40. Dalili ya thelathini na nane kutoka katika Sunnah kwamba Allaah yuko juu ya viumbe


38- Muhammad ametukhabarisha: Ahmad bin al-Hasan ametuhadithia: Abu ´Aliy bin Shaadhaan ametuhadithia: Abu Sahl Ahmad bin Muhammad bin ´Abdillaah bin Ziyaad ametuhadithia: Ahmad bin Muhammad bin ´Iysaa al-Barqiy ametuhadithia: Yahyaa (al-Himaaniy) ametuhadithia: Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbali na wale Malaika wanaoandika matendo ya watu Allaah anao Malaika wanaozunguka ardhini. Wanapowapata watu wanaomdhukuru Allaah (Ta´ala) wanaita: “Njooni katika utashi wenu!” Kisha wanawazunguka. Wanapotawanyika wanapanda mbinguni ambapo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anasema: “Mmewaacha waja wangu wanafanya nini mlipowaacha?” Wanasema: “Tumewaacha wanakuhimidi, wanakutukuza na wanakutaja.” Ndipo aseme: “Kwani wamekwishaniona?” Wanasema: “Hapana.”Aseme: “Vipi lau wangeniona?” Waseme: “Lau wangekuona basi wangekuhimidi, kukutukuza na kukutaja kwa wingi kulikoni.”Aseme: “Kwani wanatafuta nini?” Waseme: “Wanatafuta Pepo.” Aseme: “Wamekwishaiona?” Waseme: “Hapana.”Aseme: “Vipi lau wangeiona?”Waseme: “Wangeiona basi wangelikuwa na bidii zaidi kulikoni.”Aseme: “Wanajilinda kutokamana na nini?” Waseme: “Wanajilinda kutokamana na Moto.”Aseme: “Kwani wamekwishauona?” Waseme: “Hapana.” Aseme: “Vipi wangeuona?” Waseme: “Wangeuona basi wangeukimbia na kujilinda nao zaidi kulikoni.”Ndipo aseme: “Mimi nakushuhudisheni kwamba nimewasamehe.” Waseme: “Wako ambao wameingia kimakosa. Wameingia humo kwa ajili ya tu haja.”Aseme: “Ni watu ambao matangamano yao si yenye kula khasara. Ni watu ambao matangamano yao si yenye kula khasara.”[1]

[1] al-Bukhaariy (6408), Muslim (4689) na at-Tirmidhiy (3600).

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 18/06/2018