Swali 39: Naomba maelezo ya Hadiyth hii: Kutoka kwa as-Saaib bin Yaziyd, kutoka kwa Mu´aawiyah ambaye amesema:

“Utakaposwali ijumaa basi usiiunganishe pamoja na swalah nyingine mpaka utapoongea au utoke nje. Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha hivo tusiunganishe swalah na swalah nyingine mpaka tuongee au tutoke nje.”[1]

Jibu: Hadiyth hii ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake. Inafahamisha kuwa muislamu atakaposwali ijumaa au swalah za faradhi nyingine, basi haifai kwake akaiunganisha na swalah nyingine mpaka azungumze kwanza au atoke nje ya msikiti. Kuzungumza kunakuwa kwa yale ambayo Allaah ameyawekea Shari´ah kama mfano wa kusema:

أستغفر الله. أستغفر الله. أستغفر الله. اللهم أنت السلام ومنك السلام تباركت يا ذا الجلال والإكرام

 “Namwomba Allaah msamaha. Namwomba Allaah msamaha. Namwomba Allaah msamaha. Ee Allaah! Wewe ndiye as-Salaam, amani inatoka Kwako, umebarikika, Ee Mwenye utukufu na ukarimu.”

pindi anapotoa Tasliym na aliyoweka katika Shari´ah Allaah baada ya hapo katika aina mbalimbali za Dhikr. Akifanya hivo itapata kubainika wazi kujitenga kwake na swalah ili asije kudhani mtu kwamba swalah hii ya pili ni sehemu ya ile swalah ya kwanza.

Kinacholengwa kwa kufanya hivo ni kutofautisha swalah aliyomaliza kutokamana na swalah nyingine. Akitoa Tasliym kutokamana na ijumaa basi asiiuganishe na swalah ya sunnah ili asije kudhani yeye au mwengine kwamba imefungamana nayo au ni yenye kulazimiana nayo. Vivo hivyo inahusiana na swalah nyenginezo kama vile Dhuhr, ´Aswr, Maghrib, ´Ishaa na Fajr ni lazima kuzipambanua kwa maneno kama vile Dhikr au maneno mengine au kutoka nje ya msikiti ili ifahamike kuwa haikufungamana na ilioko kabla yake.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/335-336).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 78-79
  • Imechapishwa: 04/12/2021