41. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya Qadar

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

al-Firqat-un-Naajiyah, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanaamini Qadar kheri na shari yake.

Kuamini Qadar kumegawanyika katika daraja mbili na kila daraja ina mambo mawaili.

Daraja ya kwanza:

Kuamini ya kwamba Allaah (Ta´ala) Alijua kwa Elimu Yake ya milele – ambayo Anasifiwa kwayo milele na daima – ambayo viumbe watafanya, na Akajua hali zao zote kuhusiana na utiifu na maasi, riziki zao na umri wa maisha yao. Kisha Akayaandika Allaah katika Ubao uliohifadhiwa makadirio ya viumbe. Kitu cha kwanza Alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika!” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatayokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.”[1]

Yaliyomfika mtu hayakuwa ni yakumkosa, na yaliyomkosa hayakuwa ni yakumsibu – [wino wa] kalamu umekauka na sahifu zimefungwa. Kama Alivyosema (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Je, huelewi kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni sahali.”(22:70)

Na Akasema (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla Hatujauumba [huo msiba]. Hakika hayo kwa Allaah ni sahali.”(57:22)

Makadirio haya yanafuata Elimu Yake (Subhaanah), yanakuja katika mahali kwa jumla na kwa ufafanuzi. Kaandika kwenye Ubao uliohifadhiwa Atakayo.

Baada ya Kuumba kipomoko, kabla ya kukipulizia roho, Hukitumia Malaika na huamrisha maneno mane. Huambiwa: “Andika riziki yake, umri wa maisha yake, matendo yake na kama atakuwa na maudhiko au mwenye furaha”. Makadirio haya walikuwa wakiyakanusha al-Ghulaat al-Qadariyyah mwanzoni na wanayakanusha (hata) leo japokuwa ni wachache.

Daraja ya pili:

Utashi wa Allaah (Ta´ala) unaoendelea na Uwezo Wake wa kina. Ina maana kuamini ya kwamba Atakayo Allaah, huwa, na Asiyotaka, hayawi. Yenye kufanya harakati na yaliotulia yalioko mbinguni na ardhini hayawi isipokuwa kwa Matakwa ya Allaah (Subhaanah). Hakukuwi katika Ufalme Wake kile Asichokitaka. Na Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Muweza wa kila jambo, sawa yalioko na yasiokuwepo. Hakuna kimechoumbwa katika ardhi wala mbinguni isipokuwa, Allaah (Subhaanah) ndio Kakiumba. Hakuna Muumbaji mwengine badala Yake wala Mola asiyekuwa Yeye. Pamoja na hayo, Kawaamrisha waja kumtii Yeye na kuwatii Mitume Wake na Akakataza Kumuasi. Naye (Subhaanah) Anawapenda wachaji Allaah, wenye kufanya wema na waadilifu. Yuko radhi na wale walioamini na kufanya mema. Hawapendi makafiri na wala Hawaridhii wenye kufanya maasi. Na wala Haamrishi machafu. Haridhii kutoka kwa waja Wake kufuru na wala hapendi ufisadi. Na waja ndio wenye kutenda kihakika na Allaah ndio Ameumba matendo yao.

Muumini na kafiri, mchaji Allaah na mtena dhambi, mwenye kuswali na mwenye kufunga, wote hawa ni waja. Waja wana uwezo na matakwa katika kufanya kwao matendo yao. Allaah Amewaumba na Ameumba vilevile uwezo wao na matakwa yao. Kama Alivyosema (Ta´ala):

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa Atakaye Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:28-29)

Aina hii ya Qadar wanaikanusha al-Qadariyyah wote; ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaita kuwa ni:

“Waabudu moto wa Ummah huu.”[2]

Na upande mwingine, katika wale wanaothibitisha Qadar, wamechupa mipaka kwa hilo, mpaka wakakanusha uwezo wa mja na utashi wake na wakamtoa [mja] katika Matendo ya Allaah na hukumu Yake iliyo juu ya hekima na ustawi Wake.

MAELEZO

Utafiti huu ni miongoni mwa tafiti zenye faida zaidi na zenye kujumuisha. Ni tafiti yenye faida kubwa kuhusiana na Qadar. Mwandishi (Rahimahu Allaah) ameifanyia utafiti na kuiweka wazi kama alivyofanya hivyo pia Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika “Shifaa´ al-´Aliyl fiy Masaa-il al-Qadhwaa´ wal-Qadar wal-Hikmah wat-Ta´liyl”. Mwandishi hapa amebainisha kuhusiana na Qadar ubainifu ambao ni wenye kutosheleza na mzuri kabisa.

al-Firqat-un-Naajiyah, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanaamini Qadar… – Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na sifa za Firqat-un-Naajiyah ni pamoja vilevile na kuamini Qadar kheri na shari yake. Firqat-un-Naajiyah inaamini Qadar kheri na shari yake kwa sura zake zote.

Kuamini Qadar kumegawanyika katika daraja mbili… – Kuna daraja mbili za kuamini Qadar na kila daraja ina mambo mawili. Kuamini Qadar ndani yake kunahitajia mambo mane ambayo yanaitwa “daraja nne”. Mwenye kuyakamilisha basi amekamilisha kuamini Qadar.

Ngazi ya kwanza: Ujuzi. Mtu aamini ya kwamba Allaah aliyajua mambo yote.

Ngazi ya pili: Uandishi.

Ngazi ya tatu: Utashi. Anayotaka Allaah huwa, na asiyotaka hayawi.

Ngazi ya nne: Uumbaji. Mtu aamini ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji wa kila kitu na kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye ameumba kila kitu. Hana mshirika katika kuumba na kuyaendesha mambo. Hizi ndio ngazi za Qadar. Ni ngazi nne. Mtu aamini ujuzi wa Allah juu ya mambo na kwamba ujuzi Wake umeyazunguka mambo yote. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)


لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“… ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake.” (65:12)

Hii ni elimu ya milele. Kwa msemo mwingine hakuacha hata siku moja kusifika na elimu hii. Elimu yake haifichikani na chochote:

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ

“Na hushughuliki katika jambo lolote na wala husomi humo chochote katika Qur-aan, na wala hamtendi ‘amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo.” (10:61)

Mambo yote yaliyopo duniani na Aakhirah ni yenye kujulikana Kwake. Hakuna kinachofichikana Kwake (Jalla wa ´Alaa).

Kadhalika mambo haya yameandikwa. Pamoja na kuwa aliyajua akayaandika vilevile. Amesema (Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚإِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (22:70)

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umeandikwa katika Kitabu kabla Hatujauumba [huo msiba]. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (57:22)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amekadiria makadirio ya viumbe kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu khamsini na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”

Ameandika kila kitu kwenye Ubao uliohifadhiwa.

Daraja ya kwanza ya Qadar ndani yake kunaingia ngazi mbili:

a) Ujizi.

b) Uandishi.

Daraja ya pili ndani yake kunaingia mambo mawili:

a) Utashi

b) Uumbaji.

Matakwa ya Allaah ni yenye kutekelezwa. Anayotaka Allaah huwa na asiyotaka hayawi. Yeye ndiye Muumbaji wa kila kitu (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:29)

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

“Allaah Ndiye Muumbaji wa kila kitu.” (13:16)

Hakika Yeye (Subhaanah) aliyajua mambo, akayaandika na akayaumba. Anayotaka Allaah huwa na asiyotaka hayawi.

Na waja ndio wenye kutenda kihakika… – Waja ni wenye kutenda kihakika. Matendo wanayofanya yananasibishwa kwao. Mja ni mwenye kuswali, mwenye kufunga, mwenye kuhiji, mwenye kuzini, mwenye kuiba, yeye ndiye mwenye kuuza na kununua, mwenye kuoa na kutaliki. Allaah (Subhaanah) ndiye amewaumba na akaumba vilevile matendo yao. Amesema (Ta´ala):

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Na hali Allaah Amekuumbeni na yale mnayoyatenda.” (37:96)

Naye (Subhaanah) Anawapenda wachaji Allaah… Hakika Allaah (Subhaanah) anawapenda wachaji Allaah, watenda wema na waadilifu. Hawi radhi na watenda dhambi, hawapendi makafiri, haridhii juu ya waja wake kufuru na hapendi ufisadi. Anapenda kheri na watu wake, anachukizwa na shari na watu wake. Yeye anapenda imani na uchaji Allaah na wakati huo huo anachukia ufisadi, kufuru na upotevu. Kila mmoja ni mwenye kusahilishiwa kwa yale aliyoumbwa kwa ajili yake. Pindi Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliposikia hivi kwamba ikiwa mambo ni hivyo na matendo yao yameshaandikwa wakamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iko wapi basi haja ya kutenda? Akawaambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tendeni! Hakika kila mmoja ni mwenye kuwepesishiwa kwa yale aliyoumbiwa kwa ajili yake. Wenye furaha watawepesishiwa kutenda mambo ya watu wenye furaha. Kuhusiana na waangamivu watawepesishiwa kutenda matendo ya waangamivu.”[3]

Makadirio haya walikuwa wakiyakanusha al-Ghulaat al-Qadariyyah… – Hapo zamani Qadariyyah waliopindukia walikuwa wakipinga daraja ya kwanza ambayo ni elimu ya Allaah. Baada ya hapo wakajirejea kwa hilo. Leo wanaopinga hilo ni idadi ya watu wachache, kama ambavyo amesema mwandishi (Rahimahu Allaah). Hili ni kuhusiana na elimu ya Allaah juu ya kuyajua mambo na kuyaandika.

Aina hii ya Qadar wanaikanusha al-Qadariyyah wote… – Qadariyyah wengi wanapinga daraja ya pili ambayo inahusiana na Allaah kuyaumba mambo na kwamba matakwa Yake ni yenye kutekelezwa. Miongoni mwao ni Mu´tazilah na wengineo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaita wao kuwa ni:

“Waabudu moto wa Ummah huu.”

Waabudu moto ndio wenye kusema ya kwamba ulimwengu una waungu wawili:

a) Huyu ndiye mwenye kuumba mambo mazuri.

b) Huyu ndiye mwenye kuumba mambo mabaya.

Kadhalika watu hawa ni miongoni mwa ambao wamewashirikisha viumbe katika matendo yao na kusema ya kwamba viumbe ndio wenye kuumba matendo yao na kwamba matendo wayafanyayo hayakukadiriwa kwao. Wanasema kuwa wao wenyewe ndio wenye kuyafanya na Allaah hakuyaumba. Haya ni kutokana na ujinga na upotevu wao. Miongoni mwao kunaingia pia Mu´tazilah na Qadariyyah wakanushaji. Kusema kwao hivi ina maana wamemkadhibisha Allaah na Mtume Wake. Kwa ajili hiyo wamekuwa makafiri.

Na upande mwingine, katika wale wanaothibitisha Qadar, wamechupa mipaka… – Miongoni mwa Qadariyyah kuna wenye kuitwa Jabriyyah. Humo kunaingia pia Jahmiyyah na wenye kufanana nao wenye kusema kwamba mja ni mwenye kutenzwa nguvu na hana uwezo wala khiyari ya kutenda. Bali ametenzwa nguvu. Watu hawa wamepotea. Nao ni Jahmiyyah wenye kukanusha sifa za Allaah. Wamekusanya kati ya kukanusha sifa za Allaah na imani ya kutenzwa nguvu ambapo wanaamini kuwa mja ametenzwa nguvu na hawezi kutenda kwa khiyari. Mapote yote haya yamepotea kuanzia Jahmiyyah, Mu´tazilah, Qadariyyah wakanushaji na Shiy´ah al-Imaamiyyah kwa sababu na wao ni Mu´tazilah wenye kukanusha Qadar.

Makadirio haya yanafuata Elimu Yake (Subhaanah)… – Qadar ina ufafanuzi. Kuna Qadar iliyotangulia ambapo kumekadiriwa mambo ikiwa ni pamoja na kipomoko tumboni mwa mama yake, makadirio yanayokuwa kwenye usiku wenye cheo, makadirio yaliyotokea pindi alipoumbwa Aadam na Allaah akagusa kizazi chake kwenye mgongo wake. Haya ni makadirio ya ufafanuzi. Makadirio ya umri wa maisha, makadirio ya mwaka katika usiku wenye cheo na makadirio ya kila siku yote ni uufafanuzi wa Qadar iliyotangulia na yanarejea katika ile Qadar iliyotangulia. Kipomoko wala kiumbe kingine hakina namna ya kujitoa katika yaliyoandikwa kwenye Qadar iliyotangulia. Kwa ajili hii pindi Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ikiwa makazi yetu yamekwishajulikana ima Peponi au Motoni ni kwa nini basi tufanye matendo? Akawajibu kwa kuwaambia:

“Tendeni! Hakika kila mmoja ni mwenye kuwepesishiwa kwa yale aliyoumbiwa kwa ajili yake. Wenye furaha watawepesishiwa kutenda mambo ya watu wenye furaha. Kuhusiana na waangamivu watawepesishiwa kutenda matendo ya waangamivu.” Halafu akasoma maneno Yake (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ لَشَتَّى سَعْيَكُمْ إِنَّ

Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbalimbali. Basi yule anayetoa na akawa na taqwa na akasadikisha lililo jema, basi Tutamuwepesishia kwa mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na [anayejidhania kuwa] amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema, basi Tutamuwepesishia kwa magumu”. (92:04-10)

Huu ni utafiti mkubwa ambao unatakiwa kuhifadhiwa na kudhibitiwa kwa sababu unaenda kinyume na mapote yote ya Bid´ah na upotevu. Kwa I´tiqaad hii mtu anakuwa ni mwenye kwenda kinyume na mapote yote ya Bid´ah na upotevu ikiwa ni pamoja na Qadariyyah wakanushaji na Jabriyyah. Wote utakuwa ni mwenye kwenda kinyume nao na wewe utakuwa ni mwenye kuitakidi I´tiqaad ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] Ahmad (5/317), Abuu Daawuud (4700), at-Tirmidhiy (2155) na (3319). Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika kitabu cha Ibn Abiy ´Aaswim “Takhrij-us-Sunnah” (102-105).

[2] Abuu Daawuud (4691) na al-Haakim (1/85). Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) kasema kuwa ni Hasan katika kitabu cha Ibn Abil-´Izz al-Hanafiy ”Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah” (284).

[3] al-Bukhaariy (4945) na Muslim (2647)

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com