Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba imani inazidi na kupungua. Haya yanathibishwa na Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Qur-aan:

لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ

“Ili Awazidishie imani pamoja na imani zao.”[1]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu wanawake:

“Sijaona walio na akili punguani na dini pungufu wanaomghalibu mtu mwenye busara kama nyinyi wanawake.”[2]

Aayah inathibitisha kuzidi kwa imani na Hadiyth inathibitisha kuwa inapungua.

Kila dalili yenye kujulisha kuwa imani inazidi inafahamisha vilevile kuwa inapungua na kinyume chake. Kuzidi na kupungua ni mambo mawili yenye kulazimiana na yasiyoachana.

Imethibiti kutoka kwa Maswahabah kuwa imani inazidi na kupungua. Hajulikani aliyeonelea kinyume. Wengi katika Salaf wana maoni haya. Ibn ´Abdil-Barr amesema:

“Imani kuzidi na kupungua ni maoni walio nayo wanachuoni wa Hadiyth, Fiqh na wa Fataawaa ulimwenguni. Kumesimuliwa mapokezi mawili kutoka kwa Maalik juu ya kushuka. Moja wapo amekomeka na nyengine ameafikiana na wengine.”

Makundi mawili yameenda kinyume na kanuni hii:

1- Murji-ah. Wanaosema kuwa imani ni kukubali kwa moyo. Wanadai kuwa kukubali kwa moyo hakutofautiani. Wanaona kuwa mtenda dhambi na mwema wote ni wanalingana katika imani zao.

2- Wa´iydiyyah katika Mu´tazilah na Khawaarij. Hawa wanawatoa watenda madhambi makubwa nje ya imani. Hawa wanaona kuwa imani ima ipatikane yote au ipotee yote. Hawaoni kuwa inatofautiana.

Makundi yote mawili yanaanguka kwa dalili za Shari´ah na za akili. Kuhusu Shari´ah tayari zimekwishatangulia dalili. Kuhusu za akili, tunasema kuwaambia Murji-ah kwamba ´Aqiydah yao inaraddiwa kwa njia mbili:

1-  Kusema kuwa imani ni kukubali kwa moyo kunapingana na yanayofahamishwa na Qur-aan na Sunnah kwamba maneno na vitendo vyote viwili vinaingia katika imani.

2- Kusema kwamba imani haitofautiani kunapingana na hisia. Kila mmoja anajua kuwa kukubali kwa moyo kunatokana na elimu. Elimu inatofautiana kwa kutegemea na jinsi inavyochumwa. Yaliyopokelewa na mpokezi mmoja hayana uzito mkubwa kama yaliyopokelewa na wapokezi wawili na kadhalika. Maelezo ambayo mtu anapewa kwa kuelezwa hayana uzito sawa na yale ambayo anayapata kwa kushuhudia mwenyewe. Kwa hivyo yakini inatofautiana daraja, jambo ambalo linajulikana. Uhakika wa mambo ni kuwa mtu wakati fulani huhisi jinsi yakini yake ilivyo na nguvu kabisa kuliko nyakati zengine.

Ni vipi mtu mwenye akili anaweza kuonelea kwamba mtu mwema ambaye anamtii Allaah (Ta´ala), anafanya mambo ya faradhi na yaliyopendekezwa, anajiepusha na yale aliyoharamisha Allaah na pindi anapoteleza kufanya maasi basi hukimbilia kuyaacha na kuleta tawbah yuko sawa katika imani na mtu ambaye anapuuzia yale ambayo Allaah (Ta´ala) amemuwajibishia na kutumbukia katika ya haramu yasiyomtii ndani ya ukafiri? Ni vipi wawili hawa wanaweza kulingana?

Ama Mu´tazilah na Khawaarij tunawaraddi ifuatavyo:

1- Kusema kwamba mtenda dhambi kubwa anatoka nje ya imani ni jambo lenye kupingana na Qur-aan na Sunnah. Ni vipi mtu anaweza kuonelea kuwa watu wawili wako sawa katika imani ambapo mmoja wao anafanya yale ya wajibu na kujiepusha na ya haramu wakati wa pili yuko kinyume kabisa isipokuwa tu hakufuru?

2- Wacha tuseme kuwa mtenda dhambi kubwa anatoka nje ya imani. Ni vipi mtu anaweza kuonelea kuwa watu wawili wako na imani sawa ambapo mmoja wao yupo kati kwa kati na wakati mwingine ametangulia katika mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah?

[1] 48:04

[2] al-Bukhaariy (304) na Muslim (80).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 92-94
  • Imechapishwa: 15/05/2020