39. Mwenye busara na hasira


1 – Jaabir amesema:

”Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nifunze jambo ambalo litaniingiza Peponi. Usinambie mengi pengine nisije kufahamu.” Akasema: ”Usikasirike.”

2 – Watu wenye akili bora zaidi ni wale wasiokasirika. Watu wenye jibu lililoandaliwa vyema ni wale wenye kukasirika.

3 – Hasira za haraka unaidhuru zaidi akili kuliko moto unavyochoma nyasi. Anayekasirika inapotea akili yake na hivyo akasema kile akili yake imempendeza na akafanya kile kinachomfanya kuonekana mbaya.

4 – Wuhayb amesema:

”Imeandikwa katika Injiyl yafuatayo: ”Ee mwanadamu! Nikumbuke pale unapokasirika Nami nitakukumbuka pale Ninapokasirika.”

5 – Hasira za haraka ni katika sifa za wapumbavu. Kuziepuka ni katika sifa za wenye busara.

6 – Hasira ni jeraha la majuto. Mtu ana wepesi zaidi wa kurekebisha yale aliyoharibu kabla hajakasirika kuliko anavoweza baada ya kukasirika.

7 – Bakkaar bin Muhammad amesema:

”Ibn ´Awn alikuwa hakasiriki. Anapomkasirisha mtu basi humwambia: ”Allaah akubariki!”

 8 – Abu Sa´iyd amesema:

”Pindi ´Awn bin ´Abdillaah bin ´Utbah alipokuwa akimkasirikia mtumwa wake alikuwa akimwambia: ”Ni wingi uliyoje kufanana na bosi wako! Unaniasi na mimi namuasi Allaah.” Wakati hasira zake zinapozidi basi husema: ”Wewe uko huru kwa ajili ya Allaah.”

9 – Kila pale ambapo mwenye busara anapoona kitu kinachomchukiza basi ni wajibu kwake kukumbuka ni wingi uliyoje anavomuasi Mola wake na namna Allaah anavyomfanyia upole licha ya yote hayo. Baada ya hapo zitapungua hasira zake naa wala hakutompelekea yeye kufanya jambo ambalo halistahiki kufanywa na wale wenye busara. Aidha atalipwa thawabu huko Aakhirah kwa sababu ya kuwa katika wenye kusubiri na kuacha kukasirika.

10 – Kama hasira isingelikuwa na sifa mbaya zaidi ya, kwa mujibu wa baadhi ya wanamme wenye hekima, kwamba anakuwa hana lolote la kusema basi ingelikuwa inatosha kujiepusha nayo kwa kila njia.

11 – Hakuna mwanachuoni yeyote aliyempa udhuru ambaye amemtaliki mkewe au kumwacha huru mtumwa wake katika hali ya hasira.  Hata hivyo wapo wanazuoni waliyompa udhuru ambaye amemtaliki mkewe au kumwacha huru mtumwa wake katika hali ya ulevi.

12 – Katika maumbile ya kiumbe ni kuwa na hasira na upole vyote viwili. Ambaye atakasirika na akawa mpole katika hiyohiyo hasira, basi hajafanya kitu chenye kusemwa vibaya muda wa kuwa ghadhabu hiyo haijampelekea kufanya au kusema kitu cha kuchukiza. Hata hivyo ni jambo lenye kusifiwa zaidi kuepuka hasira daima.

13 – ´Abdul-Malik bin Marwaan amesema:

”Mtu asiyeghadhibika basi hawi mpole kwa sababu upole hautambuliki isipokuwa wakati wa hasira.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 138-141
  • Imechapishwa: 07/08/2021