39. Thawabu juu ya kumuosha maiti na sharti zake


30- Kwa yule anayesimamia kumuosha maiti ana ujira mkubwa kwa sharti mbili:

La kwanza: Amsitiri na wala asiseme kile anachoweza kukiona katika mambo yanayochukiza. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kumuosha muislamu akamnyamazia (zile aibu zake), basi Allaah atamsamehe mara arubaini, yule mwenye kumchimbia (shimo la kaburi) ambapo akamsitiri, basi atapitishiwa ujira kama mfano wa ujira wa aliyemjengea nyumba mwengine hadi siku ya Qiyaamah na yule mwenye kumvisha sanda, basi Allaah na yeye atamvisha sanda siku ya Qiyaamah kutokana na hariri nyororo na hariri nzito ya Peponi.”

Ameipokea al-Haakim (01/354,362), al-Bayhaqiy (03/395) na al-Aswbahaaniy katika “at-Targhiyb” (01/235) kupitia kwa Abu Raafi´ (Radhiya Allaahu ´anh). al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Mambo ni kama alivosema.

at-Twabaraaniy ameipokea katika “al-Kabiyr” kwa tamko lisemalo:

“… dhambi arubaini.”

al-Mundhiriy (04/171) amesema na akafuatiwa na al-Haythamiy (03/21):

“Wapokezi wake ni wenye kutumiwa kama hoja katika “as-Swahiyh”.

al-Haafidhw Ibn Hajar amesema katika “ad-Diraayah” (140):

“Cheni ya wapokezi wake ni yenye nguvu.”

La pili: Afanye kazi hiyo kwa kutafuta malipo ili aone uso wa Allaah. Malengo yake isiwe kutafuta malipo, shukurani wala chochote katika mambo ya kidunia. Hilo ni kutokana na yale yaliyothibitishwa katika Shari´ah kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hakubali kutoka katika ´ibaadah isipokuwa yale yaliyofanywa kwa ajili ya kutafuta uso Wake mtukufu. Dalili juu ya hilo kutoka katika Qur-aan na Sunnah ni nyingi sana. Nitatosheka hapa na kutaja sita katika hizo:

1- Maneno Yake (Tabaarak wa Ta´ala):

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَى إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

”Sema: “Hakika mimi ni mtu [wa kawaida] kama nyinyi. Nafunuliwa Wahy kwamba hakika mwabudiwa wenu wa haki ni Mungu mmoja pekee. Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[1]

Bi maana hakusudii jengine zaidi ya uso wa Allaah (Ta´ala).

2- Vilevile amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini.”[2]

3- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kutokana na kile alichonuia. Yule ambaye kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, basi kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya Allaah na Mtume. Yule ambaye kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya dunia au mwanamke anayetaka kumuoa, basi kuhajiri kwake kutakuwa kwa lile aliloliendea.”

Ameipokea al-Bukhaariy mwanzoni mwa “as-Swahiyh” yake, Muslim na wengineo kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh).

4- Vilevile amesema:

“Ubashirie Ummah huu kuinuliwa daraja, kumakinishwa katika miji, kunusuriwa na kupandishwa juu ya duniani. Yule miongoni mwao mwenye kufanya kitendo cha Aakhirah kwa ajili ya dunia, basi hana fungu huko Aakhirah.”

Ameipokea Ahmad na mtoto wake katika Zawaa-id “al-Musnad” (05/134), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (al-Mawaarid) na al-Haakim (04/311) na amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye na al-Mundhiriy (01/31) akamkubalia.

 Cheni ya ´Abdullaah ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy.

5- Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mtu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unaonaje mtu ambaye amepigana vita akitafuta ujira na kusifiwa ana nini?” Akasema: “Hana kitu. Akamrudilia mara tatu ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamjibu: “Hana kitu.” Kisha akasema:

“Hakika Allaah hakubali katika matendo isipokuwa yale yanayofanywa kwa ajili Yake pekee na kutafuta uso Wake.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (02/59) na cheni ya wapokezi wake ni nzuri kama alivosema al-Mundhiriy (01/24).

6- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Hakika Mimi nimejitosheleza kabisa kutokamana na shirki. Hivyo basi, yule atakayetenda tendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi Mimi nimejiweka nalo mbali kabisa na ni la yule aliyenishirikisha naye.”

Ameipokea Ibn Maajah katika “az-Zuhd” kupitia kwa Abu Hurayrah na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.  Ameipokea vilevile katika “as-Swahiyh” yake (08/223) na wengineo.

[1] 18:110

[2] 98:05

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 69-71
  • Imechapishwa: 18/02/2020