4. Mfano wa nne kuonyesha kuwa Raafidhwah ni Baatwiniyyah

4- al-´Ayyaashiy (02/123) amesema:

“Jaabir ameeleza kuwa alimuuliza Abu Ja´far kuhusu tafsiri ya Aayah:

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ ۖ فَإِذَا جَاءَ رَسُولُهُمْ قُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Na kila ummah [Tulituma] Mtume. Basi anapokuja Mtume wao [kwa watu wao] inakidhiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa.” (10:47)

Abu Ja´far akasema:

“Tafsiri yake iliyojificha ni kwamba kila karne katika Ummah huu ina Mtume kutoka katika watu wa familia ya Muhammad. Hujitokeza katika karne ambayo ametumwa kama Mtume. Wao ni mawalii na ni Mitume.

Ama Kauli Yake:

“… inakidhiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa.”

maana yake ni kwamba Mtume atahukumu kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa.”

Mhakiki ameelekeza katika “al-Burhaan”, “al-Bihaar” na “Swaafiy”.

Angalia upotoshaji huu uliyojengwa juu ya mfumo wa Baatwiniyyah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Anaeleza jinsi Ummah zilizotangulia zilivyoangamia kwa sababu ya kuwakadhibisha Mitume wao kama mfano wa watu wa Nuuh, watu wa Huud, watu wa Swaalih na Ummah zingine ambazo ziliwakadhibisha Mitume wao. Allaah Huadhibu kila Ummah pale wakati wake Aliyoupanga unapowadia. Allaah Anaeleza hilo ili watu waweza kupata mafunzo juu ya watu waliyoangamia ili waweze kujiepusha na sababu za maangamivu. Ndipo Baatwiniyyah wanapokuja ili kupotosha Kitabu cha Allaah kwa mfumo wao wa ki-Baatwiniy ili iweze kuenda sambamba na ´Aqiydah yao na kuwafanya maimamu, ambao ni watu kutoka katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwa Mitume; kila imaam ni Mtume wa karne aliyoishiemo. Hili vilevile linafutilia mbali ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Nabii na Mtume wa mwisho.

Tazama mara nyingine jinsi anavyofuta dalili ya Kauli ya Allaah:

“… basi anapokuja Mtume wao [kwa watu wao] inakidhiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa.”

na kuwafanya Mitume – bi maana maimamu wao – wao ndio watakidhi baina yao kwa uadilifu. Atayekidhi kwa uadilifu kati ya Mitume na Ummah zao zilizowakadhibisha ni Allaah Pekee. Maamuzi na hukumu Yake juu ya Ummah za makafiri kuangamia na kuharibika si jengine isipokuwa ni uadilifu. Si maimamu wala mwengine yeyote hatohukumu kwa lolote. Kwa sababu hawamiliki juu ya nafsi zao wenyewe wala nasfi za wengine madhara wala manufaa.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 18/03/2017