41. Hivi ndivyo Muhammad alikuwa Nabii na Mtume

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aliishi kwa umri wa miaka sitini na tatu, arubaini kabla ya utume na ishirini na tatu kama Nabii na Mtume. Alipewa unabii kwa [kupewa Suurah] “Iqra´” na akapewa utume kwa “al-Muddaththir”. Mji wake ni Makkah.

Allaah Amemtuma ili kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze! Na nguo zako zitwaharishe! Maambukizi yote ya kishirikina epukana nayo! Na wala usitoe kwa kwa kutaraji kukithirishiwa! Na kwa ajili ya Mola wako subiri!” (al-Muddaththir 74:01-07)

قُمْ فَأَنذِرْ

“Simama na uonye!”

maana yake ni kutahadharisha shirki na kulingania katika Tawhiyd.

وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ

“Na Mola wako mtukuze!”

Maana yake amtukuze kwa Tawhiyd.

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Na nguo zako zitwaharishe!”

Maana yake twahirisha matendo yako kutokana na shirki.

وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ

“Maambukizi yote ya kishirikina epukana nayo!”

Ni masanamu. Kuyakata, ina maana ya kuyaepuka na kujitenga nayo na watu wake.

MAELEZO

Mtume huyu mkubwa ambaye ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa Mtume kwa [Aayah] “Soma!”. Ya kwanza iliyoteremshwa kwake ni:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ

“Soma kwa Jina la Mola wako aliyeumba.” (96:01)

Hapa ndipo alikuwa Nabii. Wakati alipokuwa katika pango la Hiraa´ Jibriyl alimjia na kumuamrisha asome Suurah hii. Baada ya muda mfupi akamjia tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na “al-Muddaththir”. Ndipo akawa Mtume kwa maneno Yake:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ

”Ee uliyejigubika!”

Mara ya kwanza Jibriyl (´alayhis-Salaam) alipomjia alimuamrisha kusoma na akamkaba kwa nguvu ili kumwandaa juu ya jukumu na kazi kubwa ya kufikisha ujumbe. Akaogopa sana juu ya kumkaba kwake na akaenda nyumbani na kusema:

“Nigubikeni! Nigubikeni!”

Halafu Allaah akasema:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye!”

Simama na uwaonye watu! Ndipo akawa Mtume.

وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ

“Na Mola wako mtukuze!”

Bi maana muadhimishe kwa Tawhiyd.

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Na nguo zako zitwaharishe!”

Bi maana yasafishe matendo yako kutokamana na shirki. Aayah haitakiwi kufahamika kidhahiri kama ilivyo kwa kuwa wakati huo swalah ilikuwa bado haijafaradhishwa. Makusudio ya mavazi hapa ni matendo. Amesema (Ta´ala):

وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ

“… na vazi la uchaji Allaah ndiyo bora zaidi.” (07:26)

Matendo yanaweza kuitwa mavazi.

وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ

“Maambukizi yote ya kishirikina epukana nayo!”

Bi maana masanamu. Kuyaepuka maana yake ni kuachana nayo na kujitenga nayo mbali na watu wake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 03/02/2017