40. Kile tunachokijua


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hawakizunguki chochote katika elimu Yake isipokuwa kile Anachokitaka. Kursiy Yake imezienea mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo.

MAELEZO

Dalili ya kutofikiria juu ya dhati ya Allaah ni:

وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ

“Wala hawakizunguki chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa akitakacho.”[1]

Elimu ya Allaah ni pana. Sisi hatujui juu Yake isipokuwa yale aliyotufunza. Vivyo hivyo ndivo walivosema Malaika kumwambia Allaah:

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

“Utakasifu ni Wako hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika wewe ni Mjuzi wa kila jambo, Mwenye hekima wa yote.”[2]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) alisema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَأَنزَلَ اللَّـهُ عَلَيْكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُن تَعْلَمُ

“Allaah amekuteremshia Kitabu na Hekima na akakufunza yale ambayo hukuwa unayajua.”[3]

وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا

“Sema: ”Mola wangu! Nizidishie elimu.”[4]

Kile ambacho Allaah amewafunza viumbe, wanakiweza, na kile ambacho hakuwafunza, basi wanatakiwa kuchukua msimamo wa kukomeka na wasijiingize ndani yake. Kile wanachokijua ni kitu kichache ukilinganisha na elimu ya Allaah. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا

“Wanakuuliza kuhusu roho. Sema: “Roho ni katika amri ya Mola wangu” na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu.”[5]

Elimu kamilifu yuko nayo Allaah (´Azza wa Jall). Elimu yetu ni ndogo ukilinganisha na elimu ya Allaah (´Azza wa Jall). Hatuwezi kukizunguka chochote katika elimu Yake isipokuwa kile Anachokitaka na akatufunza nacho kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´akayhi wa sallam):

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ

”Mjuzi wa mambo yaliyofichikana na wala hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake, isipokuwa yule aliyemridhia ambaye ni Mtume.”[6]

Anamfanya Mtume (Swalla Allaahu ´akayhi wa sallam) kujua kile akitakacho katika mambo ya ghaibu, kwa sababu ya manufaa kwa watu na kuwabainishia watu. Hiki ni kitu kinachojulikana juu ya ´Aqiydah ya muislamu. Wale wanaodai kuwa wanajua kila kitu na kwamba wanayo elimu isiyokuwa na kikomo na wanajifakharisha kwa jambo hilo, ni waongo. Hakuna wanachokijua isipokuwa tu kichache katika kile ambacho Allaah amewafanya kukijua – na kile wasichokijua ni kikubwa na mengi zaidi.

[1] 2:255

[2] 2:32

[3] 04:113

[4] 20:114

[5] 17:85

[6] 72:26-27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 34
  • Imechapishwa: 27/07/2021