1 – Ni wajibu kwa yule mwenye akili kujiepusha na kuombaomba katika hali zote. Ile fikira peke yake ya kuazimia kuomba inamdhalilisha mtu na inamshusha hadhi yake. Kuacha kufikiria kuomba inampa mtu utukufu na inampandisha cheo.

2 – Muusa bin Twariyf amesema:

”Pindi ninapomuhitajia mtu basi huondoka utukufu kutoka moyoni mwangu. Ninapokata haja hiyo basi utukufu hurudi moyoni mwangu.”

3 – ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

”Yule mwenye kuwaomba watu ili ajikithirishie mali yake basi si vengine ni jiwe la moto linaloweka ambalo atalishwa nalo mdomoni mwake. Hivyo basi anayetaka, basi afanye hivo kwa uchache, na anayetaka, basi afanye hivo kwa wingi.”

4 – Hakiym bin Qays bin ´Aaswim amesimulia kwamba baba yake aliwausia wanawe wakati alipokuwa anataka kukata roho:

“Enyi wanangu wapenzi! Nakutahadharisheni na kuwaombaomba watu! Kuomba ndio chumo la mwisho la mtu.”

5 – Mwenye busara asiwaombe watu kitu wakamrudisha na asiwang´ang´anie juu ya kitu wakamnyima. Anatakiwa kujizuia na kujiheshimu. Asiombe kitu hali ya kukipa mgongo na wala asikiache hali ya kukielekezea uso. Kwani ni bora kukikosa kitu kuliko kukiomba kwa watu wasiostakiki. Yule anayeomba kitu kutoka kwa mtu asiyekuwa mstahiki ameiteremsha nafsi yake ngazi mbili na amempandisha yule aliyemuomba.

6 – Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

“Anayemuomba kitu mtu duni basi amempandisha cheo.”

7 – Mutwarrif bin ´Abdillaah bin ash-Shikhkhiyr alisema kumwambia mpwa wake:

“Ee mwanangu kipenzi! Ukihitajia kitu kutoka kwangu basi kiandike kwenye karatasi. Naulinda uso wako kutokamana na udhalilifu wa kuomba.”

8 – Janga lililo kubwa kabisa ni mrithi mbaya. Kuwaomba watu na kule kufikiria kuwaombaomba ni udhaifu wa uzee. Mtu asemeje kuhusu kule kuwaomba kikweli? Yule ambaye ameitukuza nafsi yake basi dunia itakuwa dhalili mbele ya macho yake. Mtu hawi mtukufu mpaka pale atakapovipa nyongo vilivyoko mikononi mwa watu na akayapuuzilia yale wanayoyafanya. Kuwaomba jamaa kunawachosha na kuwoamba wengine hakuzalishi matunda.

9 – Ibn Mas´uud amesema:

“Kuomba kitu kutoka kwa ndugu yako ni mtihani. Akimpa, basi anamsifu mwengine kuliko Yule ambaye kikweli ndiye kampa. Akimnyima, basi anamsema vibaya kuliko Yule ambaye kikweli ndiye kamnyima.”

10 – Lau katika kuomba kusingekuwa na sifa nyingine inayosimangwa zaidi ya mtu kuidhalilisha nafsi yake pale anapoomba na kudhihirisha ombi lake basi ingelikuwa inatosha kuwa ni wajibu kwa yule mwenye busara kama ametenzwa nguvu basi ameze changarawe na anyonye mbegu badala ya kuomba muda wa kuwa anaweza kujitosheleza. Hata hivyo kama atatenzwa nguvu na akamuomba mtu ambaye anajua kuwa anaweza kumsaidia au mtawala, basi hapana neno. Ni kama mfano wa kupokea unapopewa bila kuomba. Yule atakayetosheka na Allaah basi Allaah atamfanya kuwa tajiri. Yule atakayejitukuza kwa Allaah basi hatomfanya fakiri. Kama ambavo hudhalilika ambaye anatafuta utukufu kutoka kwa waja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 144-148
  • Imechapishwa: 09/08/2021