41. Kutosuniwa kumuosha maiti aliyekufa katika uwanja wa vita

32- Haikuwekwa katika Shari´ah kumuosha shahidi aliyeuawa katika uwanja wa vita ijapokuwa watu wote wataafikiana kwamba alikuwa na janaba. Kuhusina na hilo zipo Hadiyth zifuatazo:

Ya kwanza: Jaabir ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wazikeni wakiwa na damu zao – yaani siku ya Uhud – na wala hawakuoshwa.” [Katika upokezi mwingine imekuja] Akasema: “Mimi ni shahidi juu ya hawa. Wazungushieni mavazi yao kwa damu zao. Kwani hakika hakuna majeruhi yeyote mwenye kujeruhiwa [kwa ajili ya Allaah] isipokuwa atakuja na donda lake linamwaga damu siku ya Qiyaamah; rangi yake itakuwa ni ya damu na harufu yake itakuwa ni harufu ya miski.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/165) kwa upokezi wa kwanza, Abu Daawuud (02/60), an-Nasaa´iy (01/277-278), at-Tirmidhiy (02/147) ambaye ameifanya kuwa Swahiyh, Ibn Maajah (01/461-462), al-Bayhaqiy (04/10) na upokezi mwingine ni wake na vilevile Ibn Sa´diy katika “at-Twabaqaat” (juzu ya 03, q 01, uk. 07) na ziada ni yake. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Ina – yaani huo upokezi mwingine – una njia nyingine katika “al-Musnad” (03/296) kutoka katika upokezi wa Ibn Jaabir hali ya kurufaishwa kwa tamko lisemalo:

“Msiwaoshe. Kwani hakika kila donda litatoa harufu ya miski siku ya Qiyaamah na hakuwaswalia.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh ikiwa Ibn Jaabir huyu ni ´Abdur-Rahmaan. Ama akiwa ni yule Muhammad, ambaye ni nduguye ´Abdur-Rahmaan, basi ni dhaifu. Sijabainikiwa ni yupi kati ka hao wawili mkusudiwa hapa.

Kuhusu ash-Shawkaaniy yeye amesema katika “Nayl al-Awtwaar” (04/25):

“Hakika ni upokezi ambao haukutiwa dosari.”

Kisha nikaitaja katika “al-Irwaa´” (03/164). Hivyo rejea huko.

Vilevile ina njia ya tatu. Ameipokea Ahmad (05/431-432) kutoka katika upokezi wa ´Abdullaah bin Tha´labah bin Swu´ayr. Alimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini hakukuthibiti kwake kumsikia. Kwa hivyo hiyo ni Mursal ya Swahabah ambayo ni hoja. Cheni ya wapokezi mpaka kwake ni Swahiyh. al-Bayhaqiy (04/11) ameiunganisha kutoka katika Hadiyth yake kutoka kwa Jaabir.

 Ya pili: Abu Barzakhah ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika safari miongoni mwa safari zake za Jihaad ambapo Allaah akamneemesha kwa kumpa mgawira. Akasema kuwaambia Maswahabah zake: “Je, kuna yeyote mnayemkosa?” Wakasema: “Ndio, fulani, fulani na fulani.” Kisha akasema: “Je, kuna yeyote mnayemkosa?” Wakasema: “Hapana.” Akasema: “Lakini mimi simuoni Julaybiyb. Hivyo mtafuteni.” Akatafutwa miongoni mwa wale waliouawa ambapo wakamkuta akiwa pambizoni mwa watu saba aliowauwa kisha nao wakamuua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja ambapo akasimama karibu naye na kusema: “Amewaua watu saba kisha nao wakamuua! Hakika huyu ni kutokana na mimi na mimi ni kutokana na yeye. [Aliyasema mara mbili au mara tatu]. [Kisha akafanya kwa mikono yake namna hii akaikunjua]. Akamuweka mikononi mwake. Hakuna na kitanda isipokuwa mikono miwili ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akachimbiwa shimo na akawekwa ndani ya kaburi lake na wala hakutaja jambo la kuoshwa.”

Ameipokea Muslim (07/152) na mtiririko ni wake, at-Twayaalisiy (924) na ziada ni yake, Ahmad (04/421, 422, 425) na al-Bayhaqiy (04/21).

Ya tatu: Anas ameeleza:

“Mashahidi wa Uhud hawakuoshwa. Walizikwa kwa damu zao. Hakuwaswalia [zaidi ya Hamzah tu].”

Ameipokea Abu Daawuud (02/59) na ziada ni yake na ya al-Haakim – na tamko lake linakuja huko mbele – at-Tirmidhiy (02/138-139) ambaye ameifanya kuwa ni nzuri, Ibn Sa´d (1 q. 3 uk. 08), al-Haakim (01/365), al-Bayhaqiy (04/10-11), Ahmad (03/128). al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim.” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” (05/265) baada ya kuitaja kwa Abu Daawuud peke yake:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri au Swahiyh.”

Mimi naona kuwa ni nzuri ingawa iko juu ya sharti za Muslim.

Ya nne: ´Abdullaah bin az-Zubayr kuhusu kisa cha Uhud na kuuawa kwa Handhwalah bin Abiy ´Aamir ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mwenzenu anaoshwa na Malaika. Muulizeni mke wake.” Mke wake akasema: “Ametoka ilihali ni mwenye janaba pindi aliposikia sauti ya mfazaiko.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Kwa ajili hiyo ndio maana ameoshwa na Malaika.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake, al-Haakim (03/203), al-Bayhaqiy (04/15) kwa cheni ya wapokezi nzuri, kama alivosema an-Nawawiy katika sehemu nyingi katika “al-Majmuu´” (05/260). Halafu akalisahau jambo hilo na akasema baada yake:

“Tumekwishataja kwamba ni Hadiyth dhaifu.”

Ametukuka Ambaye hasahau. al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim.” na adh-Dhahabiy akamkubalia.

Ya tano: Ibn ´Abbaas ameeleza:

“Aliuawa Hamzah bin ´Abdil-Muttwalib na Handhwalah bin ar-Raahib ilihali ni wenye janaba. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nimewaona Malaika wakiwaosha.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (03/1489) kwa cheni ya wapokezi nzuri, kama alivosema “al-Haythamiy” katika “al-Majma´” (03/23). Vilevile ameipokea al-Haakim (03/195), pasi na kumtaja Handhwalah, na akasema:

“Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.” na adh-Dhahabiy akamkosoa, jambo ambalo amepatia. Lakini hata hivyo Hadiyth nyingine yenye kuitolea ushahidi ambayo ni Mursal yenye nguvu. Ameipokea Ibn Sa´d (juzu 03, q. 1, uk. 09) kutoka kwa al-Hasan al-Baswriy ikiwa ni yenye kurufaishwa mfano wake.

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Wapokezi wake wote ni waaminifu. Ndani yake kuna Radd dhidi ya al-Haafidhw ambaye ameisifia Hadiyth ya Ibn ´Abbaas kwamba ni Hadiyth geni kwa sababu ndani yake ametajwa Hamzah ingawa amesema katika cheni ya wapokezi wake: “Haina neno.” Hivo ndivo ash-Shawkaaniy amesimulia kutoka kwake (04/26). Udhahiri wa mambo ni kwamba al-Haafidhw (Rahimahu Allaah) hakuiona Hadiyth hii inayoishuhudilia.

Tambua kwamba njia iliyotumiwa kama dalili juu ya kutosuniwa kumuosha shahidi aliyekufa akiwa na janaba ni yale yaliyotajwa na ah-Shaafi´iyyah na wengineo ya kwamba lau ingelikuwa ni jambo la lazima, basi lisingedondoka kwa kuoshwa na Malaika na isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeamrisha aoshwe. Kwa sababu kilichokusudiwa juu yake ni mwanadamu kuingia ´ibaadani kupitia yeye. Tazama “al-Majmuu´” (05/263) na “Nayl al-Awtwaar” (04/26).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 72-75
  • Imechapishwa: 18/02/2020