41. Maovu ya kwanza: Kutundika picha


1- Kutundika picha

Jambo la kwanza: Kutundika picha ukutani, sawa ziwe zenye kiwiliwili cha mwanaadamu au zisizokuwa na kiwiliwili cha mwanaadamu, zenye kivuli au zisiwe na kivuli, zilizochorwa kwa mkono au zilizotengenezwa kutumia vifaa vya kisasa, yote hayo hayajuzu na ni wajibu kwa yule mwenye kuweza kuyaondosha na asipoweza kuyaondosha basi kuiharibu. Kumepokelewa juu ya hilo Hadiyth zifuatazo:

1- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia akisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwangu na mimi nilikuwa nimefungua pazia la chumba cha hazina ambalo lilikuwa na picha.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… ambalo lilikuwa na picha zilizo na farasi wenye mbawa. Aliponiona, basi aliliachana na uso wake ukapiga wekundu na kusema: “Ee ´Aaishah! Hakika watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale  wanaoigiza maumbile ya Allaah.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Hakika watu wa picha hizi wataadhibiwa na wataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba.” Kisha akasema: “Hakika nyumba ilio na picha hawaingii Malaika.” ´Aaishah anaendelea kusimulia: “Basi tukalikata na kulifanya mto au mito miwili. Nilimuona akigemea mto mmoja wapo ilihali ulikuwa na picha.”[1]

2- ´Aaishah amesimulia tena akisema: “Niliujaza mto pamba kwa ajili ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ulikuwa na picha. Akasimama kati ya milango miwili na uso wake ukabadilika. Nikasema: “Tuna nini, ee Mtume wa Allaah? Natubu kwa Allaah kwa niliyotenda dhambi.” Akasema: “Vipi kuhusu mto huu?” Nikasema: “Ni mto nimeutengeneza ili uweze kuegemea.” Akasema: “Hukujua ya kwamba Malaika hawaingii katika nyumba ilio na picha na kwamba atakayetengeneza picha basi ataadhibiwa siku ya Qiyaamah na ataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba?”

Katika upokezi mwingine imekujaa:

“Hakika wale wanaotengeneza picha hizi wataadhibiwa siku ya Qiyaamah.”

´Aaishah anaendelea kusimulia:

“Basi hakuingia mpaka nilipoiondosha.”[2]

3- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jibriyl alinijia jana na akanambia: “Nilikuja jana na hakuna kitu kilichonizuia isipokuwa mlangoni kulikuwa picha/kinyago na kwenye nyumba kulikuwa na pazia ilio na picha na kwenye nyumba kulikuwa na mbwa. Kwa hivyo nenda kwenye kichwa cha ile picha/kinyago ukikate na kiwe kama muonekano wa mti na nenda kwenye ile pazia auikatekate na auifanye mito miwili na mwendee mbwa umuondoshe nje. Kwani hakika sisi hatungii kwenye nyumba ilio na picha wala mbwa. Mbwa alikuwa wa Hasan na Husayn ambaye alijificha chini ya sehemu ya kutundikia nguo zao.” Katika upokezi mwingine imekuja: “… chini ya kitanda chake.” Akasema: “Ee ´Aaishah! Mbwa huu aliingia wakati gani?” Akasema: “Ninaapa kwa Allaah sijui.” Halafu akaamrisha atolewe nje kisha akachukua maji mikononi mwake na kurashia mahali alikuweko.”[3]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (01/317-318), Muslim (06/158-160) na siyaaq ni yake, al-Bayhaqiy (07/269), al-Baghawiy katika “Sharh-us-Sunnah (01/217/03) na wengineo. Katika Hadiyth hii kuna faida mbili:

Ya kwanza: Uharamu wa kutundika picha au kitu kilicho na picha.

Ya pili: Uharamu wa kuzipiga. Ni mamoja ziwe zenye kiwiliwili cha mwanaadamu au zisizokuwa na kiwiliwili cha mwanaadamu, au kwa msemo mwingine ziwe ni zenye kivuli au zisizokuwa na kivuli. Haya ndio madhehebu ya wanachuoni wengi. an-Nawawiy amesema:

“Baadhi ya Salaf wameonelea kuwa zilizokatazwa ni zile zenye kivuli. Ama zile zisizokuwa na kivuli wanaonelea moja kwa moja kuwa hazina neno kuzichukua. Haya ni maoni batili. Hakika pazia ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza ilikuwa ni ya picha isiyokuwa na kivuli. Pamoja na hivyo akaamrisha iondoshwe.”

Kuna baadhi ya watu hii leo wamenijibu juu ya vitabu vyangu kuhusu Hadiyth ya ´Aaishah kwa kusema:

“Picha hii inaenda kinyume na uhalisia wa mambo na inaeleza uongo. Kwa kuwa hakuna farasi aliye na mbawa. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mchoro huu ulimchukiza.”

Jawabu hili ni batili kwa njia mbalimbali:

Ya kwanza: Katika Hadiyth hakuna ishara hata ndogo inayoashiria sababu ya kukemea ni kuwa mchoro huu unaenda kinyume na uhalisia wa mambo. Bali kinyume chake imewekwa wazi ya kwamba sababu siyo hiyo. Nayo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Hakika nyumba ilio na picha hawaingii Malaika.”

Amesema picha moja kwa moja na wala hakuiwekea masharti kwa kusema ni ya aina fulani. Kwa ajili hiyo ndio maana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaondosha pazia ile na akaamrisha itolewe kwa sababu inazuia Malaika kuingia nyumbani. Hili ni jambo liko wazi sana.

Ya pili: Ikiwa sababu ya kuyakemea ni picha hiyo kwenda kinyume na uhalisia wa mambo – kama alivyosema mwandishi anayeashiriwa – basi ni kwa nini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkubalia ´Aaishah kumchukua farasi wake wa mbawa katika kisa kingine kama itavyokuja katika Hadiyth ya tano katika kwenye ya 40? Kwa hivyo maneno ya mwandishi huu yanapata kuanguka. Hadiyth iko wazi kabisa na haina kipingamizi…

Kitu kingine kinachopata kufahamika kutokana na yale tuliyotaja ni kwamba haijuzu kwa muislamu anayetambua hukumu ya picha kununua nguo ilio na picha – ijapokuwa ni kwa kutaka kuitweza – kwa sababu kufanya hivo ni kushirikiana katika maovu. Yule atakayenunua na huku hajui kuwa haifai, basi itafaa kwake kuitumia kwa kuitweza. Hivyo ndivyo inavyofahamisha Hadiyth ya ´Aiashah.

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (02/11) na (04/105), Abu Bakr ash-Shaafi´iy katika “al-Fawaaid” (06/68) na ziada ni yake na mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh. Hadiyth imepokelewa na Mashaykh wawili na wengineo mfano wa hiyo. Imepokelewa vilevile katika kitabu “al-Halaal wal-Haraam” cha profesa Yuusuf al-Qaradhwaawiy (121). Imekwishatangulia katika kitabu hiki, uk. 161-162.

Kuna dalili ya wazi inayoonyesha ya kwamba picha zilizokaa waziwazi zinazuia Malaika kuingia nyumbani hata kama zitakuwa ni zenye kutwezwa. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataa kuingia mpaka ilipoondoshwa na akasema juu ya hilo:

“Malaika hawaingii katika nyumba ilio na picha.”

[3] Hadiyth ni Swahiyh. Ni mkusanyiko wa mapokezi tano kutoka kwa Maswahabah Abu Hurayrah na siyaaq ni yake. Ameipokea Abu Daawuud (02/189), an-Nasaa´iy (02/302), at-Tirmidhiy (04/21). Ibn Hibbaan ameisahihisha (1487), Ahmad (02/305-308) na (478) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 185-197
  • Imechapishwa: 19/04/2018