea al-Bukhaariy na Muslim[6].

[1] al-Bukhaariy (8/252).

[2] al-Bukhaariy (2767) na Muslim (89).

[3] at-Tirmidhiy (1460), al-Haakim (8073), ad-Daaraqutwniy (112) na wengineo. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Jaami´-us-Swaghiyr” (2699).

[4] Maalik (1526) na wengineo.

[5] ad-Daaraqutwniy (113) na al-Bayhaqiy (16278).

[6] al-Bukhaariy (5763) na Muslim (2189).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 86-89
  • Imechapishwa: 12/10/2018