40. Du´aa wakati wa kuzaa


168- Abu Raafiy´ (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiadhini kwenye sikio la al-Hasan bin ´Aliy baada ya Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anha) kumzaa.”

169- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) amesema:

“Watoto wenye kuzaliwa walikuwa wakiletwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwaombea baraka na kuweka tende nyevu vinywani mwao ambayo kishaitafuna.”

170- ´Amr bin Shu´ayb amepokea kutoka kwa baba yake ambaye amepokea kutoka kwa babu yake ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha mtoto mwenye kuzaliwa kupewa jina, kunyolewa na kuchinjiwa siku ya saba.”[1]

171Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa jina mtoto wake Ibraahiym, Ibraahiym mtoto wa Abu Muusa, ´Abdullaah mtoto wa Abu Twalha na al-Mundhir mtoto wa Abu Usayd karibu tu baada ya kuzaliwa.”[2]

172- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Majina yenu yanayopendwa zaidi na Allaah ni ´Abdullaah na ´Abdur-Rahmaan.”

173- Katika Hadiyth nyingine kumezidishwa:

“Majina ya kikweli kabisa ni Haarith na Hamaam na majina mabaya kabisa ni Harb na Murrah.”

174- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibadilisha majina mabaya kwenda katika majina mazuri. Zaynab alikuwa anaitwa Barrah (mwema). Kukasemwa kuwa anajisifu mwenyewe, hivyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalibadilisha na kuwa Zaynab. Alikuwa anachukia kukisemwa kwamba mtu ametoka Barrah. Alimuuliza mtu anaitwa nani. Mtu yule akasema kuwa anaitwa Hazan (huzuni). Hivyo akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Wewe unaitwa Sahl.” Alibadilisha jina la ´Aaswiyah (muasi) na akampa badala yake jina la Jamiylah. Alimuuliza mtu mwengine anaitwa nani. Mtu yule akasema Aswram (mwenye kudungwa). Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Wewe unaitwa Zur´ah.” Alibadilisha jina la ardhi ´Afrah (vumbi) na kuipa Khadhwirah.

[1] Yaani nywele zake zitanyolewa siku ya saba sawa ikiwa ni mvulana au msichana. Hali kadhalika mvulana atachinjiwa kondoo mbili na msichana kondoo mmoja.

[2] Mapokezi haya ni Swahiyh. Hii ni dalili inayoonesha kuwa kitendo hichi kinajuzu lakini bora zaidi ni siku ya saba.

 

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 106-108
  • Imechapishwa: 21/03/2017