39. Shubuha ya tatu ya watu wa Tawassul na majibu juu yake

3- Shubuha ya tatu: Hao wanaofanywa kukaa katikati ni watu wema na wana nafasi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa hiyo sisi tunamuomba Allaah kupitia wao. Kwa sababu sisi ni wenye madhambi. Lakini watu hawa ni waja wema na wana nafasi mbele Allaah (Jalla wa ´Alaa). Sisi tunachowaomba ni watukurubishe kwa Allaah na watuombee kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Jibu ya hilo ni kwamba, wema na matendo mema ya watu wengine ni yenye kuwastahikia wao na ni matendo yao wao na wewe hayakufai lolote isipokuwa matendo yako mwenyewe. Ikiwa wewe huna matendo, basi tambua kuwa watu hawa hawatokufaa kitu:

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًا

”Siku ambayo nafsi yoyote ile haitoimilikia nafsi nyingine kitu chochote.” (al-Infitwaar 82:19)

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ وَأُمِّهِ وَأَبِيهِوَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ  لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ

”Siku mtu atakapomkimbia nduguye na mama yake na baba yake na mkewe na wanawe – kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza.” (´Abasa 80:34-37)

Wema wao hautokufaa kitu. Maadamu wewe huna wema wowote na wala matendo mema, basi wema wa wengine hautokufaa kitu. Hakuna kitachokufaa zaidi ya matendo yako. Kwa nini basi wewe usifanye matendo yako mpaka nawe uwe mwema na uwe karibu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)? Ama kusema kwamba wema wa wengine ukukurubishe wewe kwa Allaah ni katika upumbavu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُم مَّا كَسَبْتُمْۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Huo ni ummah kwa hakika umeshapita, una uliyoyachuma nanyi mna mliyoyachuma. Wala hamtoulizwa juu ya yale waliyokuwa wakitenda.”(al-Baqarah 02:141)

Hautokufaa kitu wema wao, ukaribu wao kwa Allaah ikiwa wewe huna matendo yako mema na juu ya ´Aqiydah iliosalimika. Hawatokufaa kitu kamwe. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wa waombezi wowote.” (al-Muddaththir 74:48)

Mshirikina hautokubaliwa uombezi wake. Kumfanyia ´ibaadah mwingine asiyekuwa Allaah ni shirki ijapokuwa utadai ya kwamba unawaabudu ili wakuombee kwa Allaah, bado wewe ni mshirikina na mshirikina hautomfaa kitu uombezi. Ni wajibu kwako kuyarekebisha matendo yako kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Usijishughulishe na matendo ya wengine. Hayo ni ya kwao wao na wewe hakuna kitachokufaa isipokuwa matendo yako mema. Ikiwa huna matendo mema, hakuna yeyote atakayekufaa kwa matendo yake hata akiwa ni jamaa wa karibu sana kwako.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 09/08/2018