Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kurejea ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ

“Na rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake.” (az-Zumar 39 : 54)

MAELEZO

Kurejea (Inaabah) ni kule kurudi kwa Allaah (Ta´ala) kwa kumtii na kujiepusha kumuasi. Ni tamko ambalo liko karibu na maana ya Tawbah. Tofauti iliyopo tu ni kuwa tamko hili ni lepesi zaidi kutokana na kule kumtegemea Allaah.

Hafanyiwi yeyote isipokuwa Allaah (Ta´ala). Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ

“Na rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake.”

Makusudio ya:

 وَأَسْلِمُوا لَهُ

“… na jisalimisheni Kwake.”

ni ule Uislamu wa Kishari´ah ambao una maana ya kujisalimisha kwa hukumu za Allaah za Kishari´ah. Kwa sababu mtu anaweza kujisalimisha kwa Allaah kwa njia mbili:

1- Kujisalimisha kilimwengu. Ina maana mtu akajisalimisha na hukumu Zake za kilimwengu. Hili limeenea na kukizunguka kila kilichoko ndani ya mbingu na ardhi, muumini, kafiri, mwema na muovu. Haiwezekani kwa yeyote kuwa na kiburi kwa aina hii. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ

“… na hali Kwake amejisalimisha kila aliye katika mbingu na katika ardhi akipenda asipende na Kwake watarejeshwa.” (Aal ´Imraan 03 : 83)

2- Kujisalimisha Kishari´ah. Kujisalimisha huku ina maana mtu akajisalimisha na hukumu Zake za Kishari´ah. Aina hii ni maalum kwa wale Mitume na wafuasi wao wanaomtii. Kuna dalili nyingi ya hilo katika Qur-aan na moja wapo ni Aayah hii iliyotajwa na mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 61
  • Imechapishwa: 27/05/2020