Shirki maana yake ni kumfanyia Allaah mshirika katika uola na uungu Wake. Mara nyingi kunashirikishwa katika ´ibaadah kwa njia ya kwamba mtu anamuomba Allaah pamoja na wengine au akamfanyia kitu katika aina za ´ibaadah kama mfano wa kichinjwa, kuweka nadhiri, kuogopa, kutaraji na kupenda. Shirki ndio dhambi kubwa mno kwa sababu zifuatazo:

a) Kwa sababu ni kuwafananisha viumbe na Muumba katika mambo ambayo ni maalum kuabudiwa Yeye. Mwenye kushirikisha pamoja na Allaah mwengine yeyote, basi amemshirikisha. Hii ndio dhuluma kubwa kabisa. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[1]

Dhuluma ni kule kukiweka kitu pasipo mahala pake stahiki. Mwenye kumwabudu asiyekuwa Allaah basi ameiweka ´ibaadah pasipo mahala pake stahiki na amemtekelezea nayo asiyeistahiki, mambo ambayo ni dhuluma kubwa mno.

b) Allaah ameeleza kwamba hamsamehi yule asiyetubia kwayo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[2]

c) Allaah ameeleza kuwa ameharamisha Pepo kwa mshirikina na kwamba ni mwenye kudumishwa Motoni milele. Amesema (Ta´ala):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.”[3]

d) Shirki inaporomosha matendo yote. Amesema (Ta´ala):

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha, basi pasi na shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.”[4]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[5]

e) Damu na mali ya mshirikina ni halali. Amesema (Ta´ala):

فَإِذَا انسَلَخَ الْأَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُوا لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ

“Itapomalizika miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote muwakutapo, wafanyeni mateka na wahusuruni na wakalieni katika kila sehemu ya uvamizi. Lakini wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi waacheni huru.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka waseme ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`. Wakiyasema basi imelindwa kwangu damu na mali yao isipokuwa kwa haki yake.”[7]

f) Shirki ndio dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nisikwambieni dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, kuwaasi wazazi wawili… “[8]

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ameeleza (Subhaanah) kwamba malengo ya kuumba na kuleta amri ni ili atambulike kwa majina na sifa Zake, aabudiwe peke yake bila kushirikishwa na watu wasimame kwa uadilifu ambao ndio zimesimama mbingu na ardhi. Amesema (Ta´ala):

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

“Hakika Tuliwapeleka Mitume wetu kwa hoja za waziwazi na tukateremsha pamoja nao Kitabu na Shari´ah ili watu wasimamie kwa uadilifu.”[9]

Akaeleza (Subhaanah) kwamba amewatumiliza Mitume Wake na akateremsha vitabu Vyake ili watu wasimamishe kwa uadilifu. Miongoni mwa uadilifu mkubwa kabisa ni Tawhiyd, ndio kilele cha uadilifu na kiongozi wake na kwamba shirki ni dhuluma. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[10]

Shirki ndio dhuluma kubwa kabisa na Tawhiyd ndio uadilifu mkubwa kabisa. Kupinga malengo haya makubwa ndio ukafiri mkubwa mno.” Mpaka aliposema: “Ilipokuwa shirki ni yenye kukanusha kwa dhati yake malengo haya ikawa ndio dhambi kubwa kabisa, Allaah akaiharamisha Pepo juu ya kila mshirikina, akahalalisha damu, mali yake na mke wake kwa watu wa Tawhiyd na wawafanye kuwa watumwa wao pindi walipoacha kusimama na jambo la kumwabudu. Allaah (Subhaanah) amekataa kukubali matendo kutoka kwa mshirikina, kukubali kwake uombezi au kukubali du´aa juu yake huko Aakhirah. Mshirikina ndio mjinga mkubwa kabisa juu ya Allaah kwa vile amemjaalia Allaah mwenza, jambo ambalo ni kumjahili kwa hali ya juu kama ambavyo ni dhuluma ilio kubwa kabisa kutoka kwa mtendaji huyo. Ingawa uhakika wa mambo ni kwamba mshirikina hakumdhulumu Mola Wake bali ameidhulumu nafsi yake mwenyewe.”[11]

g) Shirki ni upungufu na ni kasoro na Mola (Subhaanah) amejitakasa nafsi Yake kutokamana na viwili hivyo. Yule mwenye kumshirikisha Allaah basi amemthibitishia Allaah yale aliyojitakasa nafsi nayo. Huu ndio upeo wa juu kabisa wa kumpinga, ukaidi na kukinzana na Allaah (Ta´ala).

[1] 31:13

[2] 04:48

[3] 05:72

[4] 06:88

[5] 39:65

[6] 09:05

[7] al-Bukhaariy (01/102) na Muslim (01/150).

[8] al-Bukhaariy (5976) na Muslim (87).

[9] 57:2

[10] 31:13

[11] Jawaab-ul-Kaafiy, uk. 109.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 80-82
  • Imechapishwa: 11/03/2020