40. Muislamu isikupite fursa hii kubwa


Kwa ajili hii imependekezwa kwa muislamu aamke mwishoni mwa usiku pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Anatakiwa awe macho huku akiswali, akiomba du´aa na akiomba msamaha. Hakika huu ni wakati ambapo du´aa inakubaliwa. Asilale katika wakati huu akajinyima nafsi yake. Hivi ndivyo wanavyofanya wengi walionyima ambapo wanakesha usiku mzima na inapofika mwishoni mwa usiku wanalala na kupitwa hata na swalah ya Fajr ambayo ni faradhi. Huku ni kunyimwa. Inatakikana kwa muislamu alale mapema na ajizoweze nafsi yake. Kila kitu ni kwa mazoezi. Lengo ni ili aweze kuamka mwishoni mwa usiku. Akijizoweza nafsi yake kufanya hivi atazowea. Lakini iwapo atajizoweza uzembe na kulala, basi itamkuwia uzito kuamka hata wakati wa swalah ya Fajr.

Haitakikani kwa muislamu akapitwa na fursa kama hii. Huu ni wito wa kiungu. Anatakiwa awepo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema kuhusu wanaomcha:

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

“Walikuwa wakilala kidogo tu usiku na kabla ya alfajiri wakiomba maghfirah.” (51:17-18)

وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ

“Na waombao maghfirah kabla ya alfajiri.” (03:17)

Kuomba msamaha kabla ya alfajiri ni kitendo kilicho na sifa ya kipekee kuliko nyakati zingine.

milango ya mbingu hufunguliwa – Bi maana hufunguliwa milango ya kujibiwa. Inatakikana kwa muislamu awepo wakati kama huu na aombe msamaha, atubie na kuomba. Kwani amefunguliwa milango ya kujibiwa. Hii ni fursa kubwa. Amesema (Rahimahu Allaah):

Husema “Tanabahini! Kuna mwombaji msamaha amuombae mghufiriaji

Bi maana zindukeni kwa kitachosemwa.

aombae msamaha – Imechukuliwa katika maneno Yake:

“Je, kuna anayeomba msamaha nimsamehe?”

na mwenye kuomba kheri… – Bi maana kuna anayemuomba Allaah (´Azza wa Jall) anachokitaka katika kheri sawa katika riziki na haja yoyote ile. Haja za watu zinatofautiana. Amuombe Allaah haja yoyote ile ilio na kheri kwake. Allaah hutoa zaidi katika wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule.

Hakika Allaah (Jalla wa ´Alaa) yu karibu na ni Mwenye kujibu. Anaikubali tawbah na anasamehe madhambi katika nyakati zote. Lakini zipo nyakati ambazo ni maalum ambapo kuna matarajio zaidi ya kujibiwa. Moja wapo ni wakati huu. Mfano mwingine ni saa iliopo siku ya Ijumaa. Kuna nyakati ambazo kujibiwa kunakuwa karibu zaidi. Kwa mfano katika Sujuud. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake katika hali ya kusujudu.”[1]

Kadhalika katika hali ya safari:

“… anarefusha safari yake nywele timtim. Ananyoosha mikono yake… “[2]

Vilevile katika hali ya kudhikika:

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ

“Ni nani anayemuitika aliyedhikika anapomwomba.” (27:62)

Kuna nyakati na hali ambazo kuna matarajio makubwa ya kujibiwa kuliko nyakati na hali zingine. Vinginevyo Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasikia, anasamehe, anatunuku, anasikia du´aa na anajibu katika kila wakati usiku na mchana.

… na riziki apewe – Ni vipi mtu atajikosesha haya na akalala? Atafaidika nini na kulala? Ni vipi ataghafilika na kuendekeza upuuzi wa TV na Intaneti. Utamuona mtu ametulizana hali ya kuyakodoa macho hatikisiki na sanamu hili chafu na wala hachoshwi kabisa na anampuuza Mola Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) anajikosesha kheri hii nyingi ambayo yeye ni mwenye kuihitaji sana. Hakuna mwenye kuweza kujitosheleza na Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa muda wa kukapua macho. Ni vipi mtu anaweza kupuuza haya na asiyatilie umuhimu?

Pengine vilevile akafuata madhehebu ya Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah akakadhibisha, akapinga na kupuuza kushuka huku. Huyu anayepinga ni mbaya zaidi kuliko ambaye hapuuzi na wala hapingi. Lau kama kuna wakati fulani ambapo kunagawiwa pesa au kumefunguliwa mchango katika shirika na huku wanatarajia katika wakati huo kupata faida, mnaonaje watu watafanya nini? Hawatosongamana? Bali tumefikiwa na khabari kwamba watu hupigana kwa sababu ya msongamano kwa ajili ya kutafuta dunia itayoisha ambayo huenda mtu akaipata na huenda asiipate. Na kama mtu ataipata huenda ikawa ni shari na balaa kwa mwenye nayo. Huenda vilevile mchango huu ukawa ni haramu na ndani yake mna ribaa na kamari. Pamoja na haya yote watashindana na kupigana kwa ajili yake. Wataenda mapema kabla ya mambo kuanza ili kila mmoja awe karibu na nafasi hiyo na asiwe mbali. Ikiwa mambo ni namna hii katika jambo la kidunia ni vipi mtu atapuuza jambo la Aakhirah ambalo halihitaji msongamano na limejaa kheri tupu na hakuna msongamano, mashindano, fujo na vurugu? Ni vipi mtu atapuuza haya na kwenda katika jambo ambalo hajui kuwa ni kheri au shari? Bila shaka katika zama hizi liko karibu zaidi na shari. Wakati huu watu wengi wamekuwa hawaangalii halali na haramu. Hakika shari na fitina ya mali leo ni kubwa. Pamoja na hivyo watu wanapigana kwayo. Ni vipi basi watu wanaghafilika na fursa kama hii kubwa pamoja na Allaah (´Azza wa Jall) – ambaye ni mkarimu sana na mwenye huruma sana na ambaye hakuna yeyote awezae kujitosheleza Naye kwa muda wa kukapua macho – ambayo amewafungulia? Allaah hahitajii kwao wakeshe usiku mzima wakifanya ´ibaadah. Bali Yeye (Subhaanah) hushuka sehemu ya mwisho ya usiku kabla ya Fajr. Unaweza kuamka muda kidogo tu kabla ya Fajr ili uweze kushuhudia wakati huu mkubwa. Iwapo utaamka mapema ndio bora zaidi. Isikupite fursa kama hii kubwa na ukaghafilika nayo. Huenda huu ukawa ndio uhai wako wa mwisho na usiudiriki huko mbeleni. Maadamu uko katika wakati ambapo uko na uwezo na uko na faragha si mwenye kushughulishwa, usiipoteze fursa hii kubwa.

Kuna mwombaji msamaha… – Ni kuomba maghfirah.

… amuombae mghufiriaji – Naye ni Allaah (Jalla wa ´Alaa). Miongoni mwa majina Yake ni msamehevu (Ghaffaar/Ghafuur/Dhul-Maghfirah). Haya ni majina ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Ni yule ambaye anasitiri madhambi. Maana ya jina hili ni kusitiri. Anayasitiri madhambi kwa kuyasamehe na kutoyachukulia.

na mwenye kuomba kheri – Ni kuomba neema. Imechukuliwa katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akielezea juu ya Mola wake aliposema:

“Je, kuna mwenye kuomba nimpe?”

[1] Muslim (215) na (482)

[2] Muslim (65) na (1015)