Ee Muislamu! Utapofahamu haya basi utambue kuwa kila ambaye atazua Shari´ah ndani ya dini ya Allaah, hata kama atakuwa na nia nzuri, basi Bid´ah yake hii – mbali na kwamba ni upotofu – ni kuitukana dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Isitohe anayakadhibisha maneno Yake Allaah (Ta´ala) pale aliposema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu.”

Kwa sababu mzushi huyu ambaye amezua Shari´ah ndani ya dini ya Allaah (Ta´ala) isiyokuwemo anasema japo kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja ya kwamba dini haijakamilika na kwamba inahitajia Shari´ah hii ambayo amezusha ili kujikurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jall).

La kushangaza ni kwamba utaona jinsi mtu anavyothubutu kuzua kitu chenye kuhusiana na dhati ya Allaah (´Azza wa Jall), majina na sifa Zake na kudai kuwa anafanya hivyo kwa kumuadhimisha Mola Wake, kumtakasa na kasoro na mapungufu na kujisalimisha na maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا

“Basi msimfanyie Allaah washirika.”[1]

Utashangazwa na mtu anayezua Bid´ah yenye kufungamana na dhati ya Allaah ambayo Salaf wala maimamu wa dini hawakuitendea kazi na anasema kuwa anafanya hivo kwa ajili ya kumtakasa Allaah na kasoro na mapungufu, kumuadhimisha na kujisalimisha na maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا

“Basi msimfanyie Allaah washirika.”

Kisha isitoshe anasema mwenye kwenda kinyume ni mwenye kumfananisha na kumshabihisha Allaah na viumbe Wake na tuhuma nyinginezo mbaya.

Utashangazwa mwenyewe kuona watu wenye kuzusha ndani ya dini ya Allaah mambo yasiyokuwemo yenye kufungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwa kufanya hivo wanadai kuwa wanampenda na kumuadhimisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isitoshe ukiongezea juu ya hilo wanasema kuwa yule asiyekubaliana na wao juu ya Bid´ah zao anamchukia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tuhuma nyinginezo mbaya.

Chenye kushangaza ni kwamba watu hawa wanasema kuwa wanamuadhimisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakati huohuo bila ya shaka ni wenye kutangulia mbele ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi wanapozua katika dini ya Allaah na Shari´ah ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yasiyokuwemo. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Enyi mlioamini! Msitangulie mbele ya Allaah na Mtume Wake, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.”[2]

[1] 02:22

[2] 49:01

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 5-6
  • Imechapishwa: 23/10/2016