28. Swawm ya ambaye anatokwa na damu nyingi kwenye majeraha


Swali 28: Mwanamke amepata majeraha katika ajali na mimba ilikuwa bado changa. Matokeo yake mimba ikaporomoka na akatokwa na damu nyingi. Je, inafaa kwake kufungua au aendelee na funga? Akifungua anapata dhambi?

Jibu: Mjamzito hapati dhambi, kama alivosema Imaam Ahmad:

“Si vyenginevyo wanawake hujua kuwa wameshika mimba kwa kukatika kwa hedhi.”

Hedhi, kama walivosema wanachuoni, Allaah ameiumba kwa hekima: kipomo kiweze kupata chakula tumboni mwa mama yake. Kukiibuka mimba basi hedhi inakatika. Lakini wako wanawake ambao wanaweza kuendelea kupata hedhi kama walivyozowea kabla ya kushika mimba. Huyu hukumu yake inazingatiwa kuwa ni ya kweli. Hedhi imemwendelea na haikuathiriwa na ujauzito. Hivyo hedhi hii itakuwa yenye kumzuia kwa kila kinachomzuia mwenye hedhi, inapelekea yale inayopelekea na inadondosha yale inayodondosha licha ya kuwa ni mjamzito.

Kwa ufupi ni kwamba kuna aina mbili ya damu inayomtoka mjamzito:

1 – Aina ambayo inahukumiwa kuwa ni hedhi. Hii ni ile ambayo imeendelea kama alivyokuwa kabla ya kushika ujauzito. Hiyo ina maana kwamba hedhi haikuathiri kitu na hivyo inakuwa ni hedhi.

2 – Damu iliyozuka kwa ujauzito uzukaji ambao umetokana na ajali, kubeba kitu, kuanguka na mfano wake. Damu hii sio hedhi. Ni damu inayotoka kwenye mshipa. Kujengea juu ya haya haimzuii kuswali wala kufunga. Bali hukumu yake ni kama ya wanawake wengine wasafi.

Lakini ajali hiyo ikipelekea kuporomoka kwa mtoto au kipomoko kilichoko tumboni mwake, basi mambo ni kama walivosema wanachuoni: kipomoko kikishuka na tayari kimeshakuwa na umbile la mwanadamu, basi damu baada ya kutoka kwake inazingatiwa kuwa ni nifasi. Ataacha kwa sababu ya damu hiyo swalah, swawm na mume wake atamwepuka mpaka asafike. Kipomoko kikitoka pasi na kuumbwa, basi haizingatiwi kuwa ni nifasi.  Hii ni damu fasidi isiyomzuia kuswali, kufunga na mambo mengine.

Wanachuoni wamesema kuwa muda wa chini kabisa ambapo kunabainika uumbaji wa kipomoko ni siku 81. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuhadithia – naye ni mkweli mwenye kusadikishwa, kwa kusema:

“Hakika umbo la kila mmoja wenu linakusanywa  pamoja katika tumbo la mama yake kwa muda wa siku arubaini. Kisha baadaye tone la damu kwa muda kama huo. Kisha tena huwa ni kipande cha nyama kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika ambaye anaamrishwa kuandika mambo mane; rizki yake, maisha yake, matendo yake na kama atakuwa ni mwenye furaha au mla khasara.”

Haiyumkiniki akaumbwa kabla ya hapo. Mara nyingi uumbaji haubainiki kabla ya siku tisini. Hivo ndivo walivosema baadhi ya wanachuoni.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 27/07/2021