41. Dalili juu ya kwamba Allaah yuko juu 2

41- Abu Muhammad bin Swaa´id na Muhammad bin Makhlad ametuhadithia: Ahmad bin Mansuur ar-Ramaadiy ametuhadithia: Yahyaa bin Ma´iyn na ´Aliy bin al-Madiyniy ametuhadithia (matamshi ni ya Yahyaa): Wahb bin Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Muhammad bin Ishaaq, kutoka kwa Ya´quub, kutoka kwa Jubayr bin Muhammad bin Jubayr bin Mutw´im, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake ambaye amesema:

“Kuna mbedui alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nafsi zinaangamia, familia zinakufa kwa njaa, mali zinaharibika na wanyama wanaangamia. Muombe Allaah atunyeshelezee. Tunakushufaia mbele ya Allaah na kwa Allaah (´Azza wa Jall) mbele yako.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ole wako! Hivi unajua unachokisema?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kumsabihi na kumtakasa Allaah kutokamana na mapungufu mpaka hilo likatambulika nyusoni mwa Maswahabah zake. Kisha akasema: “Ole wako! Hakushufaiwi kwa Allaah mbele ya yeyote katika waja Wake. Shani ya Allaah ni kubwa kuliko hivo. Ole wako! Unamjua Allaah ni nani? ´Arshi Yake iko juu ya mbingu na ardhi Yake iko hivi” na akavifanya vidole vyake mviringo na inatoa sauti kwa sababu Yake kama mfano wa kitanda cha yule mpandaji.”

ar-Ramaadiy amesema:

“Kuhusu ´Aliy bin al-Madiyniy hakutuhadithia yote. Aliishilia kwenye:

“Hakushufaiwi kwa Allaah mbele ya yeyote katika waja Wake.”

Ambaye alituhadithia yote ni Yahyaa bin Ma´iyn. Yahyaa bin Ma´iyn aliniandikia kwa hati yake ya mkono (na matamshi ni ya Ibn Makhlad).”

Hafsw bin ´Abdir-Rahmaan pia ameipokea kutoka kwa Muhammad bin Ishaaq kwa mlolongo wa wapokezi huu. Mwenye kusema kuwa imepokelewa kupitia kwa Ya´quub bin ´Utbah na Jubayr bin Muhammad amekosea. Usawa ni kwamba ni kupitia kwa Jubayr bin Muhammad, kama tulivyobainisha hapa.

  • Mhusika: Imaam ´Aliy bin ´Umar ad-Daaraqutwniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-us-Swifaat, uk. 87-88
  • Imechapishwa: 31/03/2018